Apr 10, 2017 11:54 UTC

Sura ya Luqman, aya ya 25-28 (Darsa ya 736)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 736 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 31 ya Luqman. Tunaianza darsa yetu kwa aya 25 na 26 ambazo zinasema:

وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ لَيَقُولُنَّ اللَّهُ قُلِ الْحَمْدُ لِلَّهِ بَلْ أَكْثَرُهُمْ لا يَعْلَمُونَ

Na ukiwauliza: Ni nani aliye ziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka watasema: Ni Mwenyezi Mungu. Wewe sema: Alhamdulillahi! Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu. Lakini wengi wao hawajui.

لِلَّهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ إِنَّ اللَّهَ هُوَ الْغَنِيُّ الْحَمِيدُ

Ni vya Mwenyezi Mungu vyote vilivyomo mbinguni na ardhini. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mkwasi, Mwenye kusifiwa.

Aya hizi zinaashiria moja ya mambo ya wazi kabisa yanayokubaliwa na watu wote wakiwemo washirikina wanaoabudu masanamu na kueleza kwamba, kama utawauliza wao, ni nani aliyeumba ulimwengu watakujibu bila ya kusitasita wala kutafakari na kusema, ni Mwenyezi Mungu! Na sababu yake ni kwamba wanaadamu wote wanaelewa kifitra na kimaumbile kuwa hawakujiumba wao wenyewe seuze kuumba ulimwengu viumbe na vyote vilivyowazunguka. Kwa hivyo hata washirikina wanaoabudu masanamu, nao pia wanakiri kuwa masanamu hayo siyo yaliyowaumba wao wala ulimwengu bali wanayaitakidi kuwa washirika wa Mwenyezi Mungu katika uendeshaji tu wa masuala ya ulimwengu wenyewe.

Kutokana na kuungama kwao washirikina, aya hizi zinaendelea kueleza kwamba ikiwa Mwenyezi Mungu ndiye muumba wa ulimwengu, basi ndiye Mola na mmiliki wa viumbe vilivyomo ndani yake na  mtawala pia wa kila kitu; na kwa mantiki hiyo ndiye anayepasa kuhimidiwa na kushukuriwa na ni Yeye tu wa kuombwa na kuabudiwa si watu au vitu vyengine vyovyote vile.

Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba washirikina hawakuwa wakiukana uumbaji wa Mwenyezi Mungu bali chanzo cha upotofu wao kilikuwa kuyaabudu masanamu na kuomba shufaa kupitia masanamu hayo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa ujuzi wa kumtambua Mwenyezi Mungu ni jambo la fitra na maumbile na ndio maana washirikina pia wanaukubali uumbaji wa Mwenyezi Mungu, na kwamba Yeye ndiye Muumba wao na wa kila kitu. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba upotofu mwingi chanzo chake ni ujinga na ujahili. Harakati na mapambano ya Mitume na mawalii wa Allah ilikuwa ni kwa ajili ya kuwaelewesha na kuwaelimisha watu na kuwaepusha na dhalala na  upotofu.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 27 ya sura yetu ya Luqman ambayo inasema:

وَلَوْ أَنَّمَا فِي الأَرْضِ مِن شَجَرَةٍ أَقْلامٌ وَالْبَحْرُ يَمُدُّهُ مِن بَعْدِهِ سَبْعَةُ أَبْحُرٍ مَّا نَفِدَتْ كَلِمَاتُ اللَّهِ إِنَّ اللَّهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

Na lau miti yote iliyomo ardhini ikawa ni kalamu, na bahari (ikawa wino), na ikaongezewa juu yake bahari nyengine saba, maneno ya Mwenyezi Mungu yasingemalizika. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye uwezo, Mwenye hikima. 

