Jan 29, 2017 07:07 UTC
  • Maadhimisho ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sehemu ya Kwanza)

Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika mfululizo huu wa vipindi kadhaa tulivyokuandalieni kwa mnasaba wa maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran. Ni matumaini yetu mtakuwa nasi hadi mwisho wa mfululizo huu ambao tutakuwa nao kila siku hadi yatakapofikia kileleni maadhimisho hayo yaani siku ya Ijumaa ya tarehe 10 Februari.

Mpenzi msikilizaji, ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ulifungua ukurasa mpya katika historia ya taifa la Iran ukurasa ambao una umuhimu mkubwa sana katika upande wa kuwa huru taifa la Iran na kujikomboa kutoka kwenye makucha ya mfumo wa kibeberu sambamba na kujiletea wenyewe wananchi wa Iran ustawi na maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia. Makala yetu ya leo itatupia jicho kwa muhtasari hatua kubwa zilizopigwa na Iran katika njia ya ustawi na maendeleo kwenye kipindi hiki cha miaka 38 ya baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Hivi sasa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamekamilisha miaka 38 ya tangu kupata ushindi. Tangu siku zake za mwanzoni kabisa, mapinduzi hayo yamesimama imara kupambana na mfumo wa kibeberu ulimwenguni. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ulikuwa mwanzo wa mabadiliko makubwa katika nyuga zote kwa taifa la Iran na yameliletea baraka nyingi taifa hili. Uhuru na kujitegemea ni miongoni mwa mabadiliko makubwa yaliyoletwa na ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu pamoja na kuundwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa wingi mutlaki wa kura za wananchi. Uhuru huu umeliletea heshima kubwa taifa la Iran na umetoa ilhamu kwa mataifa mengi yanayopigania kujikomboa katika kona tofauti za dunia. Uhuru na kujitawala kikamilifu taifa la Iran unaonekana kwa uwazi kabisa katika hotuba za Imam Khomeini (MA) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika moja ya hotuba zake hizo muhimu sana alisema:

Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu

 

Sisi tulikuwa ni taifa lililopoteza uhuru wake kutokana na mashinikizo ya Marekani na madola mengine ya kibeberu. Uhuru wetu ulikuwa umepotea. Utajiri wetu ulikuwa ukipotea bure. Hivyo sisi tumesimama kufanya mapinduzi ili kurejesha uhuru wetu. Tumefanya mapinduzi ili kujikomboa.

Naam, mpenzi msikilizaji, kutokana na kusimama kwake imara katika malengo yake matukufu na katika kaulimbiu zake za kimataifa, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamefanikiwa kuleta mabadiliko makubwa, na ili kuweza kuyaona na kuyadiriki matunda mengi ya kila namna ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, inabidi mtu kuwa na muono wa mbali na welewa wa kutosha kuhusu utambulisho, matukufu na matunda ya mapinduzi hayo.

Hivi sasa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamekaribia kumaliza miongo minne tangu yalipopata ushindi. Kuna matunda mengi na ya kila namna yamepatikana kutokana na Mapinduzi hayo matukufu na matunda ya juu kabisa ni kukata kikamilifu utegemezi wa taifa la Iran kwa mabeberu katika upande wa kisiasa na kiutamaduni. Aidha mapinduzi hayo yameliletea taifa la Iran maendeleo ya kiuchumi, uhuru unaokwenda sambamba na kujali watu majukumu yao, kujiamini na kupata nguvu fikra ya kupigania ukombozi na uadilifu. Mapinduzi ya Kiislamu tangu yalipopata ushindi hadi kwenye kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu vilivyoanzishwa na utawala wa zamani wa Saddam huko Iraq na baada ya vita hivyo, yamekuwa yakikabiliwa na njama za kila namna za kijeshi na kisiasa kutoka kwa maadui, lakini pamoja na hayo yote taifa la Iran halijatetereka hata kidogo na limefanikiwa kupiga hatua kubwa za kimaendeleo kwa kutegemea uwezo wake wa ndani na kufanikiwa kuyalinda Mapinduzi ya Kiislamu mbele ya mawimbi na mashambulizi ya kila upande ya maadui.

