Ijumaa, 04 Novemba, 2016
Leo ni Ijumaa tarehe 4 Safar 1438 sawa na Novemba 4, 2016.
Siku kama ya leo miaka 21 iliyopita Waziri Mkuu wa wakati huo wa utawala ghasibu wa Israel Yitzhak Rabin aliuawa kwa kupigwa risasi na Mzayuni mwenye misimamo mikali. Rabin alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel kwa tiketi ya chama cha Leba katika mwaka ya 1974 na kuongoza hadi 1977 lakini alilazimika kujiuzulu kutokana na ubadhirifu wa mali ya umma. Alichaguliwa tena kuwa Waziri Mkuu wa Israel mwaka 1992 na kudumisha mazungumzo eti ya amani ya Mashariki ya Kati. Mauaji ya Yitzhak Rabin yaliyofanywa na Myahudi mwenzake Yigal Amir ni mfano wa wazi wa hitilafu kubwa zilizoko kati ya viongozi wa utawala unaoikalia Palestina kwa mabavu wa Israel. Ni muhimu kukumbusha kuwa, Yitzhak Rabin alikuwa miongoni mwa makamanda wa makundi ya kigaidi ya Kizayuni.
Miaka 29 iliyopita katika siku kama hii ya leo kulifunguliwa maonyesho ya kwanza ya kimataifa ya vitabu mjini Tehran. Maonyesho hayo yalishirikisha makampuni na taasisi 196 za uchapishaji vitabu za kigeni kutoka nchi 32 duniani yaliyokuwa na vitabu zaidi ya elfu 16. Vilevile taasisi 215 za uchapisha za ndani ya Iran zilishiriki katika maonyesho hayo. Tangu mwaka huo maonyesho ya kimataifa ya vitabu ya Tehran yamekuwa yakifanyika kila mwaka hapa nchini.
Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, wakati wa kuendelea harakati za mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala dhalimu wa Shah, serikali ya Sharif Emami ililazimika kujiuzulu. Jafar Sharif Emami alikuwa kibaraka wa siri wa ukoloni wakati wa kupamba moto harakati za wananchi Waislamu na alikuwa akitoa ahadi za uongo kwa lengo la kupotosha muelekeo wa Mapinduzi ya Kiislamu. Hata hivyo Imam Khomeini alitambua njama na hila za kiongozi huyo na kutangaza kwamba, mawaziri wanaobadilishwa ni vibaraka wa Shah na ubeberu na akawataka wananchi wasihadaike na hila za viongozi hao bali waendeleze harakati za mapambano za kutaka kuuangusha utawala dhalimu wa Shah.