Sep 09, 2016 13:46 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (134)8

Kipindi chetu cha juma hili cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain kitaendelea kuzungumzia aya ambazo zinajibu swali letu la kiitikadi kuhusiana na msingi wa Uimamu ambalo tumekuwa tukilijadili katika vipindi kadhaa vilivyopita.

Swali inasema: Je, ni kwa nini Mtume Mtukufu wa Uislamu (saw) alisisitiza katika hadithi ya Thaqalain ambayo ni hadithi inayoaminika na ambayo imenukuliwa kwa wingi katika vitabu vya kuaminika vya madhehebu zote mbili za Shia na Suni, kwamba kuepuka upotovu hutimia tu kwa kushikamana kikamilifu na kwa pamoja na vitu viwili vizito kwa thamani, ambavyo ni kitabu kitakatifu cha Mwenyezi Mungu, Qur’ani Tukufu na Ahlul Beit watoharifu wa Mtume Mtukufu (saw). Tulipata kujua katika vipindi vilivyopita kwamba hadithii hii ya Mtume (saw) ni tafsiri na ufafanuzi wa aya kadhaa tukufu zikiwemo za 43 na 44 za Surat an-Nahl na aya ya 7 ya Surat Aal Imran.

Aya hizi zinasisitiza kwamba ni katika rehema na neema kubwa ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake kwamba aliagiza Manabii na mawasii wao kubainisha na kufafanua makusudio na hakika ya wahyi na ufunuo wake mtakatifu na hilo ndilo jambo ambalo lilitimia pia kuhusiana na Qur’ani Tukufu. Hii ni kwa sababu alimfundish kikamilifu Mtume wake Muhammad (saw) elimu na maarifa yote ya Qur’ani Tukufu ili apate kuwafafanulia watu na kulifanya jambo hilo kuwa hoja kamili kwa waja. Mtume aliwafundisha Waislamu mafundisho ya kitabu hicho kitakatifu ili wapate kuongoka na kuwa wakakamavu katika kufuata njia nyoofu ya kuelekea kwa Mola wao, na hilo kuwakinga na fitina za maimamu wa upotovu na giza ambao hufuata aya za mifano katika Qur’ani na kuzifasiri kama wanavyotaka kwa msingi wa matamanio yao binafsi  ili kuwafanya watu wapate kuwaabudu.

Baada ya kuondoka Mtume Mtukufu (saw) humu duniani, aliwarithisha elimu hiyo yenye thamani kubwa mawasii wake watoharifu na wasiotenda dhambi ili wapate kuendeleza ujumbe wake wa mbinguni. Kwa hakika hili ni dhihirisho, suna na kanuni ya Mwenyezi Mungu katika kuwaongoza wanadamu ambapo aliwajaalia hoja mbili ya kwanza ikiwa ni ya batini na dhati ambayo ni akili na sheria za maumbile salama na ya pili ni ya dhahihiri ambao ni Mitume na Manabii pamoja na mawasii wao ambao hukamilisha akili na maumbile hayo kwa kuyahamasisha kupitia ufafanuzi wao wa mafundisho matakatifu ya mbinguni.

 

Hapa, hebu na tuzinagtie kwa pamoja aya za 75 hadi 80 za Surat al-Waaqia ambazo zinasema: Basi naapa kwa maanguko ya nyota! Na hakika bila ya shaka hiki ni kiapo kikubwa, lau mngelijua! Hakika hii bila ya shaka ni Qur'ani Tukufu. Katika Kitabu kilichohifadhiwa. Hapana akigusaye ila waliotakaswa. Ni uteremsho unaotoka kwa Mola wa walimwengu wote.

Ndugu wasikilizaji Maimamu Watukufu (as) na wanazuoni wakubwa wa Kiislamu wametolea hoja aya hii inayosema, Hapana akigusaye ila waliotakaswa, kuashiria katazo la Mwenyezi Mungu la kuguswa maandiko yake matakatifu katika Qur’ani Tukufu na watu ambao si wasafi, yaani wasiokuwa na wudhu, na hii ni kwa ajili ya kuonyesha utakatifu na utukufu wa kitabu hicho cha mbinguni. Na Katika hatua ya juu zaidi, Mwenyezi Mungu amekisifu kitabu chake hicho kuwa ni Kitabu kilichohifadhiwa, kumaanisha kwamba kitabu hicho kina siri na hakika nyingi ambazo zimefichwa na Mwenyezi Mungu mbele ya macho ya walimwengu na kwamba hakuna mtu anayefahamu na kufikia siri hizo isipokuwa kundi dogo tu maalumu la watu wema ambao ndio hao waliotakaswa.

Kwa kuzingatia ujumla uliobainishwa katika kuzungumzia suala hili la mambo yaliyohifadhiwa katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu na kadhalika ujumla uliotumika katika kuwasifu watu waliotakaswa, hakika ifuatayo inatubainikia wazi, nayo ni kwamba: Katika Qur’ani Tukufu kuna mambo yaliyohifadhiwa ambayo hakuna mtu anayeyafahamu isipokuwa watu wachache tu waliotakaswa. Ukanushaji huo ni wa moja kwa moja kwa maana kwamba unawajumuisha watu wote isipokuwa kundi la wema wachache ambao wametakaswa na Mwenyezi Mungu. Hii ni kwa sababu utakasaji kamilifu hautimii ila kwa msaada wa Mwenyezi Mungu mwenyewe.

Aya ya Tat’hir imetufahamisha utambulisho wa watu hao waliotakaswa na Mwenyezi Mungu ambapo imethibiti kupitia hadithi za kuaminika za madhehebu zote mbili za Kiislamu za Shia na Suni kwamba aya hiyo ilimukusudia Mtume Mtukufu (saw) na Ahlul Beit wake watoharifu ambao ni Imam Ali, Fatuma na watoto wao wawili, al-Hassan na al-Hussein (as) tu.

