Apr 20, 2017 07:19 UTC
  • Wanasayansi Wairani waunda mkono bandia kwa ajili ya walemavu

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala nyingine yenye kuangazia maendeleo ya Iran katika sekta za sayansi, teknolojia na tiba nchini Iran na maeneo mengine duniani. Katika makala ya leo tutaangazia mafanikio ya Iran katika sekta za seli shina, mkono bandia na kiwanda cha nafaka.

Tunaanza kwa kuangazia mafanikio ya watafiti Wairani katika Taasisi ya Utafiti ya Rooyan ambao kwa kutegemea utafiti waliofanya katika seli shina na seli za matibabu wameweza kufanikiwa kutumia seli hizo kuzuia tatizo sugu la figo kuathirika na kufikia kiwango cha kutoweza kufanya kazi kabisa.

Iwapo figo itakuwa na tatizo la kufanya kazi kwa muda wa miezi mitatu hatimaye hufeli kabisa kufanya kazi na huwa haiwezekani kurudi katika hali ya kawaida. Kuna sababu kadhaa ambazo hupelekea figo kukumbwa na  hali hiyo ya kutofanya kazi lakini hadi sasa hakuna tiba maalumu ya kukabiliana na hali hiyo. Hatua kadhaa huchukuliwa kujaribu kumtuliza mgonjwa.

Seli shina katika maabara

Daktari Ridha Muqaddasi, mwananchama wa jopo la kisayansi cha kitengo cha utafiti wa seli shina katika Taasisi ya Rooyan  ni mhusika mkuu katika mpango huo ujulikanao kama  "Utumizi wa  seli shina za punje ndogondogo zilizo ndani ya mfupa (bone marrow)  katika kutibu tatizo sugu la kufeli figo."

Akifafanua zaidi kuhusu mpango huo anasema: "Uchunguzi uliofanywa katika miaka ya hivi karibuni umebaini kuwa utumizi wa seli shina hasa seli shina za Mesenchymal zinaweza kwa kiasi kikubwa kuzuia kuenea ugonjwa na hata kuboreka hali ya mgonjwa. Kwa msingi huo tunalenga kutumia zaidi seli shina za Mesenchymal  kuzuia kuenea magonjwa."

Hivi sasa awamu ya kwanza ya mradi huo imekamilika na watafiti wametekeleza majaribio ya matokeo ya utafiti wao katika magonjwa saba na katika awamu itakayofuata majaribio yatafanyika katika magonjwa mengine ili kubaini uwezo wa seli shina za Mesenchymal katika kuyatibu.

Lengo la utafiti huo ni kuwasaidia wale wanaougua ugonjwa sugu wa figo lakini bado hawajafika nukta ya kutotibika ili kuwawezesha kuboreka kiafya

Uchunguzi uliofanyika umebaini kuwa seli shina za Mesenchymal zinaweza kuboresha utendaji kazi wa figo lakini mbinu muafaka ya kufanikisha jambo hilo bado haijabainika. Kwa msingi huo, watafiti wanaendeleza uchunguzi kuweza kufikia natija kuhusu mbinu bora zaidi ya kutumia seli shina za Mesenchymal kutibu matatizo ya figo.

Katika mafanikio mengine, wanasayansi Wairani wamefanikiwa kutekeleza mradi wa kuunda mkono bandia ujulikanao kama power hand orthosis ambao hutumiwa na watu wenye ulemavu wa mkono ambao husababishwa na mshtuko wa ubongo. Uvumbuzi huo umeweza kufikiwa katika Chuo Kikuu cha Ustawi wa Kijamii na Tiba ya Marekebisho cha Tehran.

Mkono bandia wa kuwasaidia waliopooza mkono

Kumefanyika utafiti kuhusu kuunda mkono bandia ambao unatumika kuwarekebisha watu waliolemaa mkono kwa sababu ya matatizo katika mfumo mkuu wa neva. Katika mikono iliyopo hivi sasa, pamoja na faida nyingi zilizopo lakini imekuwa na matatizo ambayo yamewawekea vizingiti vingi watumizi.

