May 23, 2017 06:54 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya tano ya makala yanayozungumzia jinai na ukatili wa kutisha unaofanywa na Mabudha wenye kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia ezembe unaofanywa na jamii ya kimataifa kuhusiana na jinai zinazofanywa na Mabudha wa Burma kwa kushirikiana na askari wa serikali ya nchi hiyo. Kadhalika tukasema kuwa, mbali na Mabudha hao wakatili kuhusiaka na mauaji hayo ya kutisha, pia wanahusika na vitendo vya ukatili wa kijinsia kukiwemo kuwanajisi kwa kiwango cha kutisha kabisa wanawake wa jamii ya Rohingya wasio kuwa na ulinzi wowote. Leo pia tutaendelea kuzungumzia suala hilo, hivyo endeleeni kuungana nami hadi mwisho wa kipindi hiki. Ndugu wasikilizaji kama tulivyosema ni kwamba, moja ya masuala machungu na yenye kuumiza yanayoihusu jamii ya wachache wa Rohingya ni suala zima la ubakaji na udhalilishaji dhidi ya wanawake na mabiti wa jamii hiyo. Allison Joyce, mpiga picha za habari na raia wa Marekani aliyewahi kuishi kwa muda mrefu katika viunga vya mji wa Cox's Bazar vya mkoa wa Chittagong, nchini Bangladesh, aliamua kushirikiana na wanawake wa Rohingya ili kuudhihirishia ulimwengu machungu ya wanawake hao yanayotokana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia wanavyofanyiwa na askari na Mabudha wa Myanmar. Kuhusiana na suala hilo, Allison Joyce aliazimia kuwafikishia walimwengu kilio cha wanawake wa jamii hiyo. Alianzisha uchunguzi wake kwa kuzungumza na wanawake kadhaa na kwanza alianza na Bi, Nojiba ambaye aliondoka miezi michache iliyopita kutokana kijiji cha Delpara, nchini Myanmar kuingia Bangladesh.

Bi, Nojiba anasema kuwa, kabla ya kulazimika kukimbia makazi yake alikokuwa akiishi, alikuwa ana maisha mazuri ya furaha nchini Myanmar. Lakini furaha hiyo iligeuga na kuwa msiba, baada ya kijiji chao cha Delpara kuvamiwa na askari wa serikali ambao waliwafanyia ukatili mkubwa wanakijiji kukiwemo kuwapiga, kuwatukana, kuwaua, kuwadhalilisha na kuwafanyia kila aina ya maudhi. Anaendelea kusema: "Niliogopa sana. Niliomba dua na nikasoma sana Qur'ani nikitumai kwamba hali ingeboreka. Muda wote niliishi kwa wasi wasi mkubwa. Siku moja kabla ya kukimbilia Bangladesh, askari wa Myanmar walifika katika kijiji chetu. Kwa bahati mbaya askari hao wakagundua mahala nilipokuwa nimejificha mimi na baadhi ya wanawake wengine niliokuwa nao kwenye miti.

Bi, Nojiba

Askari hao waliwachukua wasichana wadogo na kwenda nao katika nyumba zilizokuwa karibu na eneo tulipokuwa tumejificha. Baada ya kuwapiga na kuwatusi, waliwanajisi kwa ukatili mkubwa. Tulikuwa tukisikia sauti za vilio vya wasichana wale. Askari mmoja allinifuata na kuiweka silaha yake kichwani kwangu na kuniamuru niende katika nyumba zile. Nilianza kupiga kelele kuomba msaada huku nikipambana dhidi ya kufanyiwa ukatili huo. Hata hivyo sikuweza kuwashinda." Mwisho wa kunukuu. Siku ya pili tuliamua kukimbilia nchini Bangladesh. Tulitembea masafa marefu kuelekea mto Naf ulio katika mpaka wa Bangladesh na Myanmar. Baada ya hapo tulimpatia pesa mmiliki mmoja wa boti ili aweze kutuvusha kuingia nchi hiyo jirani. Ndipo tukafanikiwa kufika katika kambi ya wakimbizi ya Kutupalong. Aidha Bi, Nojiba anaendelea kusimulia kuwa: "Mwili wangu wote ulikuwa unaumwa. Nilikuwa nikidhani kwamba nisingeweza kutembea tena. Nilihisi udhaifu mkubwa. Pamoja na kwamba hapa kambini hatuna chakula cha kutosha, lakini kwa akali tunaweza kulala vizuri usingizi na wakati watoto wangu wanapoenda nje, huwa ninafahamu kwamba wako salama." Mwisho wa kunukuu. Akizungumza na mshauri wa madaktari wasio na mipaka Nojiba anasema: "Ninataka kusahau tabu zote zilizozipita." Mwisho wa kunukuu.

