May 24, 2017 16:54 UTC

Sura ya As-Sajdah, aya ya 10-14 (Darsa ya 740)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 740 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni aya ya 32 ya As-Sajdah. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 10 na ya 11 ambazo zinasema:

وَقَالُوا أَإِذَا ضَلَلْنَا فِي الْأَرْضِ أَإِنَّا لَفِي خَلْقٍ جَدِيدٍ بَلْ هُم بِلِقَاءِ رَبِّهِمْ كَافِرُونَ

Nao husema: Tutapo kwisha potea chini ya ardhi, ni kweli tutarudishwa katika umbo jipya? Bali wao wanakanusha kuwa watakutana na Mola wao Mlezi.

 قُلْ يَتَوَفَّاكُم مَّلَكُ الْمَوْتِ الَّذِي وُكِّلَ بِكُمْ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّكُمْ تُرْجَعُونَ 

Sema: Atakufisheni Malaika wa mauti aliye wakilishwa kwenu; kisha mtarejeshwa kwa Mola wenu Mlezi.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia namna mwanadamu alivyoumbwa. Aya hizi tulizosoma zinazungumzia mauti na kueleza kwamba: Wanaokanusha Kiyama wanasema: Wakati mwanadamu anapokufa na kuzikwa kwenye udongo viungo vyote vya mwili wake huoza na kusagika; kwa hivyo hakuna chochote kinachosalia katika mwili wake hata aweze kufufuliwa Siku ya Kiyama na kuwa na uhai tena! Mwenyezi Mungu Mtukufu anawajibu kwa kuwaambia: Kile kinachoingia kwenye udongo kikasagika na kugeuka vitu vingine ni kiwiliwili tu cha mwanaadamu lakini roho yake tunayompa wakati wa uhai wake huwa inachukuliwa tena na Malaika. Roho hiyo Siku ya Kiyama itaungana na kiwiliwili kilicho sawa na kiwiliwili chake cha duniani. Na kwa njia hiyo mwanadamu aliyekuwa hai tena atahudhurishwa kwenye uwanja wa Siku ya Kiyama.

Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Ma’adi, yaani kufufuliwa kwa viumbe kutakuwa kwa sura ya kimwili. Na kwa hakika kile ambacho washirikina wakikitilia shaka na kukikanusha ni ufufuliwaji huo wa kimwili wa viumbe. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa hakika ya mwanadamu ni roho yake si kiwiliwili chake; kwa hivyo kutoweka kwa viungo vya mwili wake kama mikono na miguu au macho, hakumfanyi kiumbe huyo ahisi sehemu ya hakika yake imetoweka na dhati yake imekuwa na kasoro na upungufu.

Tunaiendeleza darsa yetu hii kwa aya ya 12 ambayo inasema:

وَلَوْ تَرَىٰ إِذِ الْمُجْرِمُونَ نَاكِسُو رُءُوسِهِمْ عِندَ رَبِّهِمْ رَبَّنَا أَبْصَرْنَا وَسَمِعْنَا فَارْجِعْنَا نَعْمَلْ صَالِحًا إِنَّا مُوقِنُونَ

Na ungeli waona wakosefu wanavyo inamisha vichwa vyao mbele ya Mola wao Mlezi, (wakisema): Mola wetu Mlezi! Tumeshaona na tumeshasikia. Turejeshe tukatende mema, kwani hakika sisi tumekwisha kuwa na yakini sasa.

Aya zilizotangulia zilizungumzia imani ya washirikina ya kukanusha Kiyama na Ma’adi. Aya hii inamhutubu Bwana Mtume Muhammad SAW na waumini ya kwamba: Laiti kama ungeliwaona waovu hawa hawa watakavyoinamisha nyuso zao chini Siku ya Kiyama kwa aibu na kuomba warudi tena duniani, hali ya kuwa ombi lao hilo halitokubaliwa. Wakati watakapoiona Pepo na Moto na kusikia sauti za watu wa motoni wanaolia na kuugua kwa makali na uchungu wa adhabu watasema ewe Mwenyezi Mungu, sisi hatukanushi tena Kiyama kwa sababu tumeshakiona kwa macho yetu na sasa tuna yakini nacho. Lakini kukiri huko kutakuwa kumefanyika kwa kuchelewa na hakutawafalia kitu. Wataulizwa wakati huo, kwani hamkuyasikia maneno ya Mitume na hamkuiona miujiza waliyokuleteeni?! Kwa nini mliyapuuza yote hayo na kujifanya kama hamuyasikii wala hamuyaoni?! Basi hata hamkuyachukulia maneno yao kuwa yana uwezekano wa kuwa na ukweli? Mlikuwa na hoja yoyote ya kuyapinga maneno na wito wao wa kimantika? Au mliamua kuwakanusha tu ili muweze kuyafikia matakwa na matamanio yenu ya nafsi, na kwa dhana yenu muwe huru kwa kila hali na kuishi maishi yenu kwa raha? Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Kiyama ni siku ya kuaibika waasi na waovu; ni wale ambao duniani walikuwa wakiwadhalilisha waumini na kuwaita wajinga na wapumbavu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa waumini ni watu waliotanabahi; na tokea hapa duniani wana yakini ya Kiyama na Pepo na Moto. Lakini makafiri watagutuka na kuzinduka, na macho na masikio yao kufunguka Siku ya Kiyama na kupata yakini ya mambo hayo. Na sababu ni kuwa Kiyama ni siku ya kufichuka hakika za mambo na kufunguka macho na masikio ya watu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba kitakacho kujamfaa mtu Siku ya Kiyama na kumfanya aokoke ni amali zake njema na za kheri.

Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya 13 na 14 ambazo zinasema:

وَلَوْ شِئْنَا لَآتَيْنَا كُلَّ نَفْسٍ هُدَاهَا وَلَـٰكِنْ حَقَّ الْقَوْلُ مِنِّي لَأَمْلَأَنَّ جَهَنَّمَ مِنَ الْجِنَّةِ وَالنَّاسِ أَجْمَعِينَ

Na lau tungeli taka tunge mpa kila mtu uwongofu wake (kwa lazima). Lakini imehakikika kauli kutoka kwangu: kwa yakini nitaijaza Jahannamu kwa wote hawa, majini na watu.

فَذُوقُوا بِمَا نَسِيتُمْ لِقَاءَ يَوْمِكُمْ هَـٰذَا إِنَّا نَسِينَاكُمْ وَذُوقُوا عَذَابَ الْخُلْدِ بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ

Basi onjeni kwa vile mlivyo usahau mkutano wa Siku yenu hii. Na sisi hakika tunakusahauni. Basi onjeni adhabu ya milele kwa yale mliyo kuwa mkiyatenda.  

Aya hizi zinatilia mkazo sifa ya uongofu kama ni jambo la hiyari na kueleza kwamba Mwenyezi Mungu amewawekea wanadamu wote nyenzo za kuufikia uongofu ikiwemo kuwapelekea Mitume na vitabu vya mbinguni pamoja na akili na fitra, yaani maumbile ya mwanadamu mwenyewe. Pamoja na hayo wanadamu wana hiyari ya kukubali au kukataa kuufuata uongofu. Allah SW na Mitume wake hawawalazimishi watu kwa kuwataka waiamini na kuifuata haki kwa nguvu. Lakini ni wazi kwamba yeyote anayeukataa uongofu wa Allah atapotea kwa kufuata njia ya dhalala na upotofu na hatima yake itakuwa ni kuishia kwenye moto wa Jahanamu. Kwa msingi huo, Mitume, wao huwa ni kama walimu, ambao huwasomesha wanafunzi masomo kwa ukamilifu lakini hawamlazimishi yeyote kusoma na kudurusu masomo yake. Na ni wadhihi kwamba ifikapo mwisho wa mwaka wanafunzi ambao ni wavivu hufeli; na wao wenyewe hujikosesha mengi katika maisha haya ya dunia.

Baadhi ya watu wanasema: Vipi inawezekana kwa Mwenyezi Mungu mwenye Rehma awatie na kuwaunguza waja wake kwenye moto wa Jahannam?! Aya hizi tulizosoma zinaijibu dhana na mtazamo huo potofu kwa kusema: Rehema za Mwenyezi Mungu zinaendelea kumteremkia mja maadamu mja mwenyewe hajazifunga njia za kuteremkiwa na rehema hizo. Rehma hizo zinakuwepo ikiwa mja mtenda madhambi atajuta na kutubia kwa madhambi yake, kwa sababu Mwenyezi Mungu ni mwingi wa kupokea toba na mrehemevu. Lakini mja aliye muovu na mfanya madhambi ambaye hatubii kwa aliyoyafanya bali anashupalia na kudumu kufanya dhambi, dhulma na ufisadi wala hafikirii kutubia na kujirekebisha, huyo huwa hajibakishii fursa ya kupata rehma za kughufiriwa na kusamehewa madhambi yake na kuokoka na adhabu ya Allah. Watu wa aina hiyo ni mitihili ya mtu aliyesimama kwenye ukingo wa maporomoko; wakati wenzake wanapomwasa na kumtahadharisha kuwa hapo ulipo ni hatari na uko kwenye ukingo wa maporomoko huwa hajali chochote bali anazidi kusogea mbele kwenye ukingo wa njia isiyo sahihi mpaka mwishowe huporomoka kwenye bonde la maangamizi. Baadhi ya mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hizi ni kwamba kufuata uongofu utokao kwa Allah ni jambo la hiyari si la kulazimishwa, kwa sababu imani ya kulazimishwa haina thamani wala itibari. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, upana na ukithirifu wa rehma za Allah hauzuwii ghadhabu zake kuwashukia waovu na madhalimu. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba Mwenyezi Mungu hamsahau katu mja wake isipokuwa yeye mja atakapotaka mwenyewe asahauliwe na Mola. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa kusahau Ma’adi yaani kufufuliwa na kurejea kwa Mola ndiyo chimbuko la madhambi na matendo maovu na kumfanya mtu afikwe na adhabu kali. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 740 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamuomba Allah atupe mema duniani na akatupe mema akhera na atulinde na adhabu ya moto. Wassalamu Alaykum warahmatullahi Wabarakatuh.

Tags