Jumapili, 13 Septemba, 2026
Leo ni Jumapili Mosi Mfunguo Saba Rabiu Thani 1448 Hijria sawa na 13 Septemba 2026.
Siku kama ya leo miaka 1399 iliyopita, vilimalizika vita vya miaka 24 baina ya mfalme wa Iran na Roma. Khosrow Parvēz, mfalme wa Kisasani kwa kutekeleza mashambulizi mtawalia, aliweza kudhibiti maeneo ya Mesopotamia, Syria, Palestina, Misri na Asia Ndogo, na hivyo akawa ameweza kupanua wigo wa ushindi wake hadi kufikia Istanbul ya leo. Mwaka 591 Miladia, hatimaye amani ilifikiwa kufuatia kutiwa saini makubaliano baina ya mfalme Khosrow Parvēz na mfalme wa Roma. Hata hivyo tarehe Tano Juni mwaka 603 Miladia, kuliibuka tena vita vilivyoendelea kwa muda wa miaka 24 baina ya nchi hizo mbili. Katika vita hivyo, jeshi la Iran lilipata ushindi mtawalia katika ardhi ya Roma kiasi cha kudhibiti karibu eneo zima la Roma ya Mashariki. Baadaye jeshi la mfalme Khosrow lilidhoofika na kumfanya mfalme huyo kukimbilia eneo la Ctesiphon, moja ya tawala za Sasania, huku akikataa pendekezo la usuluhishi. Aidha kutokana na Mfalme Khosrow Parvēz kuchana barua ya Mtukufu Mtume Muhammad (saw) na kulaaniwa na mtukufu huyo, utawala wa mfalame huyo ulidhoofika na hatimaye kushindwa na Waroma. Baadaye raia wa Iran, kwa kushirikiana na jeshi la taifa, walimuengua Khosrow kwenye utawala na kumfunga jela kabla ya kuuawa kwake.
***
Miaka 776 iliyopita katika siku kama ya leo, vilianza vita vya Mansuriyya katika silsila ya Vita vya Msalaba kati ya Wakristo na Waislamu. Vita hivyo vya kihistoria vilianzishwa katika eneo lililojulikana kwa jina hilo huko Misri na mfalme Saint Louis wa Ufaransa ambaye alikuwa na lengo la kuidhibiti Misri. Katika vita vya Mansuriyya Jeshi la Msalaba lilipigwa vibaya na wapiganaji wa Kiislamu wa Misri waliokuwa wakiongozwa na Salahuddin Ayyubi. Hatimaye Saint Louis alikamatwa mateka na Waislamu na kufungwa jela katika ikulu ya Loken ambayo hii leo inatumika kama jumba la makumbusho.
***
Siku kama ya leo miaka 141 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 13 Septemba 1885, alizaliwa Aquilino Ribeiro mwandishi na mwanamapinduzi wa Ureno. Baada ya kumaliza masomo yake, Ribeiro alitumbukia kwenye uwanja wa kisiasa na kufungwa jela kwa miaka kadhaa. Mnamo mwaka 1961, Aquilino Ribeiro alifanikiwa kupokea tuzo ya Nobel katika taaluma ya fasihi, na miaka miwili baadaye yaani mwaka 1963 akafariki dunia.
***
Katika siku kama ya leo miaka 126 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, Mulla Ali bin Fat'hullah Nahavandi, mmoja wa wanazuoni wakubwa wa madhehebu ya Shia, alifariki dunia mjini Najaf. Mulla Ali bin Fat'hullah Nahavandi Najafi alikuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa karne ya 14 Hijria, na alikuwa mwanafunzi wa Sheikh Murtadha Ansari na Mirza Abul-Qasim Kalantari. Alifariki dunia baada ya kuugua ugonjwa wa kipindupindu, na akazikwa katika makaburi ya Wadi al-Salaam mjini Najaf.
***
Miaka 33 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe 13 Septemba 1993 Yasir Arafat, kiongozi wa zamani wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO na Yitzhak Rabin waziri mkuu wa wakati huo wa utawala haramu wa Israel walisaini mkataba wa mapatano kwa jina la "Makubaliano ya Ghaza-Jericho" huko Washington, Marekani. Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO na utawala wa Kizayuni zilitambuana rasmi katika makubaliano hayo yaliyosainiwa miaka miwili baada ya kuanza mazungumzo eti ya amani kati ya Waarabu na utawala wa Kizayuni.
***
Na miaka 6 iliyopita katikka siku kama ya leo kwa mujib wa kalenda ya Hijria Shamsia, Ayatullah al-Udhma Haj Sheikh Yusuf Sanei, mmoja wa Marjaa Taqlid wa madhehebu ya Shia nchini Iran, alifariki dunia. Alizaliwa mwaka 1316 Hijria Shamsia katika familia ya wanazuoni wa dini huko Nik-Abad, Isfahan. Kuanzia mwaka 1325, alianza masomo yake katika Hawza ya Isfahan, na kuanzia mwaka 1330 Hijria Shamsia akaendelea na masomo katika Hawza ya Qum. Mwaka 1334, alishika nafasi ya kwanza katika mitihani ya ngazi za juu za masomo ya dini. Alipata malezi na mafunzo kutoka kwa walimu wakubwa, wakiwemo Ayatullah Borujerdi, Muhaqqiq Damad na Imam Khomeini. Kwa mujibu wa maelezo yake mwenyewe, akiwa na umri wa miaka 22, alikuwa tayari amefikia daraja ya Ijtihadi. Kuanzia mwaka 1354 Hijria Shamsia, alianza kufundisha masomo ya juu ya fiqhi, na akalea wanafunzi wengi. Baadaye, kutokana na Imam Khomeini kumfahamu vyema na kumuamini, aliteuliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Walinzi wa Katiba (Shura-ye Negahban) kuanzia mwaka 1358 hadi 1361. Baada ya hapo, aliteuliwa kuwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali, na pia alikuwa mwakilishi wa Tehran katika kipindi cha kwanza cha Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu. Hatimaye, asubuhi ya Jumamosi, tarehe 22 Shahrivar 1399 Hijria Shamsia, Ayatullah al-Udhma Haj Sheikh Yusuf Sanei alifariki dunia mjini Qum, baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo.
***