Farza

Farza, ni msichana mwingine wa Kiislamu mwenye umri wa miaka 17 na mkazi wa kijiji cha Shikhali nchini Burma naye anasimulia kwa kusema kuwa, kabla ya jeshi la Myanmar kushambulia kijiji chao hicho walikuwa wakiishi kwa amani. Anaendelea kusema kuwa, tarehe 16 Januari mwaka huu, kundi la askari wa serikali walivamia nyumba za kijiji hicho na kuwatoa nje wakazi wake. Wakati wakiwatoa nje, askari hao walikuwa wakiwapiga wanakijiji kwa vitako vya bunduki au kwa kuwapiga mateke. Farza anasema kuwa, mbali na kuwapiga waliwafanyia ukatili wa kijinsia kwa kuwanajisi wanawake na kisha wakawafungia ndani ya nyumba moja ambapo yeye na baadhi ya wawanawake wengine walipoteza fahamu kutokana na ukatili huo.

Eneo analoishi Bi, Farza kwa sasa

Alipozinduka alijikuta akiwa ametapakaa damu mwili mzima na ndipo akaamua kutoroka kwenda nchini Bangladesh. Baada ya kufanikiwa kuingia Bangladesh alienda moja kwa moja katika kambi ya wakimbizi ya Balu Kali. Tangu alipotoka Myanmar hadi sasa imepita miezi sita na bado hajaweza kuwasiliana na mume wake ambaye alimuacha Burma. Farza anasema: "Nikiwa bado nchini Myanmar miezi minne iliyopita nilikuwa ninaishi kwa khofu na wasi wasi mwingi sana baada ya kuanza wimbi la mauaji dhidi yetu. Lakini hapa nilipo kwa akali kuna usalama." Mwisho wa kunukuu.

***********************************

Jamalida Begum ni msichana mwingine wa Kiislamu mwenye umri wa miaka 16 ambaye aliingia nchini Bangladesh kutokea kijiji cha Hadgugapara nchini Burma siku chache zilizopita.

Jamalida Begum

Jamalida anasimulia kuwa, miezi michache iliyopita, jeshi la nchi hiyo lilivavia kijiji chao hicho. Katika tukio hilo walimuua mume wake na kuichoma moto nyumba yao pamoja na vitu vyote vilivyokuwa ndani. Siku iliyofuata, askari hao walikizingira kijiji chao. Anaendelea kusimulia kwa kusema: "Askari wale walinitoa pamoja na wanawake wengine nje na kuanza kutufanyia kila aina ya ukatili kukiwemo kutupiga vikali. Tulipiga kelele za kuomba msaada. Nilimuomba sana Mwenyezi Mungu aweze kutuokoa. Askari mmoja alinidhihaki kwa kusema, (Mungu wenu yuko wapi? Mbona haji kuwaokoeni?" Mwisho wa kunukuu.

Jamalida anaendelea kusimulia: "Askari watatu walinishika na kunipeleka msituni na kunielekezea bunduki tatu kichwani. Waliniambia kuwa ikiwa nitajaribu kukaidi basi wataniua. Wakanifanyia ukatili mkubwa wa kijinsia.

Bi, Jamalida Begum

Baada ya wiki kadhaa kupita walikuja kijijini kwetu waandishi wa habari wa kigeni na kukutana nami kwa ajili ya mahojiano juu ya ukatili tuliofanyiwa na askari wa serikali. Baada ya kumalizika mahojiano yale, usiku uliofuatia askari walivamia tena kijiji chetu ambapo walimchinja mwanamume aliyekuwa akiwasaidia kutarjumu wale waandishi wa habari. Baadaye wakaanza kunitafuta mimi nyumba hadi nyumba ambapo majirani walinipa habari hiyo. Baada ya kusikia hivyo nilikimbilia msituni ambapo nilikaa huko siku tano nikila majani ya miti hadi nilipofanikiwa kufika nchini Bangladesh." Mwisho wa kunukuu. Jamalida anasema kuwa, kutokana na ukatili alioushuhudia kwa askari wale wa Myanmar, kila siku huwa anakumbwa na jinamisi usingizini.