Aya hii inaashiria adhama ya ulimwengu wa maumbile na viumbe vilivyomo ndani yake na kueleza kwamba elimu ya mwanadamu kuhusu ulimwengu wa maumbile ni ndogo na haba  mno, kwa sababu lau kama maji ya bahari zote yatafanywa wino, na miti yote ikatumika kama kalamu haitowezekana kuihesabu idadi ya vilivyoumbwa na  Mwenyezi Mungu. Katika ulimwengu wa kibinaadamu maneno hutumika kubainisha matilaba yaliyokusudiwa, lakini madhumuni ya maneno ya Allah yaliyokusudiwa katika aya hii ni aina na anuai za viumbe vya ulimwengu huu ambavyo vyote hivyo vinadhihirisha elimu, nguvu na uwezo usio na kikomo wa Muumba wake. Kwa kawaida wataalamu na wasomi wanapotaka kuandika mambo hutumia kalamu na karatasi ili kubainisha elimu na wayajuwayo. Lakini elimu ya Mwenyezi Mungu SW haina kikomo na mpaka, kiasi kwamba hata kama miti yote ingelikuwa ni kalamu na bahari ikawa wino bado havitokuwa na uwezo wa kuandika na kubainisha elimu ya Mwenyezi Mungu katika kitabu cha ulimwengu wa maumbile. Vyote hivyo si waweza wa kuhesabu vilivyoumbwa na Mwenyezi Mungu, rehma zake zisizo hesabika na neema zake Mola zisizo na kikomo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba ulimwengu wa maumbile ni kitu chenye adhama kubwa, zaidi ya vile ambavyo mwanadamu ameweza kugundua hadi sasa. Tusiuangalie ulimwengu kwa jicho na uono wetu finyu mno tulionao, kwa sababu kwa kufanya hivyo tutaishia kuwa na utambuzi na ufahamu wa kijuujuu tu wa ulimwengu huo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, vitu vyote vya ulimwengu wa maumbile vinashuhudisha juu ya kuwepo Muumba mmoja tu wa ulimwengu, kwa hivyo tujihadhari tusije tukaiendea miungu bandia, hewa na ya kubuni. Kwani elimu, izza na hekima ni vya Mwenyezi Mungu, Muumba pekee wa ulimwengu.

Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya 28 ambayo inasema:

مَّا خَلْقُكُمْ وَلا بَعْثُكُمْ إِلاَّ كَنَفْسٍ وَاحِدَةٍ إِنَّ اللَّهَ سَمِيعٌ بَصِيرٌ

Hakukuwa kuumbwa kwenu, wala kufufuliwa kwenu ila ni kama nafsi moja tu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kuona.

Baada ya aya iliyotangulia kuzungumzia adhama ya ulimwengu wa maumbile na uumbaji wa Mwenyezi Mungu aya hii ya 28 inazungumzia nguvu na uwezo usio na kikomo wa Allah SW na kueleza kwamba, katika uwezo wake Yeye Allah kuumba mwanadamu mmoja na kuwaumba wanadamu wote wa zama zote za historia ni kitu kimoja tu; na ni kitu kisicholeta maana yoyote kuzungumzia ugumu na wepesi au wingi na uchache kuhusiana na uwezo usio na kikomo wa Yeye Mola Muweza wa kila kitu. Si uumbaji wa wanaadamu tu katika dunia hii bali hata kuwafufua wao Siku ya Kiyama pia ni jambo jepesi na rahisi kwa Mwenyezi Mungu muweza wa kila kitu. Ni jambo jepesi kwa Yeye Allah kuwafufua Siku ya Kiyama wanadamu wote kwa pamoja kuanzia wa mwanzo hadi wa mwisho wao. Kwa mtazamo wa elimu, nguvu na uwezo wetu sisi wanadamu wenye mpaka na kikomo, wingi wa kitu husababisha mushkeli katika ufanyaji wake. Lakini kwa Mwenyezi Mungu hakuna tofauti baina ya uchache na wingi, bali kila kitu kwake Yeye ni rahisi na sahali kabisa. Kisha aya inaendelea kueleza kwamba Yeye Allah sio tu ni mweza wa kuwaumba tena wanadamu, lakini kwa kuwa ni mwenye kusikia na mwenye kuona ana elimu na uelewa wa yote yanayofanywa na waja wake, na atawalipa thawabu au adhabu kutokana na amali na matendo yao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba mahala na zama, na kiwango na idadi ni vitu vyenye maana maalumu kwa wanadamu. Lakini katika elimu na uwezo wa Mwenyezi Mungu idadi ya viumbe fulani pamoja na mahala na zama zao havina taathira yoyote kwa utendaji wake Yeye Mola. Kwa kutoa mfano, kuumba mwanadamu mmoja na kuwaumba wanadamu bilioni moja hakuna tofauti yoyote kwa Allah bali yote mawili ni rahisi na mepesi kwake Yeye Mola. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kama tutaelewa kwamba yote tunayoyasema anayasikia Yeye Allah na yote tunayoyatenda anayaona, tutakuwa makini zaidi katika mwenendo wetu na tutaweza kujichunga na kujiepusha na upotofu. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 736 ya Qurani imefikia tamati. Tunamuomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atupe uwezo wa kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Tags