Ijumaa, 3 Februari, 2017
Leo ni Ijumaa tarehe 5 Jamadil Awwal 1438 Hijria sawa na Februari 3, 2017.
Siku kama ya leo miaka 1433 iliyopita alizaliwa Bibi Zainab (s.a) binti mtukufu wa Imam Ali bin Abi Twalib na Bibi Fatimatu Zahraa (as). Bibi Zainab alikuwa mashuhuri miongoni mwa watu kutokana na maarifa na elimu kubwa aliyokuwa nayo. Katika tukio la Karbala, Bibi Zainab (s.a) alisimama kidete na kukabiliana na dhulma za watawala dhalimu na ujahili watu wa zama hizo ili kutimiza malengo matukufu ya kaka yake, Imam Hussein (a.s). Bibi Zainab alipelekwa Sham pamoja na mateka wengine wa Nyumba Tukufu ya Mtume (saw) baada ya mapambano ya Imam Hussein (a.s) huko Karbala. Hotuba za Bibi Zainab mbele ya majlisi ya Ibn Ziyad mtawala wa Kufa na katika ikulu ya Yazid bin Muawiya huko Sham zilikuwa na taathira kubwa katika kufichua dhulma na ukandamizaji wa Bani Umayya na kuonesha jinsi Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume walivyodhulumiwa.
Ni vyema kuashiria hapa kuwa nchini Iran siku ya kuzaliwa Bibi Zainab (a.s) husherehekewa kama 'Siku ya Wauguzi'.
Siku kama ya leo, miaka 1430 iliyopita kulijiri vita vya Mu'utah, baina ya jeshi la Waislamu na jeshi la Roma na waitifaki wake. Vita hivyo vilitokea baada ya mjumbe aliyekuwa ametumwa na Mtume (saw) njini Sham kwa ajili ya kulingania dini ya Kiislamu, kuuawa shahidi na askari wa kulinda mpaka wa eneo hilo. Baadhi ya wanahistoria wanasema kuwa, vita hivyo vilijiri kufuatia kuuawa shahidi wakufunzi 14 wa Qur'an Tukufu waliokuwa wametumwa na Mtukufu Mtume katika maeneo ya mpakani ya Sham. Kufuatia mauaji hayo, Mtume aliandaa jeshi la wapiganaji 3000 kwenda eneo hilo lililokuwa chini ya utawala wa Roma. Katika vita hivyo Mtume alimteua Jaafar bin Abi Twalib, mtoto wa ami yake, kwa ajili ya kuongoza jeshi la Kiislamu, huku akiwateua pia Zaid bin Haritha na Abdullah bin Rawwaaha kwa ajili ya kukaimu nafasi hiyo. Jeshi la Kiislamu ambalo lilikuwa limechoka kutokana na kwamba ilikuwa mara ya kwanza kwenda safari ndefu kama hiyo, lilipambana na jeshi la Roma na wapiganaji wa kikabila katika eneo la Mu'utah, magharibi mwa Jordan ya leo ambapo liliwapoteza viongozi wote watatu wa jeshi hilo la Kiislamu. Hatimaye Waislamu walimpa jukumu la kuongoza jeshi hilo Khalid Bin Walid ambaye ndiye kwanza alikuwa amesilimu, ambapo naye alitoa amri ya kuwataka Waislamu kurudi nyuma. Hata kama jeshi la Kiislamu halikushinda vita hivyo, lakini liliweza kusoma mbinu za jeshi la adui hatua ambayo ilikuwa utangulizi wa ushindi dhidi ya jeshi hilo la adui katika vita vya baadaye.
Tarehe 3 Februari miaka 549 iliyopita, alifariki dunia mvumbuzi wa mashine ya uchapishaji, Johannes Gutenberg. Mvumbuzi huyo alizaliwa nchini Ujerumani lakini alihamia Strasbourg, Ufaransa na akaanza kujishughulisha na kazi za kiufundi. Mwaka 1443 au 1444 Gutenberg alifanikiwa kutengeneza mashine ya uchapishaji na kupiga hatua muhimu katika uchapishaji na uenezaji wa elimu na maarifa kati ya wanadamu. Katika zama zake, Johannes Gutenberg pia alichapisha kitabu cha Biblia maarufu kwa jina la' Gutenberg Bible.'
Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, mfereji wa Suez uliokuwa ukidhibitiwa na Uingereza, ulishambuliwa na vikosi vya majeshi ya Ujerumani na utawala wa Othmaniya katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Udhibiti wa mfereji huo wa Suez ulikuwa na umuhimu mkubwa kwa pande mbili zilizokuwa zikipigana katika Vita vya Kwanza vya Dunia kutokana na ukweli kwamba mfereji huo ndio unaounganisha Bahari ya Mediterania na Bahari Nyekundu. Uingereza ambayo haikuwa tayari kupoteza makoloni yake ya Asia, ilipigana vikali na majeshi ya Ujerumani na utawala wa Othomaniya na kupata ushindi.Mfereji wa Suez uliendelea kudhibitiwa na Uingereza hadi ulipotaifishwa na kiongozi wa Misri Gamal Abdul Nasir hapo mwaka 1956.
Miaka 38 iliyopita katika siku kama hii ya leo, katika hali ambayo mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah yalikuwa yamefikia kileleni baada ya Imam Ruhullah Khomeini kurejea nchini akitokea uhamishoni, Waziri Mkuu wa utawala wa kifalme wa Shah, Shapur Bakhtiyar alifanya jitihada za kuwatuliza wananchi bila ya mafanikio yoyote. Bakhtiyar alifanya juhudi za kusitisha harakati za Mapinduzi kwa kujidhihirisha kuwa ni mwanademokrasia na mpigania uhuru na akasema kwamba, hatamruhusu Imam Khomeini kuunda serikali ya mpito nchini. Wakati huo uasi wa kiraia, kukimbia wanajeshi na kujiunga na safu za wananchi katika miji mbalimbali ya Iran ikiwa ni pamoja na kujiuzulu wabunge, viongozi wa ngazi za juu serikalini na kadhalika kuliifanya serikali ishindwe kudhibiti hali ya mambo nchini.
Siku kama ya leo miaka 7 iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilirusha kwa mafanikio kombora la kwanza la kupeleka satalaiti angani la Omid. Miaka iliyofuata Iran ilituma viumbe hai angani kwa mafanikio ikiwa ni pamoja na kobe na tumbili na hatua hiyo iliingiaza Iran katika klabu ya nchi zenye teknolojia ya anga za mbali tena katika kipindi hicho cha vikwazo vikali vya kiuchumi vya nchi za Magharibi.