Lakini moja ya sifa muhimu za mkono huo bandia ujulikanao kwa Kiingereza kama  power hand orthosis na ambao umeundwa katika Chuo Kikuu cha Ustawi wa Kijamii na Tiba za Marekebisho mjini Tehran ni kuwa, si mzito na unaweza kutumika kwa wepesi na unaenda sambamba na sifa za kipekee za matatizo ya kineva ya mtumizi. Aidha mkono huu uliotegenezwa na wanasayansi Wairani unaweza kutumika kirahisi katika kliniki na nyumbani pia. Mradi huu wa kiteknolojia unaendelea kuboreka na unategemea teknolojia ya hapa nchini na sasa awamu yake ya kwanza inakaribia kumalizika.

Kwingineko, wanasayansi Wairani wamefanikiwa kuunda kiwanda kikubwa zaidi cha kusaga na kusafisha nafaka Mashariki ya Kati kwa kutegemea wataalamu wa hapa nchini. 

Kiwanda hicho kilizinduliwa mwezi Januari mwaka huu  katika mkoa wa Alborz magharibi wa Tehran katika sherehe iliyohudhuriwa na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kati ya mafanikio ya kiwanda kiwanda hicho ni kuwa wanasayansi wamefanikiwa kutumia viongeza sukari asili katika nafaka na pia kuunda nafaka yenye virutubisho kwa ajili ya wanadamu na mifugo.

Kiwanda hicho cha kusafisha nafaka pia kinaweza kutoa sukari katika mahindi na kuiwezesha sukari hiyo kutumika sehemu zingine hasa katika kutegeneza sharubati ya glukosi na fraktosi  ambayo hutumika katika viwanda vingine vya chakula na dawa.  Sharubati ya glukosi ambayo huzalishwa katika kiwanda hicho huwa mbadala mzuri wa sukari ya kawaida kwani kiwango chake cha utamu ni asilimia 7 zaidi ya sukari ya kawaida.

Hali kadhalika kiwanda hiki kimeweza kufanikiwa kuzalisha wanga au starch kutoka katika nafaka na kuibadilisha iweze kutumika katika sekta mbali mbali kama vile za viwanda vya nguo, sabuni, gundi, tairi n.k.

Kiwanda cha kusafisha na kusaga nafaka Iran

Mbali na hayo, kiwanda hicho cha kusafisha nafaka Iran kina uwezo wa kutenganisha mada nyingi zilizopo katika mahindi ili kuhakikisha kuwa zao hilo linatumika kikamilifu katika sekta mbali mbali za viwanda mbali na matumizi ya kawaida ya mwanadamu na mifugo.

Bidhaa nyingine ambayo huzalishwa kutoka mahindi katika kiwanda hicho ni Gluten ambayo baada ya kutenganishwa na nafaka hutayarishwa katika muundo ambao asilimia 60 yake huwa ni proteini inayotumika kama chakula kikuu cha ng'ombe wenye kutoa maziwa.

Kiwanda hicho cha kusafisha nafaka Iran pia huweza kutoa mafuta yaliyo katika mahindi ambayo yana matumizi mengi sana yenye manufaa. Hatimaye kiwanda hicho pia huzalisha unga wa mahindi ulio safi na wenye faida nyingi kwa mwili hasa madini mengi kama vile fosfori, potasiamu, magnesium, sodiumu, kalsiamu na chuma.

Pumba za mahindi ni bidhaa nyingine muhimu ya kiwanda hicho cha kusafisha nafaka nchini Iran.

Katika muundo wa pumba ya mahindi  asilimia 20 hadi 22 huwa ni wanga, asilimia 4-5 ni mafuta na asilimia 10-12 ni protini. Bidhaa hii mbali na kuwa ni katika vyakula vya mifugo pia inaweza kutumika katika kuongoza fiber au nyuzi katika bidhaa za chakula cha mwanadamu hasa kwa wale wenye kulenga kupunguza unene.

Kiwanda hicho kinatazamiwa kupanuliwa katika siku za usoni ili kuondoa utegemezi wa nchi hii kwa nchi za kigeni katika vyakula vinavyotokana na nafaka.