Mafanikio ya Iran katika kutibu uvimbe wa saratani katika ubongo
Karibuni katika mjumuiko huu wa vipindi ambavyo huangazia maendeleo mapya katika sekta za sayansi, teknolojia na tiba duniani na hasa nchini Iran na baadhi ya maeneo mengine duniani. Karibuni
Wapenzi wasikilizaji leo tutaanza kwa kuangazia mafanikio ya watafiti Wairani katika kutengeneza chombo cha kupima uwezo wa macho. Mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka 2016, watafiti wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Mashhad kaskazini mashariki mwa Iran walifanikiwa kutengeneza combo cha kilelektroniki cha kupima uwezo wa jicho kuona rangi, uwezo wa jicho kuona kina kirefu na pia kubaini uharibifu katika uwezo wa jicho kuona. Kituo cha Matibabu ya Macho cha chuo hicho pia kinatibu matatizo ya macho ya wenye ugonjwa wa Dyslexia na Thalassemia.
Kituo hicho kimefanya uchunguzi kamilifu kuhusu matatizo ya uwezo wa kuona mbali au karibu macho na kufanikiwa kupata nafasi ya tatu duniani baada ya Marekani na Australia.
Chombo hicho kilichovumbuliwa na wanasayansi Wairani huweza kutibu udhaifu uliopo katika kioo cha jicho yaani retina. Huo ni udhaifu ambao hupelekea mtu kutoona vizuri taswira. Mwenye tatizo hilo huhitajia chombo cha kumsaidia kuona kama vile miwani au lenzi za jicho
Hali kadhalika katika kurekebisha tatizo hilo baadhi ya wakati badala ya kutumiwa miwani au lenzi madaktari humfanyia mgonjwa upasuaji. Aidha uwezo duni wa kuona au Amblyopia na matatizo ya kubaini rangi ni kati ya matatizo ya macho yanayowasumbua wengi. Watafiti katika kituo hicho cha Matibabu ya Macho katika Chuo Kikuu cha Mashhad wamechunguza matatizo hayo kwa kina na wamewasilisha mapendekezo kadhaa ya kuyatatua.
Kwingineko, watafiti Wairani katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Amir Kabir mjini Tehran, ambacho ni kati ya vyuo vikuu vyenye itibari zaidi Iran, wamefanikiwa kuunda programu ya kompyuta yenye uwezo wa kuchukua taswira za video zenye kuonyesha harakati za valvu za moyoni pasina kikomo. Chombo hicho kinaweza kuchukua nafasi ya mashine ijulikanayo kama Eco cardiography ambayo wataalamu wanasema ina matatizo. Moja ya matatizo ya mashine hiyo ni kuwa haiwezi kuonyesha taswira za harakati zisizo na kikimo na husimama mara kwa mara wakati wa kuchukua taswira. Hali kadhalika kutokana na kuwa mashine ya ultra sound ina kasi thabiti na hivyo uwezo wake wa kuchukua taswira nao pia una vizingiti hasa katika sehemu za moyo zenye harakati za kasi kama vile valvu za moyoni, inakuwa vigumu kuweza kubaini kwa usahihi ugonjwa.
Ni kwa kuzingatia tatizo hili ndio wanasayansi katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Amir Kabir wakawasilisha njia ya kutatua tatizo hilo kwa kuunda mashine hiyo maalumu yenye kuchukua video.
Kwingineko wanasayansi Wairani wamefanikiwa kuunda uzi wa kushona kwa kutumia teknolojia ya nano. Uzi huo una matumizi mengi na mapana sana katika sekta za viwanda vya nguo, polymer, petrokemikali, plastiki na viwanda vya magari. Uzi huo wa Iran sasa unauzwa katika nchi kama vile Uzbekistan, Tajikistan, Jamhuri ya Azerbaijan, Kyrgyzstan, Uturuki, Italia na nchi za Ghuba ya Uajemi.
Nchi za Ulaya zinatengeneza uzi kama huo lakini teknolojia iliyotumiwa ni dunia ikilinganishwa na ile ya Iran.
