Mjumbe wa UN ataka mchakato shirikishi wa kisiasa nchini Sudan
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Pekka Haavisto, ametoa wito Jumapili hii kwa ajili ya kufikiwa kwa maendeleo katika mchakato wa kisiasa unaojumuisha wadau wote na wenye mkakati madhubuti, uliolenga kuhitimisha mzozo wa muda mrefu nchini humo.
Haavisto alitoa kauli hizo wakati wa mazungumzo jijini Khartoum na Mkuu wa Jeshi na Mwenyekiti wa Baraza la Utawala, Abdel Fattah al-Burhan.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na baraza hilo, pande hizo mbili zilijadili hali ya usalama nchini Sudan, juhudi za kuimarisha uthabiti, na matarajio ya kufikia amani ya kina. Haavisto amenukuliwa akisema “Nimefikisha jumbe muhimu zinazohusu kupunguza makali ya mzozo na kulinda raia.”
Pia ameonyesha matumaini kuwa mazungumzo yanayoendelea yanaweza kuzaa matunda katika suala la kubadilishana wafungwa na raia wanaoshikiliwa na Jeshi la Sudan pamoja na waasi wa RSF.
Haavisto amesisitiza kuwa: “Majadiliano ndiyo njia pekee ya kufikia amani endelevu." Amongeza kuwa Umoja wa Mataifa utashirikiana na wadau wa Sudan na washirika wengine katika utaratibu wa wanachama watano ili kuendeleza mchakato wa kisiasa unaoakisi matamanio ya wananchi wa Sudan.
Utaratibu huu unahusisha Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, na Halmashauri ya Maendeleo ya Kieneo (IGAD).
Haavisto aliwasili Sudan siku ya Ijumaa kwa ajili ya mazungumzo na pande husika kuhusu kupunguza mivutano na ulinzi wa raia. Muda wa ziara yake haukuwekwa wazi.
Mnamo Agosti 30, Kamati ya Maandalizi ya Majadiliano ya Sudan ilizindua mpango huru wa kuwezesha mashauriano na kusaidia kuandaa njia ya kumaliza vita na kufikia mwafaka mpana wa kitaifa.
Sudan imekuwa ikishuhudia vita kati ya Jeshi la Taifa na waasi wa RSF tangu Aprili 2023, mzozo ambao umesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu na kupelekea karibu milioni 13 kuyahama makazi yao, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa na wadau wengine wa kimataifa. Sudan inaituhumu serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu kuwa inawaunga mkono waasi hao wa RSF.