Viongozi wa Afrika watoa mwito wa ulinzi imara zaidi dhidi ya ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141286-viongozi_wa_afrika_watoa_mwito_wa_ulinzi_imara_zaidi_dhidi_ya_ugaidi
Viongozi mbalimbali wa Afrika walisema jana Jumatatu kwamba, kuimarisha ulinzi wa miundombinu muhimu na maeneo ya umma dhidi ya vitisho vya ugaidi ni muhimu kwa malengo ya Afrika ya maendeleo ya amani, ujumuishaji, na mshikamano wa kijamii.
(last modified 2026-09-08T04:36:03+00:00 )
Sep 08, 2026 04:35 UTC
  • Viongozi wa Afrika watoa mwito wa ulinzi imara zaidi dhidi ya ugaidi

Viongozi mbalimbali wa Afrika walisema jana Jumatatu kwamba, kuimarisha ulinzi wa miundombinu muhimu na maeneo ya umma dhidi ya vitisho vya ugaidi ni muhimu kwa malengo ya Afrika ya maendeleo ya amani, ujumuishaji, na mshikamano wa kijamii.

Wakizungumza katika mkutano wa tano wa Caucus wa Nairobi nchini Kenya, viongozi hao walielezea kusitikitishwa kwao na kuongezeka udhaifu wa miundombinu ya kimkakati ya bara hilo, ikiwa ni pamoja na barabara, madaraja, viwanja vya ndege, bandar, na miundombinu ya kidijitali licha ya kwamba vitisho kutoka kwa magenge ya kigaidi vinaongezeka siku baada ya siku.

Mkutano huo umeitishwa na Kituo cha Taifa cha Kupambana na Ugaidi nchini Kenya kwa kushirikiana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Ugaidi. Kongamano hilo la siku mbili linafanyika chini ya mada "Kulinda Mifumo Muhimu ya Miundombinu na Maeneo ya Umma mbele ya Ugaidi."

Mkutano huo umewakutanisha pamoja watunga sera wakuu, wataalamu wa usalama, washirika wa maendeleo, wasomi na wawakilishi wa asasi za kiraia ili kuchunguza mikakati bunifu ya kuzuia mashambulizi ya kigaidi dhidi ya miundombinu ya umma.

Musalia Mudavadi, katibu mkuu wa baraza la mawaziri la Kenya na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, amebainisha katika kongamano hilo kwamba Afrika imekuwa kitovu cha ugaidi duniani, huku miundombinu muhimu inayosaidia kimaisha raia ikishambuliwa mara kwa mara na magaidi hao.

"Mwaka 2026, bara la Afrika limekumbwa na mashambulizi makubwa ya kigaidi, ikiwa ni pamoja na kushambuliwa miundombinu muhimu," amesema Mudavadi akibainisha kuwa, nchi sita kati ya 10 zilizoathiriwa zaidi na ugaidi ziko kusini mwa Jangwa la Sahara.

Amezitaka serikali za kikanda kuimarisha ushirikiano wao wa masuala ya kijasusi, kutumia mbinu bora za kimataifa na kufanya mageuzi ya usalama ili kulinda miundombinu muhimu, ikiwa ni pamoja na vifaa vya umeme, reli, mabwawa, vituo vya afya na kumbi za michezo.

Kwa upande wake, Steven Siqueira, naibu mkurugenzi wa Kituo cha Kupambana na Ugaidi cha Umoja wa Mataifa, amesema kwenye kongamano hilo kwamba kuzuia mashambulizi ya kigaidi kwenye miundombinu muhimu ya nchi za Afrika ni muhimu kwani miundombinu ni nguzo za kiuchumi, kuunganisha jamii na kutoa huduma za umma.