Jan 20, 2026 02:09 UTC
  • Leo Katika Historia
    Leo Katika Historia

Leo ni Jumanne tarehe 30 Rajab 1447 Hijria mwafaka na tarehe 20 Januari 2026.

Miaka 126 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia John Ruskin mwandishi, mwanafalsafa na mkosoaji mashuhuri wa Uingereza.

Msomi huyo aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 80. Ruskin alizaliwa mwaka 1819 mjini London. Awali Ruskin alifunzwa na wazazi wake akiwa nyumbani kabla ya kujiunga na chuo cha mjini London na akiwa huko akaanza kutunga mashairi.

Malenga huyo wa Uingereza alikuwa mkosoaji wa sekta ya sanaa na alibainisha mitazamo yake kuhusu sanaa katika kitabu chake alichokipa jina la "modern painters". 

Tarehe 20 Januari miaka 106 iliyopita alizaliwa mtengeneza filamu mashuhuri wa Italia, Federico Fellini. Alikuwa mtayarishaji filamu mwenye mbinu makhsusi.

Fellini alianza kuandika rasimu ya filamu (scenario) mwaka 1938 na baadaye akaingia katika uwanja wa kutayarisha filamu. Baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia Fellini alishirikiana na mtengenezaji filamu mwingine wa Italia, Roberto Rossellini, katika utengenezaji wa filamu ya "Rome, Open City" (Roma, Mji Usiokuwa na Ulinzi).

Miezi sita kabla ya kufariki dunia, Federico Fellini alitunukiwa tuzo ya fahari ya Oscar kutokana na kazi zake kubwa katika medani ya filamu. Filamu mashuhuri zaidi za Fellini ni "Saa Mbili Unusu", "Juliet of the Spirits" na "The Sweet Life".   

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita habari ya kukaribia safari ya kurejea nchini Imam Ruhullah Khomeini kutoka uhamishoni nje ya nchi ilienea kati ya wananchi wa Iran.

Habari hiyo ilizusha furaha na vifijo kati ya matabaka mbalimbali ya wananchi. Mazungumzo na mijadala kuhusu suala la kurejea nchini Imam Khomeini na jinsi ya kumpokea shujaa huyo ilitanda kona zote na vikao vya wananchi. Katika upande mwingine uamuzi wa Imam Khomeini wa kurejea nchini ulitikisa nguzo za utawala wa kifalme wa Shah.

Vibaraka wa utawala huo walikuwa wakitafuta njia ya kujiokoa na wengi miongoni mwao walijiuzulu nyadhifa zao na kukimbilia nje ya nchi. Baadhi ya majenerali wa jeshi waliokuwa karibu na Shah waliwashambulia wananchi katika jitihada za mwisho za kulinda utawala huo wa kifalme. Mashambulizi hayo yalizidisha azma na moyo wa mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran.

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita sawa na tarehe 30 Dei 1357 Hijria Shamsia, Mhandisi Mehdi Bazargan, Waziri Mkuu wa kwanza wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alifariki dunia.

Mhandisi Bazargan alizaliwa mjini Tehran na kuhitimu masomo yake ya uhandisi wa magari huko nchini Ufaransa. Alikuwa mhadhiri pia katika Chuo Kikuu cha Tehran. Aliingia katika harakati za kisiasa wakati wa kujiri tukio la kutaifishwa sekta ya mafuta ya Iran na kufanywa kuwa mali ya taifa.

Muda mchache kabla ya mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini, Mehdi Bazargan alikuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na kwa pendekezo la baraza hilo alitakiwa kuunda serikali ya muda. Hata hivyo serikali yake ilidumu kwa muda wa miezi 9 tu kutokana na kuwa na tofauti za kimsingi na Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kupenya katika serikali hiyo vibaraka waliokuwa dhidi ya mapinduzi.  Hatimaye Bazargan aliaga dunia katika siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 87 baada ya kuugua maradhi ya moyo.