Jumatano, Septemba 9, 2026
Leo ni Jumatano 27 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1448 Hijria sawa na 09 Septemba 2026 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1454 iliyopita kulianza vita maarufu kwa jina la vita vya miaka saba kati ya madola mawili yaliyokuwa na nguvu ya Iran na Roma, baada ya mfalme Justinian wa Roma kuanzisha mashambulizi yaliyokuwa na lengo la kulikalia eneo la magharibi mwa Iran.
Baada ya miaka saba ya vita mfalme wa Iran Anushirvan alimshinda mfalme Justinian wa Roma na hivyo mfalme huyo akalazimika kujiuzulu. Baada ya kujiuzulu mfalme Justinian mfalme Tiberius alishika mamlaka ya utawala wa Roma. Vita hivyo vilimalizika mwaka 579 baada ya Waroma kukubali kuilipa Iran gharama inayofikia sarafu za dhahabu elfu 45. ***
Tarehe 27 Rabiul Awwal miaka 1085 iliyopita alizaliwa mshairi na mwandishi mashuhuri wa Kiarabu Abul Alaa Maarry katika mji wa Maarrat al-Nu'man nchini Syria.
Abul Alaa alifariki dunia mwaka 449 Hijria katika mji huo huo ulioko umbali wa kilomita 33 kusini mwa Halab (Aleppo). Baadaye alielekea Baghdad kwa ajili ya kukamilisha elimu ya juu. Licha ya kuwa kipofu tangu utotoni, lakini Abul Alaa alitokea kuwa mshairi mashuhuri na hodari wa zama zake. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri la "Risalatul Ghufran" na "al Aamali." ***
Siku kama hii ya leo miaka 198 iliyopita alizaliwa Leo Tolstoy, mwandishi na mwanafasihi raia wa Russia.
Awali Tolstoy alijiunga na jeshi la Qaukasia na katika kipindi hiki ndipo alipoandika kitabu chake cha kwanza alichokupa jina la "Childhood". Mwandishi huyo wa Russia baadae alijiengua jeshini na kutumia muda wake wote kwa ajili ya kusoma na kuandika.
Miongoni mwa vitabu muhimu vya mwandishi Leo Tolstoy ni "Vita na Amani", "Waqazaki" na "Hadji Murad." Tolstoy alifariki dunia mwaka 1910. ***
Siku kama ya leo miaka 81 iliyopita yaani tarehe 9 Septemba 1945, ulitiwa saini mkataba wa kusalimu amri vikosi vya Japan vilivyokuwa vimeidhibiti na kuikalia kwa mabavu China.
Kwa mujibu wa mkataba huo askari milioni moja wa Japan waliweka chini silaha zao kwa amri ya Hirohito mfalme wa wakati huo wa Japan. Kwa utaratibu huo vita vya kihistoria kati ya China na Japan vikafikia tamati. ***
Miaka 58 iliyopita katika siku kama ya leo Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim, mkuu wa kituo cha kidini cha Najaf aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 92.
Baada ya kuaga dunia Ayatullah Burujerdi ambaye alikuwa mar'ja' mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu, Ayatulah Hakim alichukua nafasi yake na kufuatwa na Waislamu wengi na hasa wa Iraq, kuhusiana na masuala ya kifik'hi. Alipambana vikali na kila kundi au watu waliojaribu kuharibu jina la Uislamu.
Fatua yake mashuhuri ya kupinga fikra ya ukomunisti dhidi ya mafundisho ya dini ilileta mabadiliko makubwa nchin Iraq. Fatua hiyo pia ilimpelekea kutoa amri ya kupigana jihadi dhidi ya utawala haramu wa Israel. Ujenzi wa maktaba, shule na vituo vya kidini na kiutamaduni pamoja na uandishi wa vitabu kama vile Mustamsak Urwat al-Wuthqah na Nahjul Faqaha ni miongoni mwa vitabu mashuhuri vilivyoandikwa na mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kiislamu. ***
Miaka 57 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia Jalal Aal Ahmad, mwandishi na mkosoaji wa Kiirani. Aal Ahmad alizaliwa mwaka 1302 Hijria Shamsiya jijini Tehran.
Mwaka 1325, Jalal al Ahmad alitunukiwa shahada ya fasihi ya Chuo Kikuu cha Tehran. Aliingia katika uwanja wa siasa wakati wa Vita vya Pili vya Dunia na akaanza kuandika magazeti. Alijishughulisha na kuandika makala na ukosoaji na hadithi fupifupi. Jalal Aal Ahmad alikuwa hodari katika kuandika visa na hekaya fupifupi. ***
Miaka 50 iliyopia katika siku kama ya leo, aliaga dunia Mao Zedong kiongozi wa Uchina.
Mao Zedong alizaliwa mwaka 1893 na mwaka 1921 aliunda chama cha Kikomonisti cha Uchina baada ya kuungwa mkono na wafuasi wa fikra zake. Mao alikuwa akisisitiza suala la kuwatetea na kuwalinda wanavijiji na kwa sababu hiyo ilipata uungaji mkono mkubwa wa wanavijiji wa Uchina.