Apr 12, 2017 12:59 UTC
  • Wanasayansi Iran waunda roboti la kufunza lugha ya ishara

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala nyingine yenye kuangazia maendeleo ya Iran katika sekta za sayansi, teknolojia na tiba nchini Iran na maeneo mengine duniani.

Tunaanza makala yetu ya leo kwa kuangazia mafanikio ya watafiti Wairani katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Shariff cha Tehran ambao wameunda roboti ya kufunza lugha ya Ishara kwa Kifarsi. Roboti hii ni maalumu kwa ajili ya kuwafunza watoto viziwi na ina uwezo wa kutekeleza harakati za mikono. 

Aidha katika siku za usoni roboti hiyo itakuwa na uwezo wa kuwa na uhusiano na watoto wanaopata mafunzo. Hii leo roboti kama hizi zina nafasi muhimu katika kutibu matatizo ya kitabia na mienendo ya watoto ambao wanaugua ugonjwa wa Autism. Tawahudi (kwa Kiingereza Autism) ni tatizo la kiroho na kihisia linalotokea kwa watu tangu utotoni na kuathiri uwezo wao wa kuwasiliana na watu wengine. Kwa hivyo roboti hiyo yenye uwezo wa kuwa na uhusiano na watoto inaweza kutumika kutoa mafunzo kwa watoto wenye matatizo ya Autism.

Kupunguza mfadhaiko au stress katika watoto wenye maradhi ya saratani ni moja ya kazi zingine muhimu za roboti hiyo yenye uwezo wa kujenga uhusiano na watoto. Roboti kama hizi zinaweza kutumika katika mahospitali ili kupunguza mfadhaiko au stress miongoni mwa watoto. Mradi wa roboti za Rasa katika Chuo Kikuu cha Teknoloaji cha Shariff unalenga kutengeneza roboti zenye uwezo wa kuwa na maingiliano na pia kufunza lugha  ya ishara kwa watoto viziwi.

Roboti ya inayotoa mafunzo ya lugha ya ishara ya Kifarsi kwa watoto

Mohammad  Zakipour mtekelezaji wa mradi huu na ambaye pia ni mwanafunzi wa shahada ya uzamili katika taaluma ya mekaniki katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Shariff anaashiria uwezo wa roboti hiyo iliyoundwa na kulinganisha na roboti zingine za ndani na nje ya Iran zinazoshabihiana nayo na kusema: "Roboti hii inaweza kuzungumza lugha ya ishara kwa Kifarsi. Aidha vidole vya roboti hii vinaweza kutekeleza harakati huru. Halikadhalika roboti hii inaweza kuzunguka daraja 29. Hizi ni  baadhi ya sifa ambazo haziko katika roboti zinazoshabihiana nayo. Roboti hii inaweza pia kutumia picha na sauti na hivyo kuiwezesha kutumia njia hiyo kutoa mafunzo la lugha ya ishara kwa watoto viziwi.

Bw. Zakirpour anaongeza kuwa, uwezo wa kuzungumza roboti hii umekamilika na pia sehemu zake za kutumia taswira zinakaribia kumalizika. Anasema kwa kutumia taswira, roboti hii inaweza kuwa na uhusiano na watoto viziwi na hivyo iwapo mtoto atatumia lugha ya ishara, roboti inaweza kujemga uhusiano wa moja kwa moja na mtoto.

@@@@

Katika mafanikio ya mengine ya uga wa teknolojia, mtafiti Muirani ameweza kuunda mashine yenye uwezo wa kusafisha  na kuondoa vijidudu katika majani makavu ya eneo la kufuga kuku wengi. Chombo hicho kina uwezo wa kukausha na kuondoa vijidudu katika majani makavu wakati kuku wakiwa katika sehemu hiyo pasina kuhitaji kuwaondoa. Mashine hii inahakikisha kuwa kuku wengi wanaofugwa katika ukumbi mkubwa wako katika sehemu safi na hivyo kuzuia magonjwa  kuenea.

Chombo cha kusafisha na kuondoa vijidudu katika eneo la kufugia kuku

Mohammad Khosro, mtaalamu wa masuala ya lishe ya mifugo katika Chuo Kikuu cha Kilimo Cha Gorgan kaskazini mwa Iran anasema: "Kuna mashine kama hii ambayo imetegenezwa Uhispania hivi karibuni; lakini nchini Iran na maeneo mengine duniani kumekuwa kukitumiwa mashine zisizo za kitaalamu au mikono kufanya kazi hizo za usafi katika sehemu za kufugia kuku. Baada ya kusajili uvumbizi wa mashine hii mpya, sasa inatumiwa na wafugaji wa kuku nchini Iran.

