Jumanne 18 Julai, 2017
Leo ni Jumanne tarehe 23 Shawwal 1438 Hijria sawa na Julai 18, 2017
Siku kama ya leo miaka 29, iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikubali azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Azimio hilo lilizitaka nchi mbili za Iran na Iraq kusitisha vita na kufanya suluhu. Jamhuri ya Kiislamu ilikubali azimio hilo kutokana na baadhi ya vipengele vyake hususan kile kinachohusiana na kuitambulisha Iraq kuwa ndiye mchokozi katika vita hivyo na kuitaka iilipe Iran fidia ya hasara za vita hivyo. Hata hivyo utawala wa Saddam Hussein ambao pia ulikubali azimio hilo la Baraza la Usalama, uliendeleza mashambulizi dhidi ya ardhi ya Iran.
Siku kama ya leo miaka 1146 iliyopita, kilianza kipindi cha vita vya miaka 25 kati ya Uingereza na Denmark katika karne ya 9. Alfred The Great, mfalme kijana wa Uingereza alikuwa kamanda mashuhuri wakati wa kujiri vita hivyo katika kipindi hicho. Wadenmark katika siku hiyo waliivamia Uingereza na kuiteka ardhi kubwa ya nchi hiyo. Vita hivyo vilivyodumu kwa miaka 25 hatimaye vilifikia tamati kwa Waingereza kupata ushindi mnamo tarehe 9 Januari mwaka 896.
Katika siku kama ya leo miaka 326 iliyopita alifariki dunia Sayyid Neematulllah Jazairi aliyekuwa faqihi na mpokezi mkubwa wa hadithi wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 62. Alikuwa hodari katika elimu za fiqhi, hadithi, tafsiri ya Qur'ani na fasihi ya lugha ya Kiarabu na alistahamili mashaka mengi katika njia ya kulingania sheria za dini ya Kiislamu. Sayyid Neematullah Jazairi ameandika vitabu kadhaa vya thamani kama Madinatul Hadith, Qiswasul Anbiyaa na Hidayatul Muuminin.
Miaka 235 iliyopita katika siku kama ya leo William Herschel, mtaalamu maarufu wa nujumu wa Uingereza alifanikiwa kugundua hakika ya kundi la nyota na sayari ikiwemo hii yetu ya dunia. Alitumia darubini kubwa aliyokuwa ametengeneza kwa ajili ya kutazama nyota na kuthibitisha kwamba, kundi la nyota na sayari linaundwa na nyota nyingi ikiwemo sayari ya dunia ambayo ni sehemu ndogo sana ya kundi hilo. Herschel pia ndiye mvumbuzi wa sayari ya Uranus. Alifariki dunia mwaka 1822 akiwa na umri wa miaka 84.