Jumatatu, 24 Agosti, 2026
Leo ni Jumatatu tarehe 11 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1448 Hijria sawa na 24 Agosti, 2026.
Siku kama ya leo miaka 155 iliyopita alizaliwa mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Allamah Agha Bozorge Tehrani.
Alipata elimu ya msingi mjini Tehran na baadaye alielekea Najaf, Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Allamah Agha Bozorge Tehrani alikweya kwa kasi daraja za elimu na kuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa kidini. Allamah Tehrani alisafiri na kufanya uchunguzi katika maktaba nyingi za nchi kama Iran, Misri, Syria, Iraq, Hijaz, Palestina na kadhalika kwa ajili ya kutayarisha ensaiklopedia ya vitabu vya Kiislamu. Alifanikiwa kuandika tabu hilo kubwa lenye juzuu 26 ambalo alilipa jina la "Adhari'a ila Tasaanifish Shia".
Kitabu kingine muhimu cha Allamah Agha Bozorge Tehrani ni "Tabaqatu Aalami Shia" chenye juzuu 8. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia katika mji mtakatifu wa Najaf na kuzikwa katika maktaba yake kama alivyokuwa ameusia. ****
Siku kama ya leo miaka 97 iliyopita, yalianza mapambano ya Ukuta wa Nudba huko Baitul Muqaddas.
Ukuta wa Nudba huko magharibi mwa Masjidul Aqswa ni eneo alilotumia Mtume Muhammad (saw) wakati wa kupaa mbinguni katika safari ya Mi'iraj na kwa sababu hiyo eneo hilo likawa na umuhimu wa kidini na kihistoria kwa Waislamu. Tangu wiki moja kabla ya kuanza mapambano hayo ya Ukuta wa Nudba, Wazayuni ambao taratibu walikuwa wameanza kuikalia kwa mabavu Palestina kwa kuungwa mkono na Uingereza, walianzisha harakati dhidi ya Waislamu.
Siku hiyo Wapalestina wenye hasira walianzisha mapambano makali dhidi ya Wazayuni hao maghasibu. Mapambano hayo yalienea kwa kasi kwenye miji mingine ya Palestina na Waingereza wakaamua kutangaza utawala wa kijeshi huko Palestina kwa kuhofia hasira za Wapalestina. ***
Katika siku kama ya leo miaka 94 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia Ayatuullah Sayyid Hassan Sadr mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu.
Alikuwa mmoja wa mafakihi ambao walipata daraja ya Ij’tihad katika kipindi cha ujana. Sayyid Hassan Sadr alikuwa katika orodha ya walimu mashuhuri katika Chuo KIkuu cha Kidini cha Najaf, Iraq. Aliondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Sadruddin katika taaluma za fikihi, Usu, teolojia, falsafa na Hadithi. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya Sayyid Hassan Sadr ni Taasis al-Shi'a na al Kiram Lifununi al Islam. ***8
Miaka 48 iliyopita katika siku kama hii ya leo Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Ali Andarzgu aliuawa shahidi na vibaraka wa utawala wa Shah.
Shahidi Andarzgu alianza harakati za mapambano akiwa na umri wa miaka 19 na kufahamiana kwa karibu shahidi Nawab Safawi, kiongozi wa kundi la Waislamu wanamapinduzi.
Baada ya hapo Shahid Andarzgu alijiunga na harakati ya Muutalifeye Eslami na alikuwa miongoni mwa waliotekeleza mauaji ya kimapinduzi dhidi ya Waziri Mkuu wa wakati huo wa Shah, Hussein Ali Mansour.
Shahid Andarzgu aliendesha mapambano ya siri dhidi ya utawala wa Shah kwa kipindi cha miaka 13 na hatimaye aliawa shahidi shahidi na vibaraka wa Shah katika siku kama hii ya leo katika mapambano ya silaha. ****
Siku kama leo miaka 35 iliyopita, Ukraine ilipata uhuru toka kwa Umoja wa Kisovieti.
Russia ilianza kuikalia kwa mabavu Ukraine ambayo wakati huo ilikuwa chini ya udhibiti na utawala wa Poland, katikati mwa karne ya 17 Miladia. Hata hivyo mwaka 1922, nchi hiyo iliunganishwa na mataifa yaliyokuwa yakiunda Umoja wa Sovieti.
Hatimaye katika tarehe kama ya leo, Ukraine ikajipatia uhuru wake. ***