May 02, 2017 23:18 UTC
  • Jumatano tarehe 3 Mei, 2017

Leo ni Jumatano tarehe 6 Rajab 1438 Hijria sawa na tarehe 3 Mei, 2017.

Leo ni Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari.

Maadhimisho haya yanalenga kulinda na kutetea uhuru wa vyombo vya habari na kuwaenzi wadau wa sekta hiyo ambao wakati mwingine wanahatarisha maisha yao wakitekeleza wajibu na majukumu yao.

Siku hiyo iliainishwa kutokana na pendekezo lililotolewa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO). Hii leo uhuru wa vyombo vya haabri unabinywa na kukandamizwa na baadhi ya tawala za kidikteta na kimabavu zisizopenda kuona ukweli ukiwafikia watu. Katika upande mwingine uhuru wa vyombo vya habari unatumiwa vibaya na baadhi ya nchi hususan za Magharibi kutangaza kila kitu na makala, picha na filamu chafu na zinazokiuka maadili ya kibinadamu. Mwenendo huo umekwenda mbali zaidi kiasi cha kutumiwa uhuru wa vyombo vya habari kwa ajili ya kuvunjia heshima matukufu ya kidini ya mabilioni ya watu kote duniani.

Siku kama ya leo miaka 588 iliyopita, Jeanne d'Arc alianzisha harakati ya kihistoria ya kuzikomboa baadhi ya ardhi za Ufaransa zilizokuwa zikikaliwa kwa mabavu na Uingereza. Jeanne d'Arc alikuwa kamanda wa jeshi ambaye alipewa jukumu na Mfalme wa Ufaransa la kuongoza mapambano dhidi ya majeshi ya Uingereza yaliyolikalia kwa mabavu eneo la kaskazini mwa Ufaransa. Hatimaye Kamanda huyo alikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kimaonyesho nchini Uingereza kwa tuhuma za kuritadi na kuacha dini na mwaka 1431, aliuawa kwa kuchomwa moto akiwa hai.

Sanamu la Jeanne d'Arc

Siku kama ya leo miaka 548 iliyopita alizaliwa Niccolò di Bernardo dei Machiavelli, mwanahistoria na mwanasiasa wa Italia katika mji wa Florence. Sambamba na shughuli zake za kisiasa, Machiavelli aliandika pia historia ya Florence. Katika mtazamo wa kisiasa, Machiavelli alikuwa akiamini kwamba yawezekana kutumia wenzo wowote ule kwa ajili ya kupata madaraka na kwa ajili ya kuyalinda, na kwamba hakuna udharura wowote wa kuheshimu misingi ya maadili katika masuala kama hayo. Miongoni mwa kazi za mwanahistoria na mwanasiasa huyo wa Italia ni "The Art of War" na "The Prince."

Niccolò di Bernardo dei Machiavelli

Siku kama ya leo miaka 502 iliyopita yaani tarehe 3 Mei 1515 Miladia, manowari za Ureno zilianza kushambulia kisiwa cha Hormoz cha Iran na hivyo kuanzisha wimbi la uingiliaji na ukoloni wa nchi za Magharibi katika eneo la Mashariki ya Kati. Kisiwa hicho kiko katika eneo la kiistratijia la lango la Hormoz lililoko katika Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman, kusini mwa Iran. Kutokana na kuwa Iran ilikuwa dhaifu katika upande wa jeshi la majini, wakoloni wa Kireno walivikalia kwa mabavu visiwa kadhaa vya Iran vilivyoko katika Ghuba ya Uajemi, kikiwemo cha Bahrain ambacho wakati huo kilikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Hatua kwa hatua, Iran iliimarisha jeshi lake la majini, na ilipofika mwaka 1652, iliweza kuvikomboa visiwa vyote vilivyokuwa vikikaliwa kwa mabavu na Wareno.

Kisiwa cha Hormoz

Na siku kama ya leo miaka 210 iliyopita ulitiwa saini Mkataba wa Finckenstein kati ya Iran na Ufaransa wakati mfalme Napoleon wa Ufaransa alipokuwa katika vita na nchi nyingine za Ulaya. Kwa mujibu wa mkataba huo uliokuwa na vipengee 16, ilipangwa kuwa Iran ingepata silaha za aina mbalimbali kutoka Ufaransa kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi ya Warusi. Ufaransa pia iliahidi kutuma wataalamu wa mizinga na wahandisi wa masuala ya kijeshi nchini Iran kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa jeshi la nchi hiyo. Kwa upande wake, Iran iliahidi kukata uhusiano wake na Uingereza na kuisaidia Ufaransa katika kupeleka majeshi yake huko India. 

Mkataba wa Finckenstein