May 06, 2017 14:36 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya nne ya makala yanayozungumzia jinai na ukatili wa kutisha unaofanywa na Mabudha wenye kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar.

Kwa hakika hata jeshi la Myanmar  haliwaonei huruma watu wa jamii hiyo. Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa hapo tarehe 19 Disemba mwaka jana, askari na polisi wa serikali ya Myanmar wanawamiminia risasi ovyo raia wa kawaida na wasio na hatia yoyote na kuwaua. Aidha askari hao huwabaka wanawake na mabinti wa Kiislamu, kuzichoma moto nyumba zao, kuwatia mbaroni wanaume na kuwazuilia mahala pasipojulikana bila ya kuwafungulia mashtaka yoyote. Katika hujuma za mwaka 2012 wakati Mabudha walipoanzisha mauaji ya kinyama dhidi ya Waislamu hao, walichoma moto kikamilifu vijiji vya Waislamu na hivyo kuwalazimu Waislamu hao kwenda kuishi katika kambi za wakimbizi.

Baada ya hapo, mauaji ya kutisha dhidi ya Waislamu hao huko kaskazini mwa nchi yaliibuka tena mwezi Oktoba mwaka jana baada ya askari tisa wa kulinda mpaka wa Myanmar kuuawa na watu wasiojulikana. Hata hivyo na bila ya kufanya uchunguzi wala kuwepo ushahidi wowote, serikali ya Burma iliwatuhumu Waislamu wa Rohingya kuwa ndio waliohusika na shambulizi hilo. Viongozi wawili wa Umoja wa Mataifa wamenukuliwa wakisema kuwa, katika operesheni za hivi karibuni za askari wa Myanmar huko kaskazini mwa nchi, zaidi ya Waislamu wa Rohingya 1000 waliuawa.

Maafisa hao wa Umoja wa Mataifa ambao walikuwa wakichunguza jinai hizo wakati Waislamu hao walipokuwa wakikimbia kutokana na ukatili wa askari hao walitangaza idadi kubwa ya maafa hayo kinyume na ile iliyotolewa na serikali ya Burma. Kwa kutegemea ripoti zilizokusanywa kwa kipindi cha miezi minne kutoka kwa wakimbizi hao Waislamu wanaoishi katika kambi za wakimbizi nchini Bangladesh afisa mmoja alisema: "Mazungumzo kuhusiana na mauaji hayo yanaonyesha kujiri maafa makubwa ya watu. Suala hilo linaonyesha kuwepo uwezekano kwamba takwimu zilizotolewa awali na serikali si sahihi.

​Jinai za Mabudha dhidi ya Waislamu

Katika shughuli za uchunguzi huo tulishuhudia mamia ya watu wa kabila la Rohingya wakiwa wameuawa. Ripoti zilizokusanywa kutoka kwa wakimbizi hao zinaonyesha kwamba idadi ya watu waliouawa inavuka idadi ya  watu 1000." Mwisho wa kunukuu.

**************************************

Akthari ya Waislamu wa Rohingya wanaokimbilia nchini Bangladesh wanaishi katika kambi za muda nchini humo huku wengine wakipelekwa katika kambi rasmi za wakimbizi za vijiji vilivyopo kusini mashariki mwa Bangladesh. Wengi wa watu hao mbali na kushuhudia kwa macho yao wenyewe, walikumbwa pia na jinai na ukatili kukiwemo kuteswa, kudhalilishwa au ubakaji wa umati dhidi ya wanawake na mabinti wa Kiislamu, unaofanywa na askari wa Myanmar. Baadhi ya wanawake waliwaelezea wachunguzi hao wa timu ya Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch namna watoto wao wadogo na hata wachanga walivyouawa kwa kukanyagwa na kupondwa na askari katili wa Myanmar?

