Ijumaa tarehe 11 Septemba 2026
-
Leo Katika Historia
Leo ni Ijumaa tarehe 29 Mfunguuo Sita Rabiul-Awwal 1448 Hijria sawa na tarehe 11 Septemba 2026.
Siku kama ya leo miaka 228 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Milaadia, kisiwa cha Sri Lanka kilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na wakoloni wa Kiingereza.
Kisiwa hicho ambacho kijiografia kipo kusini mwa Bara Hindi, kuanzia karne ya 3 Miladia kilikuwa kikihesabiwa kuwa moja ya vituo muhimu vya kiutamaduni vya Mabudha. ***
Miaka 82 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 29 Rabiul-Awwal, kuliasisiwa taasisi ya kukurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu huko Cairo Misri.
Taasisi hiyo ilianzishwa kwa hima na juhudi kubwa za Muhammad Taqi Qommi mwakilishi wa Ayatullah Sayyid Hussein Tabatabai Boroujerdi, Marjaa Taqlidi katika zama hizo na Imamu wa al-Azhar, Sheikh Muhammad Shaltut. Watu kama Sayyid Jamaluddin Asadabadi, mashuhuri kama Jamal Afghani, Sheikh Muhammad Abdu, Sheikh Muhammad Hussein Kashif al-Ghitaa na Sheikh Abdul-Majid Salim walijihusisha na kubadilisha mawazo na fikra katika uga huo.
Baada ya kuasisiwa taasisi hiyo ya kukurubisha maadhehebu za Kiislamu iliyojulikana kama Dar al-Taqrib Baina al-Madhahib al-Islamiyah" jarida la "Risalat al-Islam" nalo likaanza kuchapishwa. Jarida hili lilikuwa likichapisha makala za kielimu zenye thamani kuhusiana na madhehebu mbalimbali. ***
Miaka 77 iliyopita katika siku kama hii ya leo, aliaga dunia Muhammad Ali Jinnah, mwasisi wa Pakistan.
Jinnah alizaliwa mwaka 1876 katika mji wa Karachi kusini mwa Pakistan. Muhammad Ali Jinnah alikuwa miongoni mwa shakhsiya walioasisi chama cha Muslim League mnamo mwaka 1906.
Chama cha Muslim League awali kilikuwa kikijishughulisha na masuala ya kitamaduni na kidini, lakini baadaye kikaingia katika uwanja wa siasa na kutaka kuundwa nchi huru kwa ajili ya Waislamu wa India. ****
Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita, Jenerali Agustino Pinoche kamanda wa wakati huo wa vikosi vya majini vya Chile aliipindua serikali halali ya Salvador Alande katika mapinduzi yaliyoungwa mkono na Marekani.
Alande ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kisoshalisti cha Chile, alichaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo mwaka 1970. ****
Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita inayosadifiana na tarehe 20 Shahrivar 1360 Hijria Shamsia, aliuawa Shahidi Ayatullah Sayyid Asadullah Madani, Imamu wa Swala ya Ijumaa katika mji wa Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran wakati wa kuswalisha Swala ya Ijumaa.
Shambulio hilo la kigaidi lilifanywa na kikundi cha kigaidi cha Munafiqin. Ayatullah Madani alipatia elimu kwa maulamaa kadhaa katika mji wa Qum na kisha kuelekea Najaf Iraq, ambako aliweza kujipatia daraja ya juu ya kielimu ya Ijitihad.
Msomi huyo alikamatwa na kuteswa mara kadhaa na askari wa utawala wa mfalme wa Iran kutokana na misimamo yake ya kuupinga utawala huo. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini MA alimteua Ayatullah Madani kuwa Imam wa Swala ya Ijumaa katika mji wa Tabriz. ***
Miaka 25 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 11 Septemba mwaka 2001, ndege mbili kati ya nne za abiria za Marekani zilizotekwa nyara ziligonga minara miwili pacha ya jengo la Biashara la Kimataifa la mjini New York huku ndege moja ikigonga jengo la Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) huko Washington.
Ndege ya nne ililengwa ikiwa katika anga ya Pensylvania na kuangushwa. Baadhi ya ghorofa za jengo la Biashara ya Kimataifa ziliporomoka na sehemu ya jengo la Pentagon pia ikaharibiwa katika mashambulizi hayo ya kigaidi. Karibu watu 3200 waliuawa katika mashambulizi hayo. Marekani ilitangaza kuwa mtandao wa al Qaida uliokuwa ukiongozwa na Usama bin Laden raia wa Saudi Arabia, ndio uliohusika na mashambulizi hayo.
Baada ya matukio ya Septemba 11 nchini Marekani, kulianza wimbi la ubaguzi na mashambulizi dhidi ya Waislamu na matukufu ya dini yao katika nchi za Magharibi. ****