Jan 18, 2026 02:35 UTC
  • Jumapili, 18 Januari, 2026

Leo ni Jumapili 28 Rajab 1447 Hijria sawa na 18 Januari 2026 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1387 iliyopita, ilianza safari ya msafara wa Imam Hussein (as) kutoka Madina kwenda mjini Makka. Hatua hiyo ilijiri baada ya kufariki dunia Muawiyah Bin Abu Sufiyan tarehe 15 ya mwezi wa Rajab na kutwaa madaraka mwanaye, Yazid Bin Muawiyah. Baada ya Yazid kutwaa madaraka, haraka sana alimtaka mtawala wa mji wa Madina amlazimishe Imamu Hussein (as) kutoa baia (kiapo cha utiifu) kwake na kwamba iwapo angekataa kufanya hivyo basi amuuwe. Kwa kuzingatia kwamba Yazid alikuwa mtu muovu na mtenda madhambi, Imamu Hussein alikataa kutoa kiapo hicho na kwa ajili hiyo akaamua kuondoka Madina yeye na watu wa familia ya Mtume Muhammad (saw) kuelekea mjini Makkah. Kabla ya kuanza safari hiyo, Imamu Hussein (as) alimuusia kaka yake Muhammad Ibnil-Hanafiyyah akisema: "Ninatoka kwa ajili ya kurekebisha umma wa babu yangu, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw); ninataka kuamrisha mema na kukataza maovu na kufuata njia ya babu yangu, Muhammad, na baba yangu, Ali Ibn Abi Twalib (as)…."  Baada ya kufika Makka na kufuatia kukithiri barua za watu wa mji wa Kufa Iraq, waliokuwa wamemtaka aelekee huko kwa ajili ya kuwaongoza, Imamu Hussein (as) aliamua kuelekea Kufa ambapo hata hivyo alizuiliwa na jeshi la Yazid eneo la Karbala na kuuawa shahidi yeye na watu wa familia ya Mtume (saw) katika eneo hilo. ***

 

Siku kama ya leo miaka 337 iliyopita alizaliwa mwandishi na mwanafalsafa maarufu wa Ufaransa, Charles de Montesquieu. Alikuwa miongoni mwa wasomi ambao fikra na itikadi zao zilikuwa na taathira kubwa katika harakati ya mapinduzi ya Ufaransa na alikuwa mtu wa kwanza kutoa nadharia ya udharura wa kutenganishwa nguvu kuu tatu za dola.  Kitabu maarufu zaidi cha Charles de Montesquieu ni "The Spirit of the Laws" (Roho ya Sheria) ambacho kilichapishwa mwaka 1748 huko Geneva. Katika kitabu hicho alichunguza aina mbalimbali za serikali zilizojitokeza katika kipindi chote cha historia, ada na sheria za kimaumbile, sheria za kibinadamu na uhusiano baina yao. Kitabu kingine cha mwanafalsafa huyo wa Kifaransa ni "Persian Letters" (Barua za Kiiran). Alifariki dunia mwaka 1755. ***

 

Tarehe 18 Januari miaka 111 iliyopita 'Mkataba wa Siri' ulitiwa saini kati ya nchi tatu za Ufaransa, Uingereza na Russia wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia. Lengo kuu la mtakaba huo lilikuwa ni suala la kujiunga utawala wa Kiothmani (Ottoman Empire) na waitifaki wa Vita vya Kwanza vya Dunia, yaani Ujerumani na Austria. Kwani kujiunga utawala huo na waitifaki kungekata uhusiano wa jeshi la majini la Russia na waitifaki wake katika Bahari Nyeusi. Baada ya kutiwa saini mkataba huo, nchi waitifaki zilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya lango bahari la Dardanelles linalounganisha Bahari Nyeusi na Bahari ya Mediterranean. 

 

Siku kama ya leo miaka 110 iliyopita alifariki dunia Ayatullahil-Udhma Sayyid Mohammed Kazem Tabatabai Yazdi maarufu kwa jina la Allamah Yazdi, msomi mashuhuri wa elimu ya fiqhi. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi alijiunga na hauza ya kielimu ya mjini Najaf, Iraq na kupata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo kama vile Ayatullah Mirza Shirazi ambapo alifikia daraja ya ijtihadi. Baada ya hapo alijishughulisha na kazi ya ufundishaji huku akihusika pia na kuasisi vituo vya misaada, misikiti na shule za kidini. Ameacha taathira mbalimbali lakini maarufu ni kitabu cha 'Al Urwatul-Wuthqa' na 'Bustane Niyaz' ambacho kinahusiana na dua. 

 

Siku kama ya leo miaka 107 iliyopita yaani tarehe 18 Januari 1919, ulifanyika mkutano wa kihistoria wa amani wa Versailles baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, kwa kuwashirikisha wawakilishi wa nchi 27 kutoka mabara matano duniani. Mkuu wa mkutano huo alikuwa Georges Clémenceau, waziri mkuu wa wakati huo wa Ufaransa. Nchi tano zilizokuwa zimeshindwa kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia yaani Ujerumani, Austria, Hungary, Bulgaria na dola la Othmania, hazikushiriki kwenye mkutano huo. Kwa mujibu wa mkataba uliotiwa saini katika mkutano huo, Ujerumani ililazimishwa kulipa fidia kubwa na kutoa sehemu za ardhi zake kwa Austria. Mkutano huo ulikuwa utangulizi wa kuanzishwa Jumuiya ya Kimataifa.