Katika hotuba yake aliyoitoa tarehe 7 Februari 1993, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema:

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

 

Mapinduzi ya Kiislamu yamehuisha na kufufua utambulisho wa Kiislamu kati ya Waislamu duniani, yameleta mwamko wa mataifa ya dunia na kuleta nishati na matumaini kwa vikosi vya wanamapambano na wanamapinduzi duniani na hayo ni matunda ya wazi kabisa na yasiyokanushika ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Taathira nyingine za Mapinduzi ya Kiislamu ni kwamba yamemwamsha adui wa Mapinduzi ya Kiislamu na ndio maana leo hii tunaona jinsi kambi iliyoungana ya kibeberu ikiwemo Marekani na madola yenye fikra mgando, kambi ya wachokozi na iliyo dhidi ya wananchi wao pamoja na madola mengine ya kibeberu duniani ambayo yanadhani dunia ni mali yao na yanataka kuyaweka chini yao mataifa dhaifu duniani, leo hii yote yamepanga safu kukabiliana na Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu.

Athari na baraka za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yanaonekana pia kwenye mabadiliko adhimu na kupata nguvu matukufu ya kidini na kuyafanya yasimame kupambana na fikra za kibeberu za madola ya kiistikbari ulimwenguni. Ni kwa sababu hiyo ndio maana madola ya kibeberu yanatumia nguvu na uwezo wao wote katika nyuga tofauti ili kuhakikisha kuwa harakati hiyo inasimama au yanaidhibiti mikononi mwao. Madola hayo ya kiistikbari yameelekea zaidi njama zao dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo ni mhimili mkuu wa muqawama na mwamko wa Kiislamu duniani. Hata hivyo mwamko na kutotetereka taifa la Iran na viongozi wao kumepelekea kushindwa njama na mashambulizi yote ya maadui. Taifa la Iran limefanikiwa kubadilisha vitisho vya maadui na vikwazo vyao kuwa fursa ya kujiletea maendeleo na kujitegemea. Katika miaka yote hii ya tangu yalipopata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, harakati ya taifa la Iran inazidi kupiga hatua siku baada ya siku. Licha ya kuwekewa vikwazo vikubwa sana vya kiuchumi, kulazimishwa kupigana vita vya miaka minane vilivyokuwa na uharibifu mkubwa na kuongezwa mashinikizo dhidi yake kila siku zinavyopita, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa kufikia vilele vya juu kabisa vya ustawi na kupata mafanikio makubwa kwenye nyuga tofauti kwa kutawakali kwa Mwenyezi Mungu na kwa kutegemea watu wake, utajiri wake na kufanya jitihada zisizochoka.

Sehemu ya maendeleo ya kiteknolojia ya Iran

 

Mwaka huu pia, taifa la Iran linaingia katika maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu huku kukiwa kumeanza mabadilio mapya katika masuala ya kisiasa na kiuchumi nchini Iran. Katika kipindi cha miaka yote iliyopita, maadui walikuwa wanaiwekea Iran vikwazo vya kila namna kwa kisingizio cha miradi yake ya nyuklia. Muda wote huo Magharibi ilifanya njama za kila namna za kujaribu kuifanya Iran itengwe. Lakini taifa la Iran haikutetereka hata sekunde moja katika njia yake bali ilifanya juhudi kubwa zaidi na kwa yakini na kujiamini zaidi na kufanikiwa kupiga hatua kubwa za maendeleo. Licha ya kuweko mashinikizo na vikwazo katika mambo yake mengi, taifa la Iran limefanikiwa kuuthibitishia ulimwengu kuwa ni taifa lisiloyumba. Maendeleo ya kupigiwa mfano liliyopata taifa hili katika nyanja tofauti, yamewalazimisha hata maadui wakubwa wa taifa hili wakiri. Miongoni mwa maadui hao ni viongozi wa Marekani ambao wameshindwa kuficha ukweli huo. Katika moja ya matamshi yake, John Kerry, Waziri wa Mambo ya Nje ya serikali ya Barack Obama wa Marekani alisema:

John Kerry, Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani wa Marekani

 

Vikwazo vimeshindwa kuidhoofisha Iran na ushahidi wa hayo ni kwamba Jamhuri ya Kiislamu licha ya kuwa kwenye vikwazo lakini imezidi kusonga mbele kwenye njia yake. Iran imepasi katika mtihani wa vikwazo.

Kwa kweli ni kama alivyosema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, katika moja ya hotuba zake kwamba: Katika miaka yote hii, taifa la Iran licha ya kuweko vikwazo na mashinikizo mengi lakini imezidi kupiga hatua za maendeleo katika nyuga za elimu na maarifa na kufanikiwa kupata teknolojia mpya na kuwa na nafasi muhimu sana katika maendeleo ya kiuchumi na ustawi endelevu, na kila leo taifa la Iran linazidi kupiga hatua mbele.

 

Tags