Jun 20, 2017 22:13 UTC
  • Jumatano, Juni 21, 2017

Leo ni Jumatano tarehe 26 Ramadhani, 1438 Hijria, sawa na Juni 21, 2017.

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita inayosadifiana na tarehe 31 Khordad 1360 Hijria Shamsia, sawa na tarehe 21 Juni mwaka 1981, aliuawa shahidi Dakta Mustafa Chamran, msomi na kamanda shujaa wa vikosi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakati wa vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. Dakta Chamran alifanikiwa kupata shahada katika fani ya elektroniki na kisha alielekea Marekani ambako alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu. Kwa miaka kadhaa Dakta Chamran alikuwa nchini Lebanon kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa nchi hiyo waliokuwa wakipambana na utawala wa Kizayuni wa Israel. Mara baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu Dakta Chamran alichaguliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na kisha akawa mbunge wa Tehran. 

Dakta Mustafa Chamran

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita yaani sawa na tarehe 21 Juni 1970, alifariki dunia Dakta Ahmed Sukarno mpigania uhuru wa Indonesia. Sukarno alizaliwa mwaka 1901, na alikuwa mstari wa mbele katika mapambano yake dhidi ya mkoloni Mholanzi nchini humo. Kwa minajili hiyo, Sukarno aliwahi kukamatwa na kufungwa jela miaka minne na utawala wa kikoloni wa Uholanzi. Baada ya kifungo hicho alitiwa tena mbaroni na kubaidishwa. Mnamo mwaka 1949 alichaguliwa kuwa Rais wa Indonesia na ilipofika mwaka 1965 Ahmed Sukarno aliondolewa madarakani baada ya kufanyika mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Janerali Suharto.

Dakta Ahmed Sukarno

Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, inayosadifiana na 31 Khordad 1369 Hijria Shamsia, mikoa ya Gilan na Zanjan iliyoko kaskazini na kaskazini magharibi mwa Iran ilikumbwa na mtetemeko mkubwa wa ardhi wenye ukubwa wa 7.3 kwa kipimo cha rishta, na kuleta maafa makubwa. Zaidi ya watu elfu hamsini walifariki dunia na wengine zaidi ya elfu sitini kujeruhiwa, na laki tano kukosa makaazi. Mtetemeko huo licha ya maafa yake kwa binadamu, ulisababisha hasara kubwa ya kiuchumi kwa wananchi na serikali, na hasa kwenye miundombinu.

Siku kama ya leo miaka 313 iliyopita inayosadifiana na 26 Ramadhani 1125 Hijria, alifariki dunia Sheikh Muhammad Khansari mwenye lakabu ya Jamaluddin, mmoja kati ya wasomi wakubwa nchini Iran katika karne ya 11 na 12 Hijria Qamaria. Sheikh Khansari alizalwia katika familia ya kidini na kupata elimu mbalimbali katika mji wqa Esfahan ulioko katikati mwa Iran. Albobea zaidi katika elimu za mantiki, falsafa, fiqhi, usuul fiqh na tafsiri ya Qur'ani. 

Sheikh Jamaluddin Muhammad Khansari