Jumamosi, 11 Oktoba, 2025
Leo ni Jumamosi 18 Mfunguo Saba Rabiuthani 1447 Hijria mwafaka na 11 Oktoba 2025 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 845 iliyopita, alizaliwa Abul Qasim Jafar bin Hassan Hilli maarufu kwa lakabu ya Muhaqiq Hilli, mmoja wa wanazuoni wakubwa na faqihi ya Kiislamu, katika mji mashuhuri wa Hillah, nchini Iraq. Muhaqiq Hilli alikuwa msomi aliyekuwa na nafasi ya juu na mtaalamu wa sheria za Kiislamu na alibobea pia katika fasihi na uandishi wa mashairi. Baada ya kukamilisha masomo ya awali na kupaa daraja za juu za kiroho, alitambuliwa kuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa zama zake. Kitabu muhimu zaidi cha Muhaqqiq al Hilli ni Sharaiul Islam, fii Masaailil-Halal Walharaam'. Mwanazuoni huyo pia ameandika vitabu vya "Al Nafi", "Maarij" na "al Tanbih". Muhaqqiq al Hilli alifariki dunia mwaka 676 Hijria akiwa na umri wa miaka 74.

Katika siku kama ya leo miaka 126 iliyopita, vilianza vita vya umwagaji damu kati ya wazungu wa Kiholanzi kwa jina la Boers wakazi wa Afrika Kusini na Waingereza. Wanajeshi wa Uingereza waliwasili Afrika Kusini mwaka 1841 lengo likiwa ni kuikoloni Afrika. Waingereza walidhibiti Afrika Kusini baada ya kujenga maeneo ya kiraia nchini humo. Wahamiaji wengine kutoka Ulaya hususan Waingereza walimiminika huko Afrika Kusini baada ya kugunduliwa madini ya dhahabu na Almasi. Wazungu wa Uholanzi yaani Maboers waliwasili Afrika Kusini katika karne ya 19 na kupinga kuwasili wahamiaji wapya nchini humo. Sababu hiyo ilipelekea kuanza vita kati ya Wazungu hao na wahamiaji wa Kiingereza, lakini uungaji mkono wa serikali ya Uingereza kwa wahamiaji hao, ulitoa pigo kwa Maboers na kwa msingi huo Afrika Kusini ikaloloniwa na Uingereza.

Miaka 110 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia Jean Henri Fabre msomi wa elimu ya sayansi na bingwa wa elimu ya wadudu au entomolojia. Fabre alizaliwa mwaka 1823 nchini Ufaransa. Msomi huyo ambaye pia alikuwa mwandishi amefanya utafiti mkubwa na kuandika vitabu kadhaa kwenye uwanja wa elimu ya wadudu.

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Haji Mirza Khalil Kamarei, mfasiri wa Qur'ani Tukufu na mhadhiri wa chuo kikuu. Ayatullah Kamarei alijifunza elimu za fiqih, usul-fiqih na masomo mengine ya kidini katika Hauza ya kielimu ya mji mtakatifu wa Qum nchini Iran na baadaye alianza kufundisha falsafa. Haji Kamarei ameandika vitabu vingi kwa lugha za Kifarsi na Kiarabu. Miongoni mwa vitabu hivyo ni tafsiri ya Qur'ani, sherhe ya Nahjul Balagha na kitabu cha maisha ya Imam Hussein (as) na mashahidi wengine wa Karbala.

Miaka 35 iliyopita katika siku kama ya leo, kwa amri ya Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, nchini Iran kuliundwa Jumuiya ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu. Kabla ya hapo taasisi hiyo ilikuweko katika zama za Ayatullah Burujerdi na kwa ajili ya kunufaika na mambo ya pamoja Madhehebu za Kiislamu, alikuwa akituma jumbe mbalimbali huko Cairo Misri ambazo zilikuwa zikikutana na kufanya mazungumzo na wasomi na wanazuoni wakubwa wa Kisuni. Safari na mazungumzo hayo yalikuwa na matokeo mazuri ambapo katika zama za Sheikh Shaltut akiwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha al-Azhar, maulamaa wa Kisuni katika chuo kikuu hicho waliyatambua rasmi Madhehebu ya Kishia. Duru mpya ya jumuiya hii imeandaa uwanja wa kukurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu katika uga wa kiitikadi, kifikra, kifikihi na kielimu.

Na 11 Oktoba mwaka 1991 yaani siku kama ya leo miaka 34 iliyopita shughuli za Shirika la Ujasusi la Urusi ya zamani (KGB) zilifikia kikomo muda mfupi baada ya kusambaratika nchi hiyo. KGB iliundwa mwaka 1954 kwa lengo la kukabiliana na harakati zilizokuwa na lengo la kuuangusha mfumo wa Kikomonisti wa Urusi ya zamani. Shirika hilo aidha lilikuwa na majukumu kama vile kuwakandamiza wapinzani wa chama cha Kikomonisti na kuendesha operesheni za kijasusi na zile zilizo dhidi ya ujasusi ndani na nje ya Muungano wa Kisovieti.
