Maswali yetu a Majibu ya Thaqalain (154)
Assakaam Aleikum wapenzi wa sikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayoikutangazieni kutoka mjini Tehran. Hii ni sehemu ya 154 katika mfululizo wa vipindi vya Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambavyo huchambua, kuchunguza na kujibu maswali mbalimbali yanayohusiana na itikadi ya Kiislamu.
Wapenzi wasikilizaji katika vipindi kumi vilivyopita tumekuwa tukichunguza majukumu na wajibu tulionao sisi Waislamu kwa Maimamu wa Nyumba Tukufu ya Mtume Muhammad (saw) ambapo kupitia maandiko matakatifu tumepata kujua majukumu au haki kumi tunazowajibika kuzitekelezwa kwa Maimamu hao watoharifu. Haki hizo tisa ni: Haki ya kuwatii, kuwarejea wakati hitilafu na ugomvi unapotokea miongoni mwetu ili wapate kutusuluhisha, haki ya kuwaswalia pamoja na Bwana wao Muhammad al-Mustafa (saw), haki ya kuwapenda, kuwakirimu na kuwaenzi, kuwabai, kuwazuru, kuwapa khumsi pamoja na kuwapa haki zote za ubaba wa kimaanawi. Baada ya kuzijua haki hizo tunajiuliza kwamba je, haki yao ya kumi ni ipi? Hii ndiyo haki tutakayoizungumzia katika kipindi hiki, hivyo kuweni pamoja nasi hadi mwisho wa kipindi, karibuni.
Wapenzi wasikilizaji, tunaporejea maandiko matakatifu tunapata kwamba yanasema waziwazi kuwa kufanya juhudi za kupata radhi za Ahlul Beit wa Mtume Mtukufu (as) ni miongoni mwa wajibu na majukumu ya Umma wa Kiislamu kwa watukufu hao kwa sababu radhi yao ni radhi ya Mwenyezi Mungu pamoja na Mtume wake (saw). Na katika upande wa pili tunapasa kuepuka kuwaudhi kwa sababu kuwaudhi ni kumuudhi Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw). Mwenyezi Mungu anasema hivi katika aya za 61 na 62 za Surat at-Tauba:
وَمِنْهُمُ الَّذِينَ يُؤْذُونَ النَّبِيَّ وَيَقُولُونَ هُوَ أُذُنٌ قُلْ أُذُنُ خَيْرٍ لَّكُمْ يُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَيُؤْمِنُ لِلْمُؤْمِنِينَ وَرَحْمَةٌ لِّلَّذِينَ آمَنُواْ مِنكُمْ وَالَّذِينَ يُؤْذُونَ رَسُولَ اللَّهِ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ. يَحْلِفُونَ بِاللَّهِ لَكُمْ لِيُرْضُوكُمْ وَاللَّهُ وَرَسُولُهُ أَحَقُّ أَن يُرْضُوهُ إِن كَانُواْ مُؤْمِنِينَ.
Na miongoni mwao wapo wanaomuudhi Nabii na kusema: Yeye huyu ni sikio tu. Sema: Basi ni sikio la kheri kwenu. Anamwamini Mwenyezi Mungu, na ana imani na Waumini, naye ni rehema kwa wanaoamini miongoni mwenu. Na wale wanaomuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu watapata adhabu iumizayo. Wanakuapieni Mwenyezi Mungu ili kukuridhisheni nyinyi, hali ya kuwa wanao stahiki zaidi kuridhishwa ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake, lau kama wao ni Waumini.
Kuna aya nyingi sana zinazowakataza Waislamu kumuudhi Mtume (saw) na hakuna shaka kwamba kuudhi kizazi na Watu wa Nyumba yake ni mifano ya wazi zaidi ya kumuudhi Mtume (saw). Isitoshe familia na watu hao wa Nyumba ya Mtume (as) ni mfano wa wazi zaidi wa watu wanaotajwa kuwa ni waumini ambao Mwenyezi Mungu amesema wasiudhiwe kwa njia yoyote ile. Baada ya Mwenyezi Mungu kuamuru Mtume wake Mtukufu (saw) aswaliwe katika Surat a-Ahzab anasema katika aya za 57 na 58 za sura hiyo:
إِنَّ الَّذِينَ يُؤْذُونَ اللَّهَ وَرَسُولَهُ لَعَنَهُمُ اللَّهُ فِي الدُّنْيَا وَالآخِرَةِ وَأَعَدَّ لَهُمْ عَذَابًا مُّهِينًا. وَالَّذِينَ يُؤْذُونَ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ بِغَيْرِ مَا اكْتَسَبُوا فَقَدِ احْتَمَلُوا بُهْتَانًا وَإِثْمًا مُّبِينًا.
Hakika wale wanaomuudhi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Mwenyezi Mungu amewalaani duniani na Akhera, na amewaandalia adhabu ya kufedhehesha. Na wale wanaowaudhi waumini wanaume na wanawake pasina wao kufanya kosa lolote, bila shaka wamebeba dhulma kubwa na dhambi zilio dhahiri.