Wapenzi wasikilizaji kama mnavyojua ustawi wa sayansi za kisasa umewezesha wanandoa wenye utasa au ugumba kufanikiwa kupata mtoto au watoto. Mbinu kadhaa zinatumiwa kama vile upandikizaji wa mimba katika mirija ya uzazi kitaalamu inayojulikana kama, In Vitro Fertilization,(IVF), ambapo mwanamke kupewa au kununua mbegu za kiume n.k. Kuna watoto wengi duniani ambao sasa wanazaliwa kwa njia hizo. Ni kwa sababu hii ndio watafiti wa Kituo cha Utafiti cha Royan mjini Tehran wakapata umashuhuri duniani kwa mafanikio yao ya kuwasaidia wanawake tasa au wanaume wenye ugumba kupata mtoto au watoto. Kwa kuzingatia utumizi wa mbinu hizo tulizozitaja za upandikizaji mimba au mwanamke kupewa au kununua mbegu za kiume, watafiti katika Taasisi ya Royan wamefanya uchunguzi wa kina kuhusu kiwango cha mfungamano wa mama na mtoto anayezaliwa kutokana na mimba iliyopatikana kwa njia zisizo za kawaida. Matokeo ya utafiti huo yamechapishwa katika jarida la kimataifa la IJFS yaani International Journal of Fertility & Sterility.
Utafiti huo uliofanyika Iran unaonyesha kuwa watoto waliozaliwa kutokana na mimba zilizopatikana kwa njia za kitiba nao pia huwa na mafungamano ya juu na mama mzazi. Watafiti hao walitumia Vipimo vya Muller ambavyo hutumiwa duniani kubaini kiwango cha mahaba na mafungamano ya mama na mtoto.
Leo katika maeneo mbali mbali duniani kuna ongezeko la utumizi wa meli za utafiti na uchunguzi katika ziwa au baharini. Iran nayo pia haijaachwa nyuma katika hili na hivi karibuni watafiti Wairni walifanikiwa kuunda meli erevu yenye kufanya uchunguzi wa maji ya bahari. Meli hiyo ina uwezo wa kuchunguza sifa za maji, mada za kemikali zilizomo, uwezekano wa maji kutumiwa na mwanadamu n.k. katika maji. Meli hiyo iliyotegenezwa na wanasayansi Wairani inaweza kufika maeneo ya mbali katika oparesheni za utafititi.
Hivi karibuni Iran pia imezindua meli ya utafiti ijulikanayo kama MV Persian Gulf Explorer ambayo ina urefu wa mita 50, upana wa mita 10 na urefu wa kutoka chini kwenda juu wa mita 12.
Meli hiyo iliyotengenezwa na watafiti Wairani ndani ya nchi hii itakuwa na jukumu la kufanya utafiti kuhusu masuala mbali mbali ya kibahari katika Ghuba ya Uajemi, Bahari ya Oman na Kaskazini mwa Bahari ya Hindi.
Na mwisho katika makala yetu ya leo tutaangazia mafanikio mengine ya wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Mashhad nchini Iran ambao Novemba mwaka jana walifanikiwa kuunda chombo cha kutibu vimbe za saratani katika maeneo mbali mbali mwilini. Chombo hiki kinaweza kutibu vimbe ndogo ndogo za saratani mwilini hasa katika ubongo ambao kinyume na maeneo mengine mwilini vimbe zilizo hapo haziwezi kutibiwa kwa mbinu ya radiolojia na joto.
Kwa kuzingatia kuwa kuna uwezekano mkubwa kuwa uvimbe wa saratani katika ubongo huwa sehemu nyeti sana na kuugusa yamkini kukasababisha hata mauti kwa mgonjwa, kunahitajika chombo maalumu cha kufanya kazi hiyo kupitia miale maalumu ya kuangamiza uvimbe huo. Hicho ndicho chombo ambacho wanasayansi hao wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Mashhad wameunda ili kuondoa uvimbe wa saratani katika ubongo kwa kutumia miale maalumu.
Wapenzi wasikilizaji, makala yetu inafikia tamati hapa kwa leo, usikose kujiunga nasi wiki jayo tukuletee mapya zaidi katika uga wa sayansi, teknolojia na tiba.