Askari wa Myanmar wakiwanyanyasa Waislamu

Ripoti ya Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch iliyoandaliwa kuhusiana na ukubwa wa ukandamizaji wa serikali ya Myanmar dhidi ya jamii ya wachache ya Rohingya inasema kuwa, mashambulizi ya kikatili ya hivi karibuni dhidi ya Waislamu yanajumuisha pia uchomaji nyumba 1500 katika miji ya Waislamu, ubakaji na ukatili mbalimbali wa kijinsia dhidi yao. Katika ripoti hiyo pia Human Rights Watch ilitangaza kuwa, mwishoni mwa mwaka jana 2016 askari na polisi wa serikali walianzisha operesheni ya kuwabaka wanawake na wasichana wa Kiislamu wa Rohingya.

Jamii ya wanawake wa Kiislamu Myanmar

Katika ripoti hiyo, ilielezwa kuwa, katika operesheni za jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu, maafisa wa usalama walihusika na vitendo hivyo vya ubakaji katika vijiji zaidi ya tisa ambapo pia walifanya jinai nyingine mbalimbali dhidi ya binaadamu. Mashuhuda waliwaambia maafisa hao wa Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch kwamba, baadhi ya wasichana waliokumbwa na ukatili huo wa kijinsia walikuwa na umri ulio chini ya miaka 13. Priyanka Motaparthy, afisa anayehusika na masuala ya dharura ya Human Rights Watch anasema: "Ukatili wa kutisha dhidi ya wanawake na wasichana wadogo wa Rohingya uliofanywa na askari wa usalama wa Myanmar unafungua kipindi kipya cha dhulma katika historia ya muda mrefu ya gonjwa la ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake wa Burma." Mwisho wa kunukuu.

Ripoti ya kurasa 50 ya Shirika la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa iliyoandaliwa kwa kuwahoji mamia ya Waislamu hao katika maeneo ya Myanmar kulikojiri ukatili huo, ilionyesha pia kujiri vitendo vya ubakaji na udhalilishaji mkubwa wa kijinsia dhidi ya wanawake na mabinti wadogo wa Kiislamu, kuwaua watoto wadogo na jinai nyingine nyingi dhidi ya binaadamu. Inaelezwa kuwa, kwa kipindi cha miezi minne kabla ya kujiri kwa operesheni za usafishaji katika maeneo ya mpakani baina ya nchi hiyo na Bangladesh, zaidi ya Waislamu wa Rohingya elfu 70 walikimbilia nchini Bangladesh kwa ajili ya kuokoa maisha yao. Licha ya kuwepo mashinikizo ya kuitaka serikali ya Bangladesh ifungue mipaka yake ili kuwaruhusu Waislamu hao waweze kuingia nchi hiyo, lakini serikali ya Dhaka ilipuuza mashinikizo hayo huku ikiimarisha askari wa gadi wa kulinda mpaka kwa lengo la kuwazuia Waislamu hao wa Rohingya kuingia ardhi ya nchi hiyo.

Moja ya mitumbwi inayotumika kuwasafirisha Waislamu hao

Kwa kipindi cha miezi mitatu askari walinda mpaka wa Bangladesh waliwazuia maelfu ya watoto na wanawake wa Rohingya kuingia nchi hiyo na hivyo kulazimika kusafiri kwa kutumia mitumbwi na maboti ambayo akthari yalizama maji. Pamoja na hayo karibu Waislamu elfu 73 tangu ulipoanza ukandamizaji wa jeshi la Myanmar waliweza kuvuka mpaka na kuingia Bangladesh katika kipindi cha miezi hiyo minne. Hadi sasa akthari ya wakimbizi hao wanaishi katika kambi za wakimbizi za mji ulio mpakani na mkoa wa Rakhine. Suala hilo ndilo lililomrahisishia kazi Bi, Yang Hee Lee mjumbe wa Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch kuweza kukutana na idadi kubwa ya wakimbizi hao wa Rohingya huko, kusini mashariki mwa Bangladesh hapo tarehe 21 mwezi Februari mwaka 2017.

