Apr 10, 2017 12:01 UTC

Sura ya Luqman, aya ya 29-34 (Darsa ya 737)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 737 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 31 ya Luqman. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 29 na 30 ambazo zinasema:

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّهَ يُولِجُ اللَّيْلَ فِي النَّهَارِ وَيُولِجُ النَّهَارَ فِي اللَّيْلِ وَسَخَّرَ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ كُلٌّ يَجْرِي إِلَى أَجَلٍ مُّسَمًّى وَأَنَّ اللَّهَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ

Je huoni kwamba Mwenyezi Mungu huuingiza usiku katika mchana, na huuingiza mchana katika usiku, na amelitiisha jua na mwezi? Vyote hivyo vinakwenda mpaka wakati ulio wekwa. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yafanya.

ذَلِكَ بِأَنَّ اللَّهَ هُوَ الْحَقُّ وَأَنَّ مَا يَدْعُونَ مِن دُونِهِ الْبَاطِلُ وَأَنَّ اللَّهَ هُوَ الْعَلِيُّ الْكَبِيرُ

Hayo ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye wa kweli, na kwamba wanacho kiomba badala yake ni batili, na hakika Mwenyezi Mungu ndiye Aliye juu na ndiye Mkubwa.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia jinsi elimu na uwezo wa Allah SW ulivyouenea ulimwengu wote wa maumbile ikiwa ni moja ya hoja ya kuthibitisha nguvu na uwezo wake usio na kikomo wa kuweza kuwaumba na kuwafufua tena wanadamu Siku ya Kiyama. Aya hizi tulizosoma nazo pia zinaashiria mifano mingine ya uwezo huo wa Mola na kumhutubu Bwana Mtume Muhammad SAW pamoja na Waislamu kwa kuwaambia: Kufupika na kurefuka usiku na mchana katika kipindi chote cha mwaka kunakoambatana na kujitokeza misimu minne ya machipuo, joto, mapukutiko na baridi ni ishara ya kutiishwa sayari ya dunia na kuwa chini ya tadbiri ya Mwenyezi Mungu, Muweza wa kila kitu. Ukweli ni kwamba ni kwa tadbiri yake Yeye Mola mabadiliko hayo yanatokea kutwa na kucha ya siku na yanaweza kuthibitika pia kwa mahesabu ya kisayansi. Kisha aya zinaendelea kueleza kuwa si ardhi pekee inayotiishwa na Mwenyezi Mungu bali jua na mwezi, ambavyo vina taathira kubwa kwa uhai wa ardhi na viumbe wa ardhini, navyo pia vimeratibiwa kwa namna ambayo vitawezesha kupatikana mazingira mwafaka yanayohitajika kwa ajili ya maisha ya viumbe ardhini, ikiwemo mimea, wanyama na watu.

Sababu ya utiishwaji huo ni kwamba hali na mazingira hayo hayatodumu daima dawamu bali ni hadi pale tu atakapotaka Yeye Mola, na siku atakapoamuru kisimame Kiyama mfumo wote uliopo wa ulimwengu utasambaratika na kutoweka. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba mojawapo ya njia za kumjua Mwenyezi Mungu ni kutalii na kuchunguza ulimwengu wa maumbile na siri zilizomo ndani yake; njia ambayo inatiliwa mkazo na Quráni. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa mfumo wa ulimwengu na mwendo wa maumbo ya angani ni vitu vilivyowekewa mpangilio maalumu wa wakati. Ulimwengu uliopo una tamati na mwisho wake ambao unajulikana katika elimu ya Mwenyezi Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi kwamba Allah SW ni hakika thabiti na ya kudumu. Asili ya ulimwengu na kila kitu inatokana na Yeye; na ghairi yake Yeye Mola, kingine chochote kile hakidumu bali kina mwisho na kitatoweka.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 31 na 32 ya ambazo zinasema:

أَلَمْ تَرَ أَنَّ الْفُلْكَ تَجْرِي فِي الْبَحْرِ بِنِعْمَتِ اللَّهِ لِيُرِيَكُم مِّنْ آيَاتِهِ إِنَّ فِي ذَلِكَ لَآيَاتٍ لِّكُلِّ صَبَّارٍ شَكُورٍ

Je huoni kwamba marikebu hupita baharini kwa neema za Mwenyezi Mungu, ili kukuonyesheni baadhi ya Ishara zake? Hakika katika haya kuna Ishara kwa kila mwenye subira nyingi, mwenye shukurani.

