Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (149)
Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran.
Kipindi cha leo bado kinajadili suala ambalo tumekuwa tukilizungumzia katika vipindi vitano vilivyopita kuhusiana na majukumu waliyonayo Waislamu kwa Maimamu wa Ahlul Beit ya Mtume Mtukufu (saw). Katika vipindi hivyo tulipata kujua majukumu matano kati ya majukumu hayo ambayo ni: Wajibu wa utiifu kwao na kufuata njia na mienendo yao ya maisha zikiwemo Suna za Mtume (saw). Kisha kuna wajibu wa kuhukumiwa na kurejea kwao ili kujua hukumu sahihi ya Mwenyezi Mungu na Kitabu chake kitakatifu katika matukio yanayoibuka na kuhusu kila hitilafu. Wajibu wa tatu ni kuwaswalia kama sehemu ya kumswalia Mtume Mtukufu (saw). Wajibu wa nne ni kuwapenda na kuwatangulizia mahaba ambayo yanaandamana na mahaba kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake Mtukufu. Hatimaye wajibu wa tano ni kuwatukufuza kutokana na nafasi muhimu na adhimu waliyonayo mbele ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake kutokana na kujitolewa kwao kwa ajili ya kulinda na kutetea dini na haki kama minara ya kuwaongoza wanadamu. Baada ya kujua majukumu hayo matano, tunajiuliza kwamba je, wajibu au haki ya sita ya Maimamu wa Ahlul Beit wa Mtume (as) ni ipi? Hiii ndiyo haki tutakayoijadili katika kipindi hiki cha sita kuhusiana na haki za watukufu hao, hivyo basi endeleeni kuwa nasi hadi mwisho wa kipindi ili mpate kunufaika na yale tuliyokuadalieni katika kipindi hiki, karibuni.

Ndugu wasikilizaji, tunaporejea riwaya tunapata kwamba kuna hadithi nyingi mno zilizopokelewa na pande zote mbili ambazo zinathibitisha kwamba Mtume Mtukufu (saw) alifikisha ujumbe alioteremshiwa na Mwenyezi Mungu kuhusiana na wilaya na uongozi wa wasii wake al-Murtadha Abu al-Hassan Amir al-Mu’mineen Ali (as). Katika kutekeleza amri hiyo ya Mwenyezi Mungu, Swadiq al-Amin (saw) aliwaita Waislamu na kuwataka wambai khalifa wake ambaye ni Amir al-Mu’mineen (as). Alichukua beia ya Waislamu waliojumuika naye katika eneo la Ghadir Khum kwa ajili ya wasii wake al-Imam Ali al-Murtadha (as) ambapo aliamuru hema litundikwe hapo kwa ajili ya kupongezwa na kubaiiwa Imam Ali, na hatimaye Waislamu kufika hapo kwa ajili ya kumpongeza na kutangaza baia yao kwake. Kwa msingi huo tunafahamu vyema wapenzi wasikilizaji kwamba moja ya majukumu ya Waislamu kwa makhalifa na Maimamu wa Mtume Mtukufu (saw) ni wajibu wa kuwapa baia ambayo ni sawa na kutangaza baia kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw).
Tunaona kwamba maulamaa wamethibitisha katika utafiti na maandishi yao ya vitabu muhimu kama vile al-Ghadir na hadithi nyingi ambazo zimethibitishwa usahihi wake na madhehebu yote mawili ya Kiislamu kwamba Mtume (saw) aliwafahamisha Waislamu hadithi ya Thaqalain katika hotuba aliyoitoa katika siku hiyohiyo ya Ghadir Khum na kusisitiza juu ya kutotengana kizazi chake na Qur’ani Tukufu na vilevile kuwafahamisha uimamu wa makhalifa wake kumi na wawili katika kizazi chake. Kwa maelezo hayo tunatambua pia kwamba wajibu wa baia hauishii kwa Imam Ali (as) bali unawajumuisha Maimamu wote kumi na wawili katika makhalifa wa Mtume ambao Mtume mwenyewe (saw) aliubashiria Umma wake katika hotuba ya Ghadir na hotuba zake nyinginezo.

