May 03, 2017 21:50 UTC
  • Alkhamisi 4 Mei, 2017

Leo ni Alkhamisi 7 Shaaban 1438 Hijria, sawa na Mei 4, 2017.

Siku kama ya leo miaka 1011 iliyopita Arifu na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu na Kiirani, Khajah Abdullah al Ansari aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 83 katika mji wa Herat. Aliishi katika zama za Khajah Nidhamul Mulk na Abu Said Abul Kheir. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vikiwemo vya Monajatnameh, Asrar, Mohabbatnameh, na Haft Hesar. 

Khajah Abdullah al Ansari

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita chama cha National Socialism cha Ujerumani mashuhuri kwa jina la chama cha Nazi, kilivunjwa rasmi nchini humo. Kwa utaratibu huo kipindi cha utawala wa kidikteta, ukandamizaji na mabavu cha chama hicho ambacho kiliingia madarakani tangu mwaka 1932 nchini Ujerumani, kilifikia ukingoni. Si vibaya kuashiria hapa kuwa, chama cha Nazi kiliundwa mwezi Oktoba mwaka 1920 baada ya kuongezeka harakati ya kisiasa za Munich. Hadi mwaka 1929 chama hicho kilikuwa na wanachama laki moja na 76 elfu tu lakini mwaka 1933 idadi hiyo iliongezeka na kufikia milioni mbili na kuongezeka zaidi hadi kufikia milioni sita katika miaka iliyofuata. Inaelezwa kuwa, chama hicho kilikuwa na lengo la kuyaunganisha mataifa yanayozungumza Kijerumani na kuanzisha dola moja lenye nguvu ambalo lingeweza kupanua mipaka yake. Hata hivyo baada ya kushindwa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia chama hicho cha Nazi kilisambaratika na kutoweka.

Nembo ya chama cha Manazi wa Ujerumani

Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, yaani tarehe 4 Mei mwaka 1958 Miladia, upinzani mkubwa na vita vya ndani nchini Lebanon dhidi ya utawala wa Camille Chamoun vilianza. Chamoun alikuwa rais wa Lebanon tangu mwaka 1952 Miladia, huku akiendesha siasa zilizokuwa mbali na misimamo ya Waarabu na kufuata mtindo wa Magharibi. Siasa hizo ziliibua hasira na upinzani mkali wa Waislamu wa Lebanon na kusababisha kuzuka vita vya ndani nchini humo baada ya Rais Chamoun kutaka kuwaweka madarakani huko Lebanon Wakristo wa Kimaroni.

Na siku kama ya leo miaka 515 iliyopita ardhi ya Costa Rica iligunduliwa katika safari ya nne ya kivumbuzi ya Christopher Columbus. Kwa karne tatu Costa Rica ilikuwa koloni la Uhispania, lakini hatimaye mnamo mwaka 1821 Miladia vikosi vya Uhispania vililazimika kuondoka nchini humo kufuatia mashinikizo viliyoyapata kutoka kwa wananchi wapigania uhuru wa Costa Rica.