@@@@

Mwezi Disemba mwaka 2016 wanasayansi Wairani, kwa mara ya kwanza duniani, walifanikiwa kuunda simiti au seruji kwa kutumia takataka. Mohammad Assadi Mkurugenzi wa Shirika la Seruji la Sepahan mjini Isfahan kati mwa Iran anasema: "Watafiti 30 wamefanya kazi kwa muda wa miaka mitatu na kutumia uwezo wa kielimu wa ndani ya nchi kuzalisha seruji hii. Baada ya kununua mashine za kigeni na kuweka vifaa vinavyohitajika, tumefanikiwa kuunda seruji hii. "

Seruji ya Kijani iliyoundwa Iran

Kutokana na uzingatiwaji mazingira katika uundwaji wake, sasa seruji hii imetajwa kuwa seruji wa kijani. Seruji hii ina uwezo wa asilimia 20 zaidi ya ile ya kawaida . Kiwanda cha Seruji cha Sepahan, Isfahan kila mwaka huzalisha tani milioni moja na nusu ya seruji ya kijani. Kwa kuzingatia ukakamavu wake, seruji hii inaweza kutumika katika kazi muhimu kama vile ujenzi wa mabwawa, madaraja n.k.

Moja ya nukta muhimu zaidi na za kipekee katika uzalishai seruji ya kijani ni kupunguza uchafuzi na uharibifu wa mazingira. Kila mwaka nchini Iran tani milioni 70 za mabaki ya mkaa au clinker huzalishwa kwa ajili ya utegenezaji seruji. Kwa hivyo iwapo viwanda vya seruji nchini vitaanza kutengeneza seruji ya kijani kwa kutegemea teknolojia  hii ya hapa nchini, kunashuhudiwa kupungua tani milioni 25 za mabaki ya mkaa na hivyo kupunguza uchafuzi wa mazingira.

@@@@

Kwingineko wanasayansi Wairani wamefanikiwa kubuni mbinu ya kusafisha maji kwa kutumia electrolysis ya sodium chloride. Kwa mafanikio hayo, Iran inajiunga na kundi la nchi tatu zenye kumiliki teknolojia hii duniani. Watafiti wa Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Amir Kabir mjini Tehran katika hatua ya ubunifu, wameweza kutumia chumvi badala ya gesi hatari ya chlorine katika kusafisha maji. Kwa hivyo mbali na kupunguza hatari zitokanazo na chlorine, wametumia mbinu mpya na yenye gharama za chini katika kutayarisha maji masafi kwa jili ya kunywa, shughuli za kilimo na viwanda. Matumizi asili ya teknolojia hii ni kusafisha maji ambapo kwa njia ya multi-oxidant, hutengeneza bidhaa mpya ambayo huondoa vijidudu katika maji ya kunywa na pia maji ya bwawa la kuogelea n.k.

Kuondoa vijidudu katika maji kwa mbinu ya electrolysis ya sodium chloride

Katika mbinu ambayo imekuwa ikitumiwa kwa muda mrefu, gesi ya chlorine, poda ya chlorine na maji ya kung'arisha ndio mbinu ambazo zimekuwa zikitumiwa kuondoa vijidudu katika maji ya mabwawa ya kuogelea na katika matangi ya kuhifadhi maji ya kunywa. Mbinu hizo ni hatari na yumkini hata gesi za sumu za chlorine zikasalia na kuhatarisha maisha ya watumiaji.

Hamid Ridha Faqihi, mtekelezaji wa mradi huu wa  kusafisha maji kwa kutumia mbinu ya electrolysis ya sodium chloride anasema: "Katika dunia kunaendelezwa mikakati ya kutafuta mbinu mbadala baada ya mbinu za jadi na zilizojaa hatari za kusafisha maji ili yawe salama kwa mwanadamu kunywa au kutumiwa kwa shughuli mbalimbali. Baada ya Marekani na Ujerumani, Iran ni ya tatu duniani kwa umiliki teknolojia ya kisasa ya kusafisha maji kwa kutumia mbinu hiyo." Anasema mafanikio hayo yamepatikana kwa ushirikiano na jitihada za miaka saba za watafiti na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Amir Kabir. Tayari mradi huu umeshaanza kutekelezwa kwa majaribio katika maeneo yenye matatizo ya maji kusini mwa Iran katika kisiwa cha Mino na Eneo la Biashara Huru la Arvand. Kwa mbinu hii watu 16 elfu wa maeneo hayo wameweza kupata maji masafi ya kunywa. Maeneo mengine ya kusini mwa Iran pia yanatazamia kuanza kutumia teknolojia hii ya kusafisha maji katika siku za usoni.