Wapenzi wasikilizaji, msisahau kwamba baia ni kufunga agano la kisheria ambalo linawajibisha utiifu, kunusuru na kuafuata. Kwa msingi huo kusimamisha mapambano kwa ajili ya kutekeleza wajibu huo kuhusiana na Maimamu kumi na wawili wa kizazi cha Mtume Muhammad (saw) ni kuwatii, kuwafuata na kuwanusuru kama ambavyo inatuwajibikia kumnusuru Mtume (saw), wajibu ambao unatekelezwa wakati wa uhai na vilevile baada ya kuuawa kwao shahidi humu duniani. Utekelezwaji wa wajibu huu katika kipindi cha uhai wao ni suala lililo wazi kwa maana kwamba wanapaswa kutiiwa, kunusuriwa na kufuatwa katika kila wanalotuamrisha. Ama baada ya kuuawa shaihidi na kufariki kwao dunia, utiifu na ufuataji huu hutimia kwa kutekeleza kivitendo maamrisho na makatazo yao pamoja na kuwanusuru kwa kutetea njia yao na kuondoa shub’ha.
Mbali na hayo tonaona kwamba kuna hadithi ambazo zinasisitiza juu ya kubaiiwa Imam aliye hai ambaye maarifa kuhusiana naye na kisha kumfua humuokoa mwanadamu kutokana na mauti ya ujahili. Na maana hii imepoekelewa kwa njia tofauti katika hadithi za pande mbili. Katika upande wa Ahlu Suna kuna hadithi nyingi mno ambazo zinasema kuwa Mtume Mtukufu (saw) alisema: ‘Mtu anayeondoa mkono wake kwenye utiifu wa Imam, atakuja Siku ya Kiama hali ya kuwa hana hoja mbele ya Mwenyezi Mungu na anayekufa hali ya kuwa hana baia kwenye shingo lake, huwa amekufa kifo cha ujahili.’ Ni wazi kuwa Mwenyezi Mungu ni muadilifu zaidi na wala hawezi kujaalia mauti ya ujahili kwa mtu ambaye hakuwafuata maimamu wa batili na upotovu. Hivyo basi makusudio ya hadithi hii ni baia ya Imam wa haki ambaye amepewa cheo hicho na Mwenyezi Mungu Mtukufu. Ni Imam huyu ambaye kumbai, kumfuata na kumnusuru ndio njia ya uongofu na kuepuka kufa kifo cha ujahili. Tafsiri nyingine yoyote ya hadithi hii isiyokuwa hii bila shaka itatuelekeza kwenye fikra za maimamu wa upotovu ambao wanahalalisha utawala wa madikteta na madhalimu na kuwalazimisha watu kuwatii na kutekeleza amri zao za kidhulma. Maimamu hao wa upotovu ndio wanaojaribu kupotosha maana halisi ya hadithi kama hizi za Mtume na kubuni nyingine bandia ambazo zinahalalisha ufuataji wa amri za watawala dhalimu na wasiofaa, ambao hatimaye hudhibiti na kuukandamiza Umma wa Kiislamu.

Wapenzi wasikilizaji, ama hadithi za Ahlul Beit (as) zinazozungumzia suala hili ni nyingi sana ikiwemo ile iliyonukuliwa na Sheikh al-Hamiri (MA) katika kitabu chake cha Qurb al-Isnad kutoka kwa Imam Baqir (as) akimnukuu Mtume (saw) kwamba alisema katika hadithi ndefu kuhusiana na Ahlul Beit (as): ‘Mtu anayeaga dunia bila ya kuwa na Imam hai anayemjua huwa ameaga mauti ya ujahili…… Hoja ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa viumbe wake haitimii ila kupitia Imam aliye hai wanayemjua.’
Naye al-Imam al-Hassan al-Askari (as) amesema kuhusu mwanaye al-Mahdi (AF) kama ilivyonukuliwa na Sheikh as-Swaduq katika kitabu chake cha Kamal ad-Deen: ‘Yeye ndiye Imam na Hoja baada yangu. Mtu anayekufa bila ya kumjua huwa amekufa kifo cha ujahili.’
Na Imam Swadiq (as) amesema kupitia hadithi iliyonukuliwa katika kitabu cha al-Mahasin alipoulizwa kuhusiana na kauli ya Mtume (saw) inayosema, ‘mtu anayekufa bila ya kuwa na Imam huwa amekufa kifo cha ujahili’: ‘Nam, lau kama watu wangelimfuata Ali bin Hussein (as) na kumuacha Abdul Malik bin Mar’wan wangeongoka.’
Tunakamilisha kipindi cha juma hili katika mfululizo wa vipindi vya Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain wepenzi wasikilizaji kwa kusoma kipande hiki cha dua tukufu ya al-Ahad ambayo Imam Swadiq (as) alitutaka tuisome katika kipindi cha ghaiba ya Imam wa Mwisho al-Mahdi Muahidiwa (AF). Kufanya hivyo kwa hakika ni katika mifano ya wazi ya kutangaza baia yetu kwa Imam Mwokozi wa ulimwengu na hivyo kuepuka kifo cha ujahili.
Allahumma! Ninamtangazia upya agano, mkataba na baia kwenye shingo langu katika asubuhi ya siku yangu hii na katika siku nitakazoishi katika maisha yangu, sitageuka wala kubadilika kamwe. Allahumma! Nijaalie kuwa miongoni mwa wanaomnusuru na wasaidizi wake, na ambao humtetea na kuharakisha kukidhi haja zake, wanaotekeleza amri na makatazo yake, wanaofuata irada yake na kumtetea na wanaouawa shahidi kwenye njia yake, kwa baraka zako ewe Mbora wa warehemevu!