Jan 24, 2026 02:46 UTC
  • Jumamosi, 24 Januari, 2026

Leo ni Jumamosi 4 Shaaban 1447 Hijria awa na 24 Januari 2026 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1421 iliyopita, yaani tarehe 4 Sha'ban mwaka 26 Hijria, alizaliwa Hadhrat Abbas bin Ali Bin Abi Talib, mashuhuri kwa lakabu ya Abul Fadhl. Mama yake ni Ummul-Banin, ambaye aliolewa na Imam Ali bin Abi Twalib (as) baada ya kufariki dunia Bibi Fatima Zahra (as). Abul Fadh al-Abbas alikulia katika familia ya watu adhimu kama vile baba yake Imam Ali (as), kaka zake Imam Hassan na Hussein na dada yake mtukufu Zaynab (as). Alimpenda sana kaka yake Hussein Bwana wa Mashahidi, kiasi kwamba alisabilia maisha yake katika ardhi ya Karbala kwa lengo la kumtetea yeye na risala yake kwa nguvu zake zote. Abbas alifahamika mno kutokana na elimu, ukweli na uchaji Mungu wake. Kutabahari kwake katika elimu kuliwafanya watu wengi warejee kwake kwa  ajili ya kutatuliwa masuala mbalimbali ya kielimu. Siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Abul Fadhl Abbas inajulikana hapa nchini Iran kama Siku ya Vilema wa Vita. Aidha katika siku ya kuzaliwa mtukufu huyo, watu wa Iran huwa wanawakumbuka na kuwaenzi mashujaa waliosimama imara katika vita vya kulazimishwa vya utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya Iran. 

 

Katika siku kama ya leo miaka 1006 iliyopita, sawa na tarehe 4 Shaban 440 Hijiria, alifariki dunia Abu Said Abul-Khayr, mtaalamu wa elimu ya Kumjua Mwenyezi Mungu (irfan) na malenga wa Iran akiwa na umri wa miaka 83. Abu Said alizaliwa mwaka 357 Hijiria na kujifunza elimu ya hisabati na historia ya wafalme. Aidha alitabahari katika elimu za tafsiri ya Qur’ani, Hadithi na fiqhi (sheria za Kiislamu), huku akipata elimu ya irfani kutoka kwa wanazuoni mashuhuri wa elimu hiyo wa karne ya nne na ya tano Hijiria. Kitabu cha ‘Asraarut-Tawhid’ ni moja ya turathi za Abu Said Abul-Khayr. Aidha alipendelea sana kusoma mashairi. 

Kaburi la Said Abul-Khayr

 

Miaka 359 iliyopita katika siku kama ya leo, mkataba wa Breda ulitiwa saini kati ya Uingereza na Uholanzi. Kwa mujibu wa mkataba huo, Uholanzi ambayo haikuwa na uwezo wa kulinda makoloni yake katika bara lililokuwa ndio kwanza limegunduliwa la Amerika, iliyakabidhi makoaloni yake hayo kwa Uingereza. Eneo muhimu ambalo Uingereza ilikabidhiwa ni New York, ambalo leo kijiografia linapatikana mashariki mwa Marekani. 

 

Katika siku kama ya leo miaka 167 iliyopita, kisima cha kwanza kabisa cha mafuta katika historia kilichimbwa huko Pennsylvania nchini Marekani.  Kisima hicho kilichimbwa na Edwin Laurentine Drake kikiwa na kina cha urefu wa mita 230. Uchimbaji wa kisima hicho uliendelea kwa kipindi cha mwaka mmoja. Vifaa vilivyotumika kuchimbia kisima hicho vimehifadhiwa hadi leo katika jumba moja la makumbusho nchini Marekani.

 

Miaka 61 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Winston Churchill, mwanasiasa maarufu wa Kiingereza akiwa na umri wa miaka 91. Churchill alizaliwa mwaka 1874 na mwaka 1895 alijiunga na jeshi la Uingereza na kushiriki katika vita vya kikoloni. Mwaka 1900 Winston Churchil aliingia katika Bunge la Uingereza akikiwakilisha chama cha Kihafidhina na mara kadhaa aliongoza wizara mbalimbali na kwa vipindi viwili alikuwa Waziri Mkuu wa Uingereza.

 

Siku kama hii ya leo miaka 47 iliyopita sawa na tarehe 4 Bahman mwaka 1357 Hijria Shamsiya, Shapour Bakhtiar Waziri Mkuu wa utawala wa Shah ambaye alikuwa akielewa kuwa kurejea Imam Khomeini nchini kutoka uhamishoni Paris kungempokonya udhibiti wa hali ya mambo, alitoa amri ya kufungwa viwanja vyote vya ndege vya Iran ili kuzuia kurejea nchini Imam Khomeini. Shapour Bakhtiar alichukua hatua hiyo baada ya kuchapishwa habari ya kukaribia kuwasili hapa nchini Imam Khomeini kutoka uhamishoni huko Paris Ufaransa. Hatua hiyo ya serikali ya utawala wa Shah iliwakasirisha wananchi ambao walikuwa wakisubiri kwa hamu kubwa ujio huo wa Imam Ruhullah Khomeini nchini Iran.