Aug 23, 2026 02:44 UTC
  • Leo katika Historia
    Leo katika Historia

Leo ni Jumapili 10 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1448 Hijria mwafaka 23Agosti 2026 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1493 iliyopita alifariki dunia babu wa Mtume, Abdul Muttalib katika mji wa Makka.

Mtukufu huyo alikuwa miongoni mwa wakuu wa kabila la Quraish kabla ya kudhihiri Uislamu na alikuwa hodari mno katika fasihi ya lugha ya Kiarabu. Bwana Abdul Muttalib alikuwa msimamizi na mshika ufunguo wa nyumba tukufu ya al-Kaaba. Vilevile babu huyo wa Mtume alikuwa akitayarisha chakula na maji kwa ajili ya watu wanaozuru nyumba hiyo ya Mwenyezi Mungu na kazi hiyo aliirithi kutoka kwa baba yake. Aliheshimu mno mikataba na ahadi zake na kwa sababu hiyo alikuwa na ushawishi mkubwa baina ya watu. Miongoni mwa watoto wa mtukufu huyo ni Abdullah, baba yake Mtume wetu Muhammad (saw) na Abu Twalib, baba yake Imam Ali bin Abi Twalib (as).

***

Tarehe 10 Rabiul Awwal miaka 1474 iliyopita, miaka 28 kabla ya Hijra, Mtukufu Mtume Muhammad (saw) alimuoa Bibi Khadija binti Khuwailid (as). Bibi Khadija alikuwa mwanamke sharifu, mwenye imani na maarufu kwa ukarimu wake katika zama za ujahilia na alikuwa maarufu kwa lakabu ya "Twahira" kwa maana ya msafi na mtoharifu. Baada ya kufunga ndoa na Nabii Muhammad (saw) Bibi Khadija alikuwa msaidizi mkubwa na mwenzi wa mtukufu huyo katika hatua zote za maisha yake. Alisabilia kila kitu kwa ajili ya Uislamu na Mtume Muhammad (saw). Bibi Khadija (as) aliishi pamoja na Mtume kipindi cha miaka 25 na daima alikuwa mke mwema na mwenye kujitolea kwa mumewe Mtume Muhammad (saw) mbora wa walimwengu. 

***

Tarehe Mosi Shahrivar katika kalenda ya mwaka wa Hijria Shamsia ni siku ya kumuenzi Hassan bin Abdullah maarufu kwa jina la Abu Ali Sina na siku ya daktari. Abu Ali Sina alizaliwa tarehe 3 Safar mwaka 370 Hijria katika eneo la Balkh na kujifunza elimu za zama hizo akiwa bado kijana hadi alipopata umashuhuri mkubwa katika taaluma mbalimbali na kutambuliwa kuwa gwiji wa zama hizo. Alikuwa miongoni mwa wanafalsafa, maurafa na matabibu wakubwa. Ibn Sina alihifadhi Qur'ani yote alipokuwa na umri wa miaka 10. Alijifunza utabibu baada ya kupata elimu za mantiki, hisabati, nujumu, falsafa pamoja na elimu nyinginezo.  Alianza kuandika vitabu akiwa na umri wa miaka 21 na miongoni mwa vitabu vyake maarufu ni Qanun, Shifaa na Isharaat.

***

Siku kama ya leo, miaka 82 iliyopia mji wa Paris ulikombolewa kutoka kwenye uvamizi wa Ujerumani. Miezi 15 baada ya kushtadi moto wa Vita vya Pili vya Dunia na katika kuendeleza njama zake za kutaka kujitanua, dikteta Adolph Hitler aliyaamuru majeshi ya nchi hiyo kuushambulia mji wa Paris kwa lengo la kutaka kuudhibiti mji huo. Tarehe tano Juni mwaka 1940, Hitler alitoa amri ya kuharibiwa kikamilifu muundo wa majeshi ya Ufaransa na siku tatu baadaye yaani tarehe nane Juni mwaka 1940, vikosi vya Wanazi vilikishinda kikosi cha ulinzi cha Ufaransa katika eneo la kaskazini mashariki mwa taifa hilo, na hivyo kutoa mwanya kwa jeshi la Ujerumani kuingia nchini Ufaransa. 

***

Siku kama ya leo miaka 23 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 23 Agosti 2003, alifariki dunia Michael Kijana Wamalwa, Makamu wa Rais wa Kenya. Wamalwa alizaliwa 25 Novemba 1944 katika kijiji cha Sosio karibu na Kimilili, wilayani Bungoma. Michael Kijana Wamalwa alikuwa mtoto wa mwanasiasa na mbunge machachari William Wamalwa. Mwaka 2002, Wamalwa akiwa pamoja na wanasiasa wengine mashuhuri nchini Kenya, wakiongozwa na Mwai Kibaki wa chama cha National Rainbow Coalition NARC, walifanikiwa kuung'oa madarakani utawala wa chama cha KANU uliotawala nchi hiyo kwa zaidi ya miongo minne. Kijana Wamalwa alizikwa kwenye shamba lake lililoko Kitale.