Jumanne, Agosti 25, 2026
-
Leo Katika Historia
Leo ni Jumanne tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1448 Hijria sawa na 25 Agosti, 2026.
Katika siku kama ya leo miaka 1501 inayosadifiana na tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal miaka 53 kabla ya Hijria, kwa kauli ya baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu akiwemo Mas'udi, alizaliwa Mtume Muhammad SAW.
Wanachuoni wengine wa Kiislamu wanaamini kwamba, Mtume Muhammad (saw) alizaliwa tarehe 17 Rabiul Awwal mwaka huohuo. Kwa msingi huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza kipindi cha kuanzia tarehe 12 hadi 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal kila mwaka kuwa ni Wiki ya Umoja kati ya Waislamu kote duniani.
Wiki ya umoja ni fursa nzuri ya kuzikurubisha nyoyo za Waislamu na kuimarisha umoja na mshikamano wao katika kukabiliana na maadui wa Umma wa Kiislamu. ****
Tarehe 12 Rabiul Awwal mwaka wa kwanza Hijria, Mtume Muhammad (saw) aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa msikiti wa kwanza kabisa katika Uislamu katika kijiji cha Quba kilichoko pambizoni mwa Madina.
Mtume (saw) aliweka jiwe la msingi la msikiti huo wa kihistoria wakati aliposimama kwa siku chache katika eneo la Quba akiwa njiani kutoka Makka akielekea Madina. Mtukufu huyo alisimama kwa muda katika kijiji cha Quba akimsubiri Ali bin Abi Twalib na jamaa wa familia ya Mtume. ***
Siku kama ya leo miaka 1207 iliyopita, inayosadifiana na 12 Rabiul Awwal 241 Hijria, alifariki dunia Imam Ahmad bin Hanbal, mmoja kati ya maulamaa wakubwa wa Kiislamu katika mji wa Baghdad, Iraq ya leo.
Ahmad bin Hanbal alizaliwa mwaka 124 Hijria, katika mji wa Baghdad na kujipatia elimu ya kidini katika mji huo kutoka kwa maulamaa wakubwa akiwemo Imam Shafii. Imam Hanbal amesafiri katika miji kadhaa kama vile Kufa, Basra, Makka, Madina, Sham na Yemen kwa minajili ya kukusanya hadithi za Bwana Mtume SAW.
Ahmad bin Hanbal ni mwasisi wa Madhehebu ya Kisuni ya Hanbal na ameacha kitabu mashuhuri cha hadithi, kiitwacho al Musnad. ***
Katika siku kama ya leo miaka 931 iliyopita sawa tarehe 25 Agosti mwaka 1095, vilianza Vita vya Msalaba kati ya Wakristo na Waislamu.
Watu wa msalaba walianzisha vita hivyo kidhahiri wakiwa na lengo la kuteka Baitul Muqaddas, ingawa shabaha halisi ya wapiganaji hao ilikuwa kudhibiti ardhi kubwa za Waislamu, kuwanyonya na kuwakoloni wafuasi wa dini hiyo.
Katika vita hivyo wafuasi wa kanisa walichora alama za msalaba kwenye mabega na mavazi yao, na kwa sababu hiyo vita hivyo vimekuwa maarufu kwa jina la Vita vya Msalaba. Baada ya vita vingi na Waislamu, wapiganaji wa msalaba hatimaye waliuteka na kuukalia kwa mabavu mji wa Baitul Muqaddas mnamo mwaka 1099, ambako waliua raia wengi na kupora mali zao. Mji huo ulikombolewa mwaka 1187 na wapiganaji wa Kiislamu waliokuwa wakiongozwa na Salahuddin Ayyubi. ***
Miaka 201 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo, Uruguay ilipata uhuru. Tangu Uruguay ivumbuliwe na wagunduzi wa Kihispania mwaka 1516, ilitawaliwa na Wareno na Wahispania.
Baina ya mwaka 1810 na 1814 kulitokea uasi uliopelekea umwagaji damu mkubwa, ambapo baada ya matukio hayo, nchi hiyo ilipata huru wa kiasi fulani. Hata hivyo mwaka 1820 Brazil iliikalia tena kwa mabavu na miaka mitano baadaye Uruguay ikajikomboa na kujipatia uhuru kamili. ***
Katika siku kama hii ya leo miaka 159 iliyopita alifariki dunia msomi mashuhuri wa Uingereza, Michael Faraday.
Faraday alizaliwa mwaka 1791 mjini London na licha ya kuwa hakuwa na elimu ya juu lakini alifanikiwa kupata maendeleo muhimu katika fizikia na kemia kwa kutumia majaribio na tajiriba. Michael Faraday aligundua chombo cha mkondo wa umeme kinachojulikana kwa kitaamu kama ''Electric Current''.
Kwa ugunduzi huo Faraday akawa amefanikiwa kupiga hatua kubwa katika elimu ya fizikia. Miongoni mwa mafanikio mengine makubwa yaliyoletwa na mtaalamu huyo ni pale alipogundua mota ya umeme pamoja na kubadilisha nguvu za sumaku kuwa nguvu za umeme.