Na Madhehebu zote mbili za Kiislamu yaani Shia na Sunni zimepokea hadithi nyingi ambazo zinasema kuwa Mwenyezi Mungu alijaalia radhi zake na za Mtume wake (saw) kwenye radhi za watu watoharifu katika kizazi chake (as). Kama ambavyo alijaalia kuudhiwa kwao (as) kuwa ni kumuudhi Yeye MwenyezI Mungu pamoja na Mtume wake (saw), jambo ambalo linasababisha adhabu kali kwa wahalifu. Tutanufaika na baadhi ya hadithi hizo hivi pundu, hivyo endeleeni kuwa pamoja nasi.
AL-Hakim amenukuu katika kitabu chake cha al-Mustadrak kuhusiana na vitabu viwili vya Sahih Bukhari na Muslim hadithi iliyopokelewa na Abu Malika akisema: ‘Mtu mmoja kutoka Sham alifika na kumtukana Ali mbele ya Ibn Abbas, naye - yaani Ibn Abbas -akamkataza kufanya hivyo na kusema: Ewe adui wa Mwenyezi Mungu! Umemuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu (Hakika wale wanaomuudhi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Mwenyezi Mungu amewalaani duniani na Akhera, na amewaandalia adhabu ya kufedhehesha.) Kama Mtume wa Mwenyezi Mungu angekuwa hai ungekuwa umemuudhi.
Al-Hakim anafafanua hadithi hii kwa kusema kuwa ni sahihi kimapokezi kwa masharti ya Bukhari na Muslim na pia kwamba imethibitishwa na adh-Dhahbi.
Vilevile madhebu zote mbili za Kiislamu zimepokea hadithi nyingine ambapo Mtume Mtukufu (saw) anasema wazi kwamba kumuudhi Mrithi wake yaani Imam Ali (as) ni kumuudhi Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw). Anasema: ‘Mtu anayemuudhi Ali huwa ameniudhi na anayeniudhi huwa amemuudhi Mwenyezi Mungu na anayemuudhi Mwenyezi Mungu anahofiwa kulipizwa kisasi na Mwenyezi Mungu.’ Na madhehebu mbili hizo pia zimenukuu kauli ya Mtume Muhammad al-Mustafa (saw) iliyonukuliwa na al-Muhaqiq al-Kurki katika kitabu chake cha Rasail, alipomwambia wasii wake Ali al-Mrtadha (as) kwamba: ‘Ewe Ali! Mtu anayeudhi unywele wako huwa ameniudhi na anayeniudhi huwa amemuudhi Mwenyezi Mungu.’
Hadithi nyingine iliyonukuliwa kwa njia sahihi na madhehebu zote mbili kutoka kwa Mtume (saw) inasema: ‘Mwenyezi Mungu anaridhia kwa ridhaa ya Fatuma na kughadhabika kwa ghadhabu yake.’
Kadhalika kuna hadithi hii kutoka kwa Mtume (saw) ambayo imenukuliwa katika kitabu cha Bukhari na vitabu vinginevyo inayosema: ‘Fatuma ni sehemu ya mwili wangu. Hivyo anayemughadhabisha huwa amenighadhabisha mimi.’ Na riwaya nyingine inasema: ‘Mtu anayemuudhi huwa ameniudhi mimi na anayeniudhi mimi huwa amemuudhi Mwenyezi Mungu.’
Naye Imam Hussein (as) amepokelewa akisema: ‘Ridhaa ya Mwenyezi Mungu ni ridhaa yetu sisi Ahlul Beit.’
Na madhumuni ya hadithi hii imenukuliwa katika hadithi nyingi zilizopokelewa kwa njia ya Ahlul Beit (as) ambapo tunatoa muhtasari wa madhumuni ya hadithi hizo kwa kusema: Miongoni mwa haki zilizosisitiziwa Umma wa Kiislamu kuhusiana na Ahlul Beit wa Mtume Muhammad (saw) ni kufanya juhudi za kupata ridhaa na radhi za watukufu hao kwa sababu kufanya hivyo kunaandamana na kupata radhi za Mwenye Mungu Mtukufu na hivyo kupata mafanikio makubwa katika maisha ya humu duniani na ya huko Akhera. Umma wa Kiislamu pia unapasa kuepuka kuwaudhi watukufu hao wa Nyumba ya Mtume (saw) kwa sababu kufanya hivyo pia kunaandamana na kumuudhi Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw) ambapo jambo hilo husababisha adhabu kali na laana ya Mwenyezi Mungu humu duniani na huko Akhera.
Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain kwa juma hili. Kipindi hiki kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikikutangazieni kutoka hapa mjini Tehran. Basi hadi tutakapojaliwa kukutana tena Juma lijalo, la ziada hatuna isipokuwa kukuageni kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.