Eneo ambalo wanaishi maelfu ya Waislamu wa Rohingya baada ya kukimbia mashambulizi ya jeshi la Myanmar. Baada ya hapo, Yang Hee Lee alielekea mjini Dhaka, mji mkuu wa nchi hiyo na kufanya mazungumzo na viongozi wa taifa hilo kuhusiana na kadhia nzima ya mgogoro unaowakabili Waislamu hao. Katika mazungumzo ya pande mbili, viongozi wa Bangladesh walionyesha wasi wasi wao mkubwa kuhusiana na suala hilo. Katika fremu hiyo,

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) liliitaka serikali ya Bangladesh kuruhusu kufanyika mazungumzo juu ya kuwahamishia karibu Waislamu 10000 wa Rohingya nchini Marekani, Canada na baadhi ya nchi za Ulaya. Hata hivyo licha ya baadhi ya nchi hizo hususan Marekani kukataa suala la kuwapokea wakimbizi wa Rohingya, lakini shirika la UNHCR limeendelea kusisitiza utekelezwaji wa suala hilo.

*******************************

Shinji Kubo, mjumbe wa UNHCR nchini Bangladesh anasema: "Umoja wa Mataifa utaendelea kushirikiana na viongozi wanaohusika na suala hilo wakiwemo wa Marekani. Nadhani UN ina msimamo ulio wazi kwa ajili ya ratiba ya kuwahifadhi wakimbizi hao. Karibu maelfu ya Waislamu wa Rohingya tayari wameweza kutambuliwa na kuhifadhiwa." Mwisho wa kunukuu.

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR)

Ndugu wasikilizaji mauaji na ukatili dhidi ya Waislamu wa Rohingya yamekabiliwa na malalamiko ulimwenguni kote. Hii ni kusema kuwa, jumla ya shakhsia 23 na washindi wa zawadi ya amani ya Nobel, sambamba na kuuandikia Umoja wa Mataifa ripoti pana juu ya mauaji hayo, wameutaka umoja huo kuhitimisha haraka mgogoro wa kibinaadamu unaoikabili jamii ya wachache ya Waislamu hao nchini Burma. Katika ripoti hiyo shakhsia hao wameonya vikali juu ya kutokea janga la kibinaadamu na mauaji ya kimbari ya kibaguzi nchini Myanmar. Kadhalika shakhsia hao wamekosoa vikali undumakuwili wa Aung San Suu Kyi, kama mmoja wa washindi wa zawadi hiyo ya amani ya Nobel kushindwa kuwatetea Waislamu wa Rohingya. Aidha machungu yanayoikabili jamii hiyo ya Waislamu yalifikia hata Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis, kuonyesha masikitiko yake kuhusu ukatili huo na kuwaombea dua watu wa jamii hiyo madhulumu. Tarehe nane Februari mwaka huu kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani alitoa hotuba na kulaumu miamala mibaya ya maafisa usalama wa Myanmar katika kuwalenga Waislamu wa Rohingya huku akiwataja Waislamu hao kuwa watu wema na wapenda amani ambao wamekuwa wakikabiliwa na matatizo makubwa na ukatili wa hali ya juu kwa miaka mingi.

Papa Francis alisema

Katika hotuba hiyo Papa Francis alisema: "Ninakusudia leo kwa kushirikiana nanyi, kuwaombea dua maalumu dada na ndugu zetu wa Rohingya nchini Myanmar. Watu hao sasa wamefukuzwa nchini humo. wanatolewa sehemu moja kwenda nyingine. Ni kwa nini wanafukuzwa, ilhali wao ni watu wema na wapenda amani? Sio Wakristo, lakini ni watu wazuri. Wao ni ndugu na dada zetu. Kwa miaka mingi wamevumilia tabu na mateso makubwa. Kutokana na suala jepesi la kufuata dini yao (Waislamu wa Myanmar) ndio wanaadhibiwa na kuuawa. Hebu kwa pamoja tuwaombee dua kaka na dada zetu hawa wa Rohingya." Mwisho wa kunukuu.

Ndugu wasikilizaji sehemu ya nne ya makala haya yanayozungumzia jinai na ukatili wa kutisha unaofanywa na Mabudha wenye kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar inakomea hapa. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./

 

 

 

Tags