Apr 26, 2025 02:33 UTC
  • Jumamosi, 26 Aprili, 2025

Leo ni Jumamosi 27 Mfunguo Mosi Shawwal 1446 Hijria sawa na 26 Aprili 2025 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1105 iliyopita alizaliwa malenga wa Kiirani, Abu Is'haq Kesa-i Marvazi. Kipindi cha ujana wake kiliambatana na kumalizika kwa kipindi cha utawala wa Wasaman na mwanzoni mwa zama za utawala wa Waghaznavi.  Kwa sababu hiyo malenga huyu Mfarsi alitunga mashairi kadhaa ya kusifu tawala hizo mbili. Fauka ya hayo Marvazi alitunga beti kadhaa za mashairi ya kumsifu Mtume Muhammad na (saw) na kizazi chake kitoharifu hasahasa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Malenga huyu mkubwa wa Kiirani ameacha diwani ya mashairi.

Abu Is'haq Kesa-i Marvazi

 

Tarehe 26 Aprili miaka 420 iliyopita lilichapishwa gazeti la kwanza kabisa duniani nchini Ufaransa. Mhariri mkuu wa gazeti hilo lililopewa jina la Relation alikuwa Johann Carolus. Gazeti hilo liliendelea kuchapishwa kwa kipindi cha miaka 70. Hii leo maelfu ya magazeti huchapishwa kila siku katika pembe mbalimbali za dunia na Wajapani wanahesabiwa kuwa wasomaji wakubwa zaidi wa magazeti kuliko watu wa maeneo mengine ya dunia.   

Relation

 

Katika siku kama ya leo miaka 92 iliyopita, shirika la kuogofya la Gestapo la  Ujerumani liliasisiwa. Shirika hilo liliasisiwa na Hermann Wilhelm Goering aliyekuwa mmoja wa maafisa wa juu wa utawala wa Adolph Hitler kiongozi wa Wanazi wa Ujerumani. Shirika hilo lilikuwa polisi wa siri wa Kijerumani katika kipindi cha utawala wa Wanazi. Jukumu la German for Secret State Police, kama lilivyojulikaa pia, lilikuwa ni kuwafatilia, kuwatia mbaroni na kuwanyongwa watu waliokuwa wakimpinga Hitler na siasa zake za Kinazi. Kiongozi mashuhuri kabisa wa Gestapo alijulikana kwa jina la Heinrich Himmler na alianza kuwaongoza polisi hao wa siri wa Kijerumani mwaka 1934.

 

Miaka 61 iliyopita katika siku kama ya leo, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliundwa baada ya nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar kuungana. Kabla ya kuungana huko Tanganyika na Zanzibar zilikuwa zikikoloniwa na nchi mbalimbali ambapo nchi mkoloni wa mwisho ilikuwa Uingereza. Tanganyika ilipata uhuru mwaka 1961 na Zanzibar mwaka 1963 baada ya mapambano ya wananchi ya kupigania uhuru dhidi ya mkoloni Muingereza. Julius Kambarage Nyerere alitoa wito wa kuungana Tanganyika na Zanzibar na ilipofika tarehe 26 mwezi Aprili mwaka 1964 nchi mbili hizo ziliungana na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tanzania iko mashariki mwa Afrika na katika pwani ya Bahari ya Hindi huku ikipakana na Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, Malawi na Msumbiji. 

 

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa azimio nambari 620 likilaani hatua ya Iraq ya kutumia silaha za kemikali dhidi ya Jamhuri ya Kislamu ya Iran. Baada ya utawala wa zamani wa Iraq kushambulia kwa mabomu ya kemikali makazi ya raia nchini Iran na kufuatia mashtaka yaliyowasilishwa na Iran, ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulitumwa katika nchi za Iran na Iraq na ukatoa ripoti mbili ambazo zilieleza kuwa, utawala huo ulitumia mara kadhaa silaha za kemikali dhidi ya majeshi na raia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kukiri waziwazi kwamba, jeshi la Iraq lilitumia silaha za kemikali dhidi ya Iran. Katika kipindi chote cha vita vya miaka 8 vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran, utawala wa Saddam Hussein uliua shahidi maelfu ya wanajeshi na raia wa Iran kutokana na kutumia silaha za gesi yenye kemikali. Kwa sababu hiyo Iran inatambuliwa kuwa mhanga mkubwa zaidi wa silaha za kemikali duniani baada ya Vita vya Pili vya Dunia. 

 

Siku kama ya leo 39 iliyopita, kituo cha nguvu za nyuklia cha Chernobyl huko Ukraine ambacho kilikuwa kikidhamini sehemu kubwa ya nishati ya umeme ya nchi hiyo kiliripuka na kusambaza mada hatari za miale ya radioactive. Awali Russia ilikadhibisha habari ya kutokea mlipuko katika kituo hicho. Hata hivyo baadaye ililazimika kukiri kutokea mlipuko katika kituo hicho cha nguvu za nyuklia cha Chernobyl baada ya wingu kubwa la nyuklia lililosababishwa na mada za radioactive kuoneka waziwazi katika kituo hicho. Kasoro za kiufundi zilitajwa kuwa chanzo cha mlipuko huo. Katika tukio hilo, makumi ya maelfu ya watu waliathirika kwa namna tofauti ikiwemo kuongezeka maradhi mbalimbali. Mwaka 2000 Ukraine ilikifunga kabisa kituo cha nyuklia cha Chernobyl.