Aug 26, 2026 05:56 UTC
  • Jumatano, tarehe 26 Agosti, 2026

Leo ni Jumatano tarehe 13 Rabiul Awwal 1448 Hijria sawa na tarehe 26 Agosti 2026.

Katika siku kama ya leo miaka 1158 alizaliwa Qadhi Jorjani maarufu kwa lakabu ya Abulhassan, faqihi, mwandishi na malenga wa Kiislamu. 

Jorjani alifunzwa masomo hayo ya kidini na Qadhi Mkuu wa mji wa Rey ulioko karibu na Tehran ya leo. Qadhi Jorjani ameandika vitabu vingi na miongoni mwake ni "Tafsirul Qur'an" na "Tahdhibul Tarikh".

Qadhi Jorjani alifariki dunia mwaka 366 Hijria huko Neishabur na akazikwa huko Jorjan au Gorgan ya leo kaskazini mashariki mwa Iran. ****

Katika siku kama ya leo miaka 680 iliyopita mzinga mkubwa ulitumika kwa mara ya kwanza katika historia.

Siku hiyo jeshi la Uingereza lilitumia silaha ya mzinga dhidi ya askari wa Ufaransa.

Katika vita hivyo Mfalme Philip wa Sita wa Ufaransa alishindwa vibaya na jeshi la Uingereza licha ya kwamba jeshi la Ufaransa lililokuwa limekaribia kupata ushindi, lilikuwa na idadi kubwa ya askari na wapiganaji. Ushindi wa jeshi la Uingereza katika vita hivyo ulitokana na utumiaji wa silaha ya mzinga.   ****

Miaka 283 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa mjini Paris Ufaransa Antoine Laurent Lavoisiere, mtaalamu wa kemia wa Kifaransa.

Baada ya kumaliza masomo yake alianza kufanya utafiti katika elimu ya kemia. Miongoni mwa uvumbuzi wa msomi huyo ni kwamba, maji yanaundwa na vitu viwili yaani gesi za oksijeni na haidrojeni na mchango wa hewa ya oksijeni katika kuchomeka vitu mbalimbali.

Mwaka 1794 Antoine Laurent Lavoisiere alituhumiwa kuwa anapinga mapinduzi na kunyongwa hapo baadaye. ***

Siku kama ya leo miaka 130 iliyopita askari wa utawala wa Kiothmani walianza kufanya mauaji ya umati dhidi ya Waarmenia.

Waturuki wa Kiothmani walifanya mauaji hayo kwa kisingizio kwamba Waarmenia waliwasaidia Wagiriki katika ghasia zilizofanyika dhidi ya utawala wa Kiothamani. Maelfu ya wanawake, wanaume na watoto wadogo wa Kiarmeni waliuawa kwa umati katika mauaji hayo yaliyoendelea kwa kipindi cha siku tano.   ***

Katika siku kama hii ya leo miaka 47 iliyopita tarehe 4 Shahrivar 1358 Hijria Shamsia, Mahdi Araghi na mwanawe Hissam waliuawa shahidi na magaidi wa kundi la Munafiqin (MKO).

Mahdi Araghi alikuwa mmoja wa shakhsia watajika wa Mapinduzi ya Kiislamju ya Iran na alipambana kwa miaka kadhaa dhidi ya utawala wa Shah.

Mahdi Araghi alikuwa na uhusiano wa karibu na Imam Khomeini MA. Mwanamapambano huyo muumini alifungwa jela na utawala wa Shah kwa miaka kadhaa na kukumbana na mateso mengi.