وَإِذَا غَشِيَهُم مَّوْجٌ كَالظُّلَلِ دَعَوُا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ فَلَمَّا نَجَّاهُمْ إِلَى الْبَرِّ فَمِنْهُم مُّقْتَصِدٌ وَمَا يَجْحَدُ بِآيَاتِنَا إِلاَّ كُلُّ خَتَّارٍ كَفُورٍ

Na wimbi linapo wafunika kama wingu litowalo kivuli, humwomba Mwenyezi Mungu kwa kumsafia dini. Lakini anapo waokoa wakafika nchi kavu, wapo baadhi yao huenda mwendo wa sawa. Wala hazikanushi Ishara zetu ila aliye khaini kafiri mkubwa.

Aya hizi zinaendelea na maudhui ya aya zilizotangulia kwa kuashiria alama na ishara nyengine mbili za Allah katika ulimwengu na kiumbe mwanadamu na kueleza kwamba safari za meli na majahazi baharini na usafirishaji wa mizigo na abiria kupitia njia hiyo ni miongoni mwa madhihirisho ya nguvu na uwezo wa Mwenyezi Mungu. Katika dunia ya leo licha ya kuwepo anuai za vyombo vya usafiri kama gari, treni na ndege, bidhaa nyingi zaidi zinasafirishwa kupitia baharini. Kwa sababu njia nyingi za majini na baharini zinatumiwa na wanadamu bila ya kuzitolea gharama wala malipo yoyote. Bahari, ambayo ndiyo njia kuu ya mawasiliano ya kuunganisha nukta mbalimbali za ardhi inawezesha kuunganika pamoja maeneo ya karibu na ya mbali ya dunia. Bahari ni mithili ya zulia laini lililojitandika chini ya miguu ya mwanadamu ili kuwa ya mbele katika utoaji huduma na kuzipita anga na nchi kavu katika kumtumikia kiumbe huyo. Baada ya kutaja neema ya bahari, Quráni inaashiria moja ya matukio yanayojiri baharini na ambalo ni mojawapo ya alama ya ujuzi wa kifitra na kimaumbile wa kumtambua Mwenyezi Mungu na kueleza kwamba, wakati inapotokea tufani baharini na merikebu ikakumbwa na mawimbi makubwa yanayoitia msukosuko wa kuisukuma kila upande, walioabiri ndani ya merikebu hiyo hujihisi kuwa mauti na maangamizi yako mbele ya macho yao. Katika hali hiyo, abiria waliomo melini au jahazini hukata tamaa ya kupata mtu wa kuwaokoa, lakini bila ya kufikiria, ghafla huhisi kuwepo kwa nguvu fulani inayoweza kuwavusha na kuwaokoa na hali hiyo ya kutisha. Na hapo ndipo humuelekea na kumwomba Mwenyezi Mungu kwa ikhlasi, wakitaradhia na kuomba msaada kwake Yeye tu. Pamoja na hayo wanadamu wasio na shukurani, mara tu hatari ya msukosuko uliowapata inapoondoka, wakanusurika kifo na kufika nchi kavu salama usalimini humsahau yule waliyemwomba na akawaokoa, bali si hasha hata wakamkufuru na kumkanusha. Hata hivyo kuna watu wengi pia ambao wanapofikwa na hali kama hiyo wanamtambua Mola wao; na baada ya kuivuka hatari iliyowakabili huendelea kufuata njia ya Mwenyezi Mungu, na imani zao kuendelea kuwa imara na thabiti. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba tusiuangalie uumbaji wa Allah kijuujuu tu na kama kitu cha kawaida. Bahari na vitu vingine vya maumbile vyenye mfungamano nayo, vyote hivyo ni alama za Mwenyezi Mungu na njia za utambuzi wa kumjua Yeye Mola. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kwa fitra na maumbile yake, mwanadamu ana hisia za kumjua Mwenyezi Mungu, lakini sababu na vitu vya kimaada huwa mithili ya pazia linaloziba na kufunika uono wa hisia hizo. Pamoja na hayo, kujiri kwa matukio na misukosuko inayomfanya mtu akate tamaa ya kusadiwa na nguvu za kimaada, huliondoa na kuliweka kando pazia hilo na kumfanya mwanadamu amuelekee Allah kwa ikhlasi na unyenyekevu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba imani ya baadhi ya watu ni thabiti na ya kuendelea, lakini imani ya wengine ni ya msimu na ya muda fulani tu.

Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya ya 33 na 34 ambazo zinasema:

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمْ وَاخْشَوْا يَوْمًا لّا يَجْزِي وَالِدٌ عَن وَلَدِهِ وَلا مَوْلُودٌ هُوَ جَازٍ عَن وَالِدِهِ شَيْئًا إِنَّ وَعْدَ اللَّهِ حَقٌّ فَلا تَغُرَّنَّكُمُ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا وَلا يَغُرَّنَّكُم بِاللَّهِ الْغَرُورُ

Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi, na iogopeni siku ambayo mzazi hatamfaa mwanawe, wala mwana hatamfaa mzaziwe kwa lolote. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli. Basi yasikudanganyeni maisha ya dunia, wala asikudanganyeni na Mwenyezi Mungu (shetani) mdanganyifu.

إِنَّ اللَّهَ عِندَهُ عِلْمُ السَّاعَةِ وَيُنَزِّلُ الْغَيْثَ وَيَعْلَمُ مَا فِي الأَرْحَامِ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَّاذَا تَكْسِبُ غَدًا وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ بِأَيِّ أَرْضٍ تَمُوتُ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ

Hakika ujuzi wa Saa (ya Kiyama) uko kwa Mwenyezi Mungu. Na Yeye ndiye anaye iteremsha mvua. Na anavijua vilivyomo ndani ya matumbo ya uzazi. Na haijui nafsi yoyote itachuma nini kesho. Wala nafsi yoyote haijui itafia nchi gani. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye khabari.

Aya hizi ambazo ni aya za mwisho za Suratu Luqman zinawausia watu wote kwa ujumla kuchunga taqwa na uchaji Mungu katika maisha yao na kutaja sababu yake kwa kueleza kwamba kinyume na inavyokuwa duniani ambako watu wa familia moja huweza kusaidiana wakati wa matatizo, Siku ya Kiyama hakuna mtu atakayebeba mzigo wa mwenzake wala hakutakuwa na uwezekano wa watu kusaidiana. Kwa hivyo tusiwe na ghururi kwa sababu ya mapenzi na mahusiano ya kifamilia wala tisitarajie kwamba bila ya kuwa na amali njema tutapata rehma za Allah. Daftari la amali za mtu Siku ya Kiyama litahakikiwa na Mwenyezi Mungu Mwenyewe ambaye ni Mjuzi wa yote ya ghaibu yaliyofichikana, seuze ya dhahiri yanayoonekana. Hayo ni pamoja na elimu ya lini kitasimama Kiyama chenyewe, lini na wapi mtu atafikwa na mauti, na hali ya kila jenini ndani ya tumbo la mama.  Kuhusu hili tufahamu kwamba elimu ya Allah kuhusu kilichomo ndani ya tumbo la mama si kuhusu jinsia ya mtoto tu kama ni mwanamke au mwanamme, bali ni pamoja na vipawa atakavyokuwa navyo, hali ya tabia na hulka zake pamoja na mambo mengine chungu nzima ambayo mwanadamu hana ujuzi na uelewa wake. Alaa kulli hal mwanadamu asije akadhani katu kuwa Mwenyezi Mungu hana habari za mambo yake anayofanya kwa siri. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba nasaba na ujamaa hautofaa kitu Siku ya Kiyama. Ikiwa baba na mtoto hawatoweza kufaana, itakuwa jamaa na marafiki wa mtu? Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kujiri kwa Kiyama hakuna chembe ya shaka japokuwa muda wake hatuujui; kama ambavyo mauti hayaepukiki, lakini hakuna anayejijua yatamfika lini na wapi. Ni Allah SW tu ndiye Mjuzi wa hayo. Aidha aya zinatutanabahisha kuwa dunia ina hadaa na ghururi na humghafilisha mtu na Siku ya Kiyama.

Wapenzi wasikilizaji darsa ya 737 ya Qur’ani imefikia tamati na ndiyo inayotuhatimishia pia tarjumi na maelezo ya sura ya 31 ya Luqman. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa wenye kunufaika na kuaidhika na yote tuliyojifunza katika sura hii. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags