Jumapili, Julai 30, 2017
Leo ni Jumapili tarehe 6 Dhul-Qaadah mwaka 1438 Hijria, sawa na tarehe 30 Julai, 2017 Miladia.
Katika kalenda ya Kifarsi, tarehe nane Mordad ni siku ya kumuenzi shahidi Shahab al-Din Yahya ibn Habash Suhrawardi, maarufu kwa jina la 'Sheikh Ishraaq'. Shahab al-Din Yahya ibn Habash Suhrawardi, aliyekuwa tabibu, mtaalamu wa elimu ya theolojia, fasihi na falsafa alizaliwa mwaka 549 Hijiria katika mji wa Suhrawardi uliopo katika viunga vya mji wa Zanjan nchini Iran. Baada ya kusoma usul fiqhi alisomea elimu ya falsafa na kutokana na uelewa wake wa hali ya juu, aliweza pia kutabahari katika elimu mbalimbali za zama zake. Alipingana katika masuala mengi na wasomi waliomtangulia huku akitumia pia baadhi ya istilahi za falsafa za Iran na zile za dini ya Uzartoshti kiasi cha kuwafanya watu wenye taasubi kumtuhumu kuwa ni kafiri au mpinga dini na kwa kutegemea rai za maulama wa mji wa Aleppo, wakatoa amri ya kuuawa kwake. Hatimaye mwaka 587 akauawa huku akiwa na umri wa miaka 38. Suhrawardi ameacha athari mbalimbali kwa lugha ya Kiarabu na Kifarsi katika fani mbalimbali.
Siku kama ya leo miaka 124 iliyopita, alifariki dunia Sayydi Mirza Abul-Hassan Jeloh, mtaalamu wa elimu ya Irfan na mwalimu mkubwa wa elimu ya akhlaq. Sayydi Jeloh alizaliwa mwaka 1238 Hijiria katika mji wa Ahmedabad nchini India. Nasabu ya shakhsia huyo inarudi nyuma hadi kwa Imam Hassan Mujtaba (as), mjukuu wa Mtume Muhammad (saw). Akiwa kijana mdogo na akiwa na familia yake alielekea mjini Isfahan na kujishughulisha na utafutaji elimu na njia ya ukamilifu (yaani ya kumjua Mwenyezi Mungu). Mwaka 1273 Hijiria alielekea mji wa Tehran ambapo aliishi mjini hapo kwa zaidi ya miaka 40 akifundisha katika shule ya Darul-Shafaa elimu za falsafa, hisabati na Irfan. Maulama kama vile Mirza Tahir Tankapani, Ayatullah Muhammad Ali Shah Abadi, Seyid Hüseyn Badkubeyi, Mula Muhammad Amoli, Jahangir Khan Ghashghaei, Allamah Tabataba na wengine wengi, ni miongoni mwa wanafunzi wa Sayydi Mirza Abul-Hassan Jeloh. Ameacha athari mbalimbali katika elimu za falsafa na Irfan.
Siku kama ya leo miaka 119 iliyopita, alifariki dunia Otto von Bismarck, Kansela wa kwanza na mwanasiasa mkongwe wa Ujerumani. Bismarck aliongoza vita vitatu ambavyo viliainisha mustakbali wa Ujerumani kama nchi huku akikabiliana pia na madola ya Ulaya wakati huo. Bismarck alikuwa rais wa Prussia akiwa na umri wa miaka 28 na kwa mara ya kwanza akawa pia Kansela wa Ujerumani. Mwaka 1862 aliteuliwa kuwa waziri mkuu wa Prussia na kuanzisha mpango wa Ujerumani moja. Ili kufikia lengo hilo hakuwa na njia nyingine ghairi ya kuiondoa Austria katika shirikisho la majimbo ya Ujerumani ya Kikatoliki sambamba na kulikomboa jimbo la Schleswig-Holstein kutoka udhibiti wa Denmark na kuhitimisha upenyaji wa Ufaransa katika majimbo ya kusini mwa Ujerumani. Baada ya kujiimarisha kijeshi alipigana vita vitatu na kufikia malengo yake katika vita vyote hivyo. Kwa mujibu wa historia, Otto von Bismarck alizishinda nchi za Denmark, Austria na Ufaransa, kulikoenda sambamba na kuteuliwa kuwa kansela wa Ujerumani mwaka 1890.
Siku kama ya leo miaka 87 iliyopita alifariki dunia, Ayatullah Mirza Swadiq Agha Mujtahed Tabrizi. Agha Mujtahed Tabrizi aliyekuwa mtoto wa alimu mkubwa wa sheria za Kiislamu na theolojia, yaani Allamah Mirza Muhammad Agha, maarufu kwa jina la Mujtahed Kuchak, alizaliwa mwaka 1273 Hijiria mjini Tabriz. Akiwa na umri wa miaka 19 na huku akiwa na kaka yake, alihajiri kwenda mjini Najaf Iraq ambapo aliishi huko kwa miaka 24. Alipata kusoma elimu mbalimbali kutoka kwa wasomi wakubwa wa zama hizo. Mwaka 1312 alielekea mjini Tehran na baadaye akaelekea mji alikozaliwa. Ameacha athari mbalimbali katika taaluma za fiqhi na theolojia.
Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita alifariki dunia mvumbuzi wa Kimarekani anayejulikana kama baba wa sekta ya utengenezaji magari wa nchi hiyo Henry Ford. Alizaliwa tarehe 30 Julai 1863 katika familia ya kimaskini na tangu utotoni alikuwa na hamu kubwa ya masuala ya umekanika. Siku moja Ford aliona gari likitembea barabarani bila ya kuvutwa na farisi na akaamua kutengeneza gari lake mwenyewe. Henry Ford alifanyia majaribio mkokoteni wa kwanza usiotumia farasi akiwa na umri wa miaka 12 tu. Mvumbuzi huyo aliboresha zaidi mkokoteni huo na mwaka 1896 akafanikiwa kutengeneza gari lake la kwanza. Mwaka 1895 alipewa kibali cha kutengeneza magari licha ya kwamba watu wengine pia walikuwa wakitengeneza chombo hicho na mwaka 1903 aliasisi kampuni ya magari ya Ford Motor. Ford aliwapiku watengeneza magari wengine kwa kutengeneza magari mengi ya bei rahisi.
Siku kama ya leo miaka 10 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Ali Akbar Faydh mashuhuri kwa jina la Ayatullah Mishkini. Ayatullah Mishkini alisoma kwa wanazuoni wakubwa wa zama hizo kama Ayatullah Burujerdi na Imam Khomeini. Alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kujiunga na harakati ya mapambano ya Imam Khomeini dhidi ya utawala wa Shah. Alitiwa nguvuni na kufungwa jela mara kadhaa sambamba na kubaidishwa. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Mishkini alishika nyadhifa mbalimbali, na muhimu zaidi ni ile ya Mwenyekiti wa Baraza la Wanazuoni Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu na Kusimamia Kazi zake. Alimu huyo ameandika vitabu vingi.