Sep 07, 2016 03:51 UTC
  • Jumatatu tarehe tarehe 5 Septemba 2016

Leo ni Jumatatu tarehe 3 Dhilhija 1437 Hijria sawa na tarehe 5 Septemba 2016.

Tarehe 5 Septemba miaka 23 iliyopita moja kati ya misikiti mikubwa na ya kuvutia zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu ulifunguliwa rasmi huko Casablanca nchini Morocco. Msikiti huo ndio wenye nafasi kubwa zaidi baada ya Masjidul Haram huko Makka. Usanifu majengo wa msikiti huo ulibuniwa na mhandisi wa Kifaransa ambaye alichanganya teknolojia ya kisasa na sanaa ya usanifu majengo wa Kiislamu. Pembeni ya msikiti huo kumejengwa maktaba ya kisasa na chuo cha Kidini.

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, baada ya kupamba moto harakati za mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran dhidi ya utawala wa kidikteta wa Shah, kulifanyika maandamano makubwa katika maeneo mbalimbali kote nchini. Kwa sababu hiyo utawala wa Shah uliokuwa umepatwa na wasiwasi mkubwa kutokana na harakati hizo za mapinduzi, uliamua kupiga marufuku maandamano ya aina yoyote ile. Wakati huo huo Imam Ruhullah Khomeini MA aliyekuwa uhamishoni huko Najaf nchini Iraq alitoa taarifa akiwataka wananchi wa Iran kudumisha harakati za mapambano. Katika sehemu moja ya taarifa yake kwa wananchi, Imam Khomeini aliyataja maandamano yanayofanywa kwa ajili ya kufikia malengo ya Kiislamu kuwa ni ibada.

Miaka 111 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 5 Septemba mwaka 1905, mkataba wa Portsmouth ulitiwa saini na hivyo kufikia tamati vita kati ya Russia na Japan. Februari 8 mwaka 1904, vikosi vya Japan vilifanya mashambulio ya kushtukiza dhidi ya meli za kivita za Russia na kisha kuyadhibiti kwa askari wa miguu maeneo ya Manchuria ambayo yalikuwa chini ya mamlaka ya Russia. Russia ilipata vipigo vya mfululizo katika vita hivyo. Hatimaye kwa upatanishi wa Marekani, katika siku kama ya leo pande mbili zikatiliana saini mkataba wa Portsmouth na huo ukawa mwisho wa vita kati ya Japan na Russia.

Na miaka 129 iliyopita mwafaka na tarehe 5 mwezi Septemba mwaka 1887, mto mkubwa wa Huang He huko China ulianza kufurika maji. Mafuriko hayo makubwa yalisababishwa na kujaa maji katika mto huo kwa zaidi ya mwezi mmoja. Zaidi ya watu laki tisa walipoteza maisha katika mafuriko hayo na taathira zake mbaya. Aidha miji kadhaa, mamia ya vijiji na mashamba mengi yaliharibiwa baada ya kukumbwa na mafuriko ya mto huo.

Tags