Jumamosi, 12 Septemba, 2026
Leo ni Jumamosi 30 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1448 Hijria mwafaka 12 Septemba 2026 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 129 iliyopita, inayosadifiana na 12 Septemba 1897, Irene Joliot- Curie mtaalamu wa fizikia na kemia wa Ufaransa, alizaliwa katika mji wa Paris. Baada ya kufanya utafiti wa muda mrefu, Irene Joliot- Curie alifanikiwa kuvumbua mada za nunurishi au radioactive. Baadaye akishirikiana na mmoja wa wasaidizi wa mama yake, mwanafizikia huyo alifanya utafiti na uhakiki katika uga huo na kupata mafanikio makubwa. Irene Joliot-Curie aliaga dunia 1957.
***
Miaka 106 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, Sheikh Muhammad Khiyabani, mwanazuoni mwanamapambano na mujahidi aliyekuwa muungaji mkono wa harakati za kupigania katiba nchini Iran aliuawa shahidi. Sheikh Muhammad alizaliwa mwaka 1297 Hijria huko Khameneh, katika eneo la Azerbaijan Mashariki. Baadaye alielekea Tabriz ambako alijishughulisha na masomo ya elimu za dini. Tofauti na wanafunzi wengine wa elimu ya dini ambao walijitosheleza kwa kujifunza fiqhi na usul al-fiqhi, Muhammad Khiyabani alijifunza hisabati, falsafa, elimu za kimaumbile, historia na fasihi. Baada ya ushindi wa harakati za kupiganmia katiba nchini Iran mwaka 1285 Hijria Shamsia, na kuanzishwa Baraza la Mkoa huko Tabriz, maisha ya Sheikh Muhammad Khiyabani yaliingia katika hatua mpya. Katika zama zake, hali ya ulimwengu wa Kiislamu, na hasa Iran, ilikuwa imevurugika sana na ya kusikitisha kutokana na uingiliaji wa mataifa ya kigeni, yakiwemo Urusi, Uingereza na Ujerumani. Baada ya Muhammad Ali Shah kuondolewa madarakani nchini Iran, Khiyabani akiwa na umri wa miaka 30, alichaguliwa kuwa mwakilishi wa wananchi wa Tabriz katika Bunge la Taifa.
***
Katika siku kama ya leo miaka 52 iliyopita, nchini Ethiopia kulitokea mapinduzi yaliyopelekea kuondolewa madarakani utawala wa Haile Selassie na mwaka mmoja baadaye utawala wa kifalme ulikomeshwa kabisa nchini Ethiopia. Haile Selassie alizaliwa mwaka 1892 nchini Ethiopia. Awali alikuwa mkuu wa mikoa kadhaa nchini humo na baadaye akawa mrithi wa kiti cha ufalme. Mwaka 1930 alishika hatamu za uongozi wa Ethiopia akiwa mfalme wa nchi hiyo. Awali alifanya jitihada kubwa za kuyaunganisha makabila ya Ethiopia kwa shabaha ya kuyadhibiti. Haile Selassie aliwaajiri wataalamu wa kigeni na kuanza kufanya marekebisho ya kiidara hatua kwa hatua. Alikomesha utumwa, akafanya marekebisho ya masuala ya kifedha na kuanzisha mfumo wa mahakama nchini Ethiopia. Hata hivyo mashambulio ya Italia dhidi ya Ethiopia mwaka 1935 yalisitisha mpango wake huo na alibakia nje ya nchi hadi mwaka 1941 aliporejea nchini kwa msaada wa Waingereza na kutwaa tena madaraka. Aliendeleza marekebisho yake ambayo zaidi yalijikita katika mji mkuu Addis Ababa na mambo yasio ya msingi huku sehemu kubwa ya Waethiopia wakikosa suhula za kimsingi za maisha. Selassie alikuwa tegemeza sana kwa nchi za Magharibi.
***
Miaka 46 iliyopita katika siku kama ya leo, nchini Uturuki kulitokea mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Jenerali Kenan Evren na kupelekea kuondolewa madarakani Waziri Mkuu Suleyman Demirel na kisha kuundwa serikali ya kijeshi. Kuibuka kashfa ya ufisadi wa fedha na kuendelea hali ya kulegalega kisiasa na kijamii nchini Uturuki kulipelekea kutokea mgogoro wa kiuchumi ambapo hatimaye katika siku kama ya leo Jenerali Kenan aliyekuwa mkuu wa majeshi alifanya mapinduzi. Baada ya mapinduzi hayo, Jenerali Kenan akiwa pamoja na Baraza la watu sita walishika hatamu za uongozi wa nchi. Mbali na Waziri Mkuu kuondolewa madarakani, kulitolewa amri pia ya kuvunjwa Bunge sambamba na kupigwa marufuku shughuli za vyama vya siasa na nchi ikawa inatawaliwa na serikali ya kijeshi.
***
Miaka 30 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 21 Shahrivar 1375 Hijria Shamsia Changiz Shahvagh, mchongaji wa sanamu, mtengenezaji wa vyombo vya udongo na mchoraji wa kisasa wa Iran, alifariki dunia. Shahvagh anahesabiwa kuwa miongoni mwa waasisi na waanzilishi wa sanaa ya kisasa nchini Iran. Alizaliwa mwezi Shahrivar mwaka 1312 Hijria Shamsia mjini Baku. Alipokuwa na umri wa miaka mitatu, alihamia Tehran pamoja na familia yake. Mwaka 1336 Hijria Shamsia, Shahvagh alijiunga na Kitivo cha Sanaa Nzuri cha Chuo Kikuu cha Tehran. Mwaka mmoja baadaye, alifanya maonyesho ya kazi zake za sanamu za udongo na kauri katika Galeria ya Estetik. Mwaka mmoja baada ya maonyesho yake ya kwanza, alijikita kwa uzito zaidi katika sanaa ya uchongaji wa sanamu. Sanamu zake zilikuwa zikivunja mitazamo na dhana za kawaida kuhusu sanaa ya uchongaji. Alikuwa akibuni mtindo maalumu wa mpangilio wa taswira (kompozisheni), ambapo mara nyingi aliacha maana ya kazi yake itokane na fikra na tafsiri ya mtazamaji, huku akitoa nafasi kubwa kwa kipengele cha ubunifu. Baadaye, kazi zake zilionyeshwa katika maonyesho mbalimbali ya ndani na nje ya Iran, na zilimpatia tuzo mbalimbali. Pia alikuwa mwanzilishi wa galeria ya kwanza katika historia ya sanaa ya Iran. Changiz Shahvagh alifariki dunia kutokana na mshtuko wa moyo, na kuizikwa katika makaburi ya Behesht-e Zahra mjini Tehran, katika sehemu maalumu ya wasanii na waandishi.
***