May 20, 2017 06:12 UTC
  • Jumamosi, Mei 20, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe 23 Shaaban 1438 Hijria sawa na tarehe 20 Mei mwaka 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 705 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, aliaga dunia Hussein bin Abdallah Tayyebi aliyekuwa na lakabu ya Sharq-deen. Aliondokea kuwa mpokezi wa hadithi na fasihi mkubwa. Abdallah Tayyebi alikuwa amebobea katika elimu za bayani na fasihi na alihesabiwa kuwa miongoni mwa shakhsia wakubwa na wasomi katika zama zake. Waaidha alimu huyo alikuwa akitilia mkazo juu ya kufundisha tafsiri ya Qur'ani pamoja na hadithi. ***

Hussein bin Abdallah Tayyebi

Katika siku kama ya leo miaka 211 iliyopita, alizaliwa John Stuart Mill mwanafalsafa na mchumi wa Uingereza. Stuart Mill alilelewa na kufunzwa na baba yake elimu za mantiki na uchumi na baadaye kuanza kuandika katika magazeti. Mill pia alichaguliwa kuwa mwakilishi wa Bunge la Uingereza kwa duru moja. Vitabu muhimu vya Mchumi wa Kiingereza John Stuart Mill ni vile alivyoviita "Principals of Political Economy " na "Principals of Political Science". Mill aliaga dunia mwaka 1873. ***

John Stuart Mill

Miaka 115 iliyopita katika siku kama ya leo, Jamhuri huru ilitangazwa huko Cuba na wanajeshi wote wa Marekani wakaondoka katika ardhi ya nchi hiyo. Cuba ambayo iligunduliwa na Christopher Columbus tangu mwaka 1492 Miladia, ilikuwa koloni la Uhispania hadi kufikia mwaka 1898 Miladia. Lakini Marekani iliingiza vikosi vyake nchini humo na kuchukua nafasi ya mkoloni Uhispania baada ya kutoa pigo na kuifukuza nchi hiyo huko Cuba, kwa kisingizio eti cha kuwaunga mkono wanamapambano wapigania uhuru wa Cuba.***

Siku kama ya leo miaka 83 iliyopita,  Yemen ilipata kipigo mwishoni mwa vita vilivyojiri kati yake na Saudi Arabia baada ya nchi mbili hizo kuhitilafiana juu ya suala la mpaka na kupelekea kusainiwa makubaliano ya Ta'if kati ya Imam Yahya wa Yemen na Mfalme Abdul-Aziz wa Saudi Arabia. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Yemen iliikabidhi Saudia maeneo ya Najran, Jizan na Asir kwa muda wa miaka 40.***

Bendera ya Yemen

Katika siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Cameroon ilitangaza kupata uhuru wake chini ya mfumo wa jamhuri na siku hii hujulikana kama siku ya taifa nchini humo.  Kwa miaka kadhaa Cameroon ilikoloniwa na Ufaransa na Uingereza na mwaka 1946 Miladia, Umoja wa Mataifa ukaiweka chini ya mamlaka yake ardhi yote ya nchi hiyo. Hata hivyo katika mwaka 1959 Miladia, udhibiti huo uliondolewa, na mwaka mmoja baadaye Cameroon ikatangaza uhuru wake kwa jina la Jamhuri ya Cameroon. Kufuatia kutangazwa kuwa huru nchi hiyo, katiba ya Cameroon ikapasishwa kupitia kura ya maoni na nchi hiyo ikakubaliwa kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa.*** 

Bendera ya Cameroon
Umoja wa Afrika

Na katika siku kama ya leo miaka 35 iliyopita yaani tarehe 30 Ordibehesht mwaka 1361 Hijria Shamshia, marhumu Ayatullah  Akbar Rafsanjani mmoja wa shakhsia muhimu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Spika wa Bunge la Iran wakati huo, alitoa pendekezo la kuundwa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Azad. Awali fikra hiyo ilitolewa katika jamii ya Kiislamu ya watu wa masuala ya Vyuo Vikuu. Baadaye pendekezo hilo liliwasilishwa kwa Imam Khomeini, Muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye aliliunga mkono na kutoa kiwango fulani cha fedha kama msaada kwa Chuo Kikuu hicho. Hii leo Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Azad ndicho Chuo Kikuu kikubwa zaidi kisicho cha kiserikali nchini Iran.***

 

Tags