Jumanne 13 Juni, 2017
Leo ni Jumanne tarehe 18 Ramadhani 1438 Hijiria sawa na tarehe 13 Juni 2017.
Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 23 Khordad 1362 Hijria Shamsia, Bi. Nusrat Amin, faqihi na mfasiri mkubwa wa Qurani Tukufu alifariki dunia katika mji wa Esfahan ulioko katikati mwa Iran. Bi. Nusrat Amin aliutumia muda wake wote katika kuishughulikia Qurani Tukufu, na kufanikiwa kufasiri juzuu 15 za Qurani na kuandika vitabu vingi. Miongoni ma vitabu vya msomi huyu ni Assair Wassuuk na Nafahaat Rahmaniyya.
Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, inayosadifiana na 23 Khordad 1359 Hijria Shamsia, Imam Ruhullah Khomeini muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiwa na lengo la kuleta mabadiliko katika vyuo vikuu hapa nchini, alitoa amri ya kuasisiwa Baraza la Mapinduzi la Kiutamaduni. Katika ujumbe wake, Imam Khomeini MA aliwataka wajumbe wa baraza hilo kuratibu na kuandaa mipango na mitalaa katika kozi mbalimbali za vyuo vikuu inayokwenda sambamba na mafunzo ya utamaduni tajiri wa Kiislamu.
Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita sawa na tarehe 13 Juni mwaka 1944, kombora la kwanza la ardhi kwa ardhi la Ujerumani ya Kinazi lililojulikana kwa jina la V-1 lilishambulia ardhi ya Uingereza, katika Vita vya Pili vya Dunia. Kabla ya hapo Ujerumani ilikuwa ikiishambulia ardhi ya Uingereza kwa njia ya anga. Baada ya vita hivyo, nchi nyingine duniani zilitengeneza makombora ya aina hiyo kwa teknolojia ya kisasa zaidi.
Siku kama ya leo miaka 96 iliyopita, muwafaka na tarehe 13 Juni 1921 katika miaka ya mwanzo ya usimamizi wa Uingereza huko Palestina, ilianza harakati kubwa ya kwanza ya wananchi katika ardhi yote ya Palestina dhidi ya Wazayuni. Harakati ya wananchi hao wa Palestina ilibainisha upinzani wao dhidi ya siasa za kikoloni za Uingereza pamoja na uungaji mkono wa nchi hiyo kwa Wazayuni waliokuwa wakiishi Palestina. Katika fremu ya sera hizo za Uingereza mwaka 1923 kulikuwa na Wazayuni 35 elfu huko Palestina na kabla ya kuundwa utawala bandia wa Israel mwaka 1948 idadi hiyo ilikuwa zaidi ya laki sita.
Siku kama ya leo miaka 125 iliyopita Ayatullah Zainul Abidin Mazandarani mmoja wa maulamaa wakubwa wa Kiislamu na marjaa Taqliq wa Mashia aliaga dunia. Baada ya kuhitimu masomo ya awali, Ayatullah Mazandarani alielekea Karbala na kisha hauza ya kielimu ya Najaf huko Iraq ili kukamilisha masomo ya kidini. Akiwa huko mwanazuoni huyo alifunzwa na maustadhi wakubwa wa zama hizo wa hauza ya Najaf na kufikia daraja ya juu ya kielimu na kimaanawi.
Miaka 111 iliyopita katika siku kama hii, chama cha Sinn Féin kilianzishwa kama tawi la kisiasa la jeshi la Warepublican wa Ireland katika kisiwa cha Ireland, magharibi mwa Uingereza. Ireland ilikuwa koloni la Uingereza na chama hicho kiliasisiwa kwa lengo la kupigania uhuru wa kisiwa hicho na mwandishi wa habari maarufu wa eneo hilo aliyeitwa Arthur Griffith. Baada ya kuendesha mapambano na mashinikizo mengi dhidi ya serikali ya Uingereza mwaka 1921 Ireland ya Kusini ilipata uhuru.