Jamila

Jamila mwenye umri wa miaka 16 ni mwanamke mwingine aliyewasili nchini Bangladesh miezi michache iliyopita kutoka kijiji cha Shikhali nchini Myanmar. Jamila anasema kuwa: "Ijumaa ya kwanza ya mwezi Disemba mwaka jana, askari wa Burma walivamia kijiji chao na kuuzingira msikiti wa eneo hilo. Mtu yeyote aliyejaribu kwenda msikitini alikuwa akikamatwa na kuadhibiwa vikali. Siku moja askari hao walivamia nyumbani kwetu. Sikuweza kukimbia kwenda kujificha mahala na hivyo wakawa wamenishika. Walinifunga mikono na miguu kwa Kamba. Baadaye walinichania nguo na kunifanyia ukatili wa kijinsia na nikapoteza fahamu. Baada ya kuzinduka nilikimbilia upande wa Mto Naf na kufanikiwa kufika nchini Bangladesh. Kwa hakika tangu uvamizi wa askari hao ujiri kijijini kwetu sijawahi kupata utulivu. Lakini namshukuru Mungu kwamba hapa kuna amani. nchini hapa ninaweza kulala usingizi kwa amani lakini Burma hata kutoka nje ulikuwa hujui kama utarejea nyumbani salama. Ingawa hadi sasa bado ninakumbwa na jinamizi la ukatili wa askari wa Myanmar usingizini." Mwisho wa kunukuu.

NurJahan

NurJahan mkazi wa kijiji cha Nerbil ni mwanamke mwingine ambaye alikumbwa na ukatili huo wa kijinsia wa askari wa serikali ya Burma. Aliwasili nchini Bangladesh miezi michache iliyopita. NurJahan anasimulia kwa kusema: "Askari watano walivamia nyumba yetu wakanishika. Baadaye walimfunga binti yangu kitambaa usoni ili asione na wakaanza kuninajisi. Baada ya kuzinduka nilikuta askari wale wakiwa wamekwishaondoka huku binti yangu akiwa bado Analia. Siku chache baadaye walimuua mume wangu. Kufuatia hali hiyo niliamua kukimbilia huku Bangladesh. Kabla sijavuka mpaka kuingia nchi hii, nililazimika kuishi siku tatu porini." Mwisho wa kunukuu. Bi, NurJahan anaendelea kusimulia kwa kusema: "Nimeishi miaka 31 nchini Burma. Sikuwahi kuona ukatili kama huu. Nimewasiliana na baadhi ya ndugu zangu waliohai niliowaacha huko Myanmar, wameniambia kuwa, leo tena askari hao wa serikali wamevamia kwa mara nyingine kijiji chetu cha Nerbil na wakazichoma moto ndevu za ami yangu akiwa hai.

NurJahan akiwasiliana na baadhi ya ndugu zake waliosalia huko Myanmar

Siku zote nimekuwa nikikumbwa na jinamizi kwa khofu kwamba isije ikatokea askari wale wakafika hata Bangladesh." Mwisho wa kunukuu.

**********************************

Mwanamke mwingine aliyesimulia ukatili wa askari hao ni Bi, Yasamin mkazi wa kijiji cha Nayneh Chong nchini Myanmar.

Bi, Yasamin

Yasamin anasimulia kwa kusema: "Askari hao wakatili walivamia nyumba yetu, wakamshikilia mume wangu na kwenda naye kusikojulikana. Kisha askari wanne wakaninajisi vikali. Baadaye nilikimbilia msituni ambapo niliishi huko kwa muda wa siku saba mtawalia. Nilifika kando ya Mto Naf na kumpa kiasi cha kyat elfu 30 za Myanmar ambazo ni sawa na Dola 22, mtu mmoja anayejishughulisha na kazi ya kuwavusha watu ili aweze kuniokoa. Hadi sasa tangu nilipofika Bangladesh, sijapata kuwasiliana na mume wangu wala sijui kama yupo hai au amekwishauawa." Mwisho wa kunukuu.

Nur Kalima

Nur Kalima ambaye naye ana miezi michache tangu awasili Bangladesh kutoka Myanmar, ni mwanamke mwingine anayesimulia ukatilia wa kutisha wa askari wa Burma dhidi ya Waislamu wakiwemo wanawake. Kalima anasimulia kwamba, majirani wake wengi waliuawa na askari hao. Anasema, kutokana na haraka aliyokuwa nayo katika kukimbia jinai hizo, hakuweza kukimbia na baba na mama yake.

Ndugu wasikilizaji sehemu ya tano ya makala haya yanayozungumzia jinai na ukatili wa kutisha unaofanywa na Mabudha wenye kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./

 

 

 

Tags