Allamah Tabatabai anasema katika kufasiri aya hii inayosema hapana akigusaye ila waliotakaswa, katika tafsiri yake ya al-Mizan kwamba kusudio ni kuadhimisha na kutukuza Qur’ani Tukufu na kwamba kugusa hapa kuna maana ya kufahamu elimu iliyomo ambayo iko kwenye Kitabu kilichohifadhiwa, yaani katika hatua ya juu zaidi, kama anavyosema Mwenyezi Mungu mwenyewe katika aya ya 3 na 4 za Surat az-Zukhruf zinazosema: Hakika Sisi tumeifanya Qur'ani kwa Kiarabu ili mfahamu. Na hakika hiyo imo katika mama wa Kitabu (Asili ya Maandiko) kilicho kwetu, ni tukufu na yenye hikima.

Kisha Allamah (MA) anaendelea kusema kwamba neno la Kiarabu la ‘mutwahharun’ lililotumika katika aya ya waliotakaswa tunayoijadili hapa ni jina la mtendewa kitendo cha utakasaji nao ni wale watu ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu ametakasa nyoyo zao kutokana na uchafu wa maana na dhambi au kutokana na jambo ambalo ni la juu zaidi nalo ni la kutakasa nyoyo zao kutokana na mafungamano ya asiyekuwa Mwenyezi  Mungu. Allamah Tabatabai anasema kuwa waliotakaswa ni wale watu waliotukuzwa na Mwenyezi Mungu kwa kutakasa nyoyo zao kama vile Malaika na waja wema katika wanadamu kama anavyosema Mwenyezi Mungu katika aya ya Tat’hir: Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba ya Mtume, na kukutakaseni kabisa kabisa, na hapa hakuna sababu wala hoja ya yoyote kubanwa utakasaji huo katika Malaika peke yao.

 

Wapenzi wasikilizaji kile ambacho kimetajwa na baadhi ya wafasiri kuwa ni Malaika ndio wanaokusudiwa na neno ‘mutwahharun’ au waliotakaswa katika aya tukufu tuliyosoma, kwa hakika hakiashiriwi na aya yenyewe na wala hilo halijatajwa katika hadithi wala maneno yoyote ya Mtume Mtukufu (saw) ambaye amekingwa na kutenda dhambi. Baadhi ya watu wameeneza maana hii kwa lengo la kufunika makusudio halisi ya watu waliotakaswa waliotajwa kwenye aya hii ya Tat’hir ambao ni Mtume Muhammad (saw) na Ahlul Beit wake watoharifu (as). Sira na mwenendo wa maisha ya watukufu hawa ulibainisha na kuthibitisha wazi maneno ya Mwenyezi Mungu kuhusiana nao. Kwa mfano Allamah Tabatabai anasema katika kubainisha kiwango cha ikhlasi ya watukufu hawa katika kuabudu na kumpwekesha Mwenyezi Mungu, katika juzuu ya 11 ukurasa wa 160 wa Tafsiri yake ya al-Mizan kwamba, ibada ya watukufu hawa ilikuwa ya kiwango cha juu na ya aina yake tofauti kabisa na wanadamu wengine ambao humuabudu Mwenyezi Mungu ima kwa kuhofia adhabu yake au kwa kuwa na tamaa ya kuingizwa kwenye Pepo Siku ya Kiama. Anasema kwamba kama watu wa aina hii wangeweza kupata Pepo bila kumuabudu Muumba wao basi wangepuuza na kusahau kabisa ibada Yake. Hali hii ni tofauiti kabisa na kama walivyokuwa watukufu wa Ahlul Beit wa Mtume (saw) akiwemo Imam Swadiq (as) ambaye anasema: ‘Je, dini ni jambo jingine isipokuwa mahaba?’ Pia anasema (as): ‘Hakika mimi ninamwabudu kutokana na mahaba niliyonayo Kwake.’ Allamah anamalizia kwa kusema kuwa hiki ni cheo cha juu zaidi kilichohifadhiwa ambacho hakifikii mtu yoyote isipokuwa wale waliotakaswa.

**********

Ndugu wasikilizaji, madhehebu zote mbili za Kiislamu zimepokea riwaya nyingi ambazo zinathibitisha Ahlul Beit wa Mtume (asaw) kufikia kiwango hiki cha juu cha utukufu cha kumpwekesha Mwenyezi Mungu katika kila jambo na hivyo kumfanya Mwenyezi Mungu kuwapa cheo cha utukufu na utakaswaji, ambacho kinawawezesha kufikia maarifa na hakika zilizofichwa na kuhifadhiwa na Mwenyezi Mungu katika kitabu chake kitakatifu na hilo ndilo jambo tukufu zaidi ambalo liko kwenye kitabu hicho.

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji, inabainika wazi kwamba kufikia hakika hizo tukufu na kufuzu kunufaika nazo hakutimii ila kwa kushikamana na watukufu hawa na kuwafuata kikamilifu, na ndio maaa Mtume Mtukufu (saw) akasisitiza katika hadithi ya Thaqalain juu ya udharura wa kushikamana kwa pamoja na Qur’ani Tukufu na Ahlul Beit wake (as) kama njia pekee ya kufikia wokovu na kuepuka upotovu wa kila aina.

Tutafafanua zaidi hakika hii ya Qur’ani Tukufu katika kipindi chetu kijacho cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain, panapo majaaliwa. Basi hadi wakati huo kutoka Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu inayokutangazia kutoka hapa mjini Tehran hatuna la ziada ila kukuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warhmatullahi Wabarakatuh.