Sep 02, 2017 15:46 UTC

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya tatu ya makala yanayozungumzia chuki na matukio ya kibaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla huko katika nchi za Magharibi.

Katika kipindi kilichopita tulisema kuwa katika mataifa ya Magharibi kuna asilimia ya kuzingatiwa ya idadi kubwa ya Waislamu na ambayo haifai kupuuzwa. Tukasema kuwa zaidi ya Waislamu milioni tatu wanaishi nchini Uingereza, huku nchi yenye kiwango kikubwa cha Waislamu barani Ulaya ikiwa ni Ufaransa ambapo karibu Waislamu milioni sita wanaishi ndani ya nchi hiyo pekee, na kwamba hata mataifa mengine ya Magharibi pia yana idadi ya Waislamu ambayo haiwezi kupuuzwa. Leo tutazungumzia mienendo hasi ya madola ya Magharibi kuuhusu Uislamu. Ndugu wasikilizaji mienendo ya madola ya Magharibi ndio imepelekea kupanuka kwa chuki dhidi ya watu wa dini nyingine ndani ya mataifa hayo. Aidha ni vyema kwa madola ya Magharibi kuweka wazi msimamo wao juu ya ugaidi. Hii ni kwa kuwa hadi sasa madola hayo yamegawa ugaidi katika pande mbili, za ugaidi mbaya na mzuri ambapo katika uwanja huo yanatumia siasa na propaganda kuzilenga nchi nyingine zisio washirika ili kufikia njama zao.

Na kwa upande mwingine ni kwamba, kuugawa ugaidi katika pande mbili kumezifanya hata jamii za mataifa hayo ya Ulaya kukumbwa na hatari kubwa ya janga hilo. Hii ni kusema kuwa siasa za undumakuwili kuhusiana na sula hilo kumezifanya nchi hizo kushirikiana na tawala ambazo zinalea ugaidi. Ni kwa msingi huo ndio maana tukasema kuwa, hivi sasa mataifa ya Ulaya si tu kwamba yanakabiliwa na tishio la ugaidi wa nje bali yanakabiliwa pia na ugaidi wa ndani. Moja ya hatua ambazo zinaweza kuthibitisha suala hilo ni kujiri mabadiliko katika mahusiano ya nchi hizo za Magharibi na nchi ambazo ndio chanzo cha kudhihiri misimamo ya kuchupa mipaka ndani ya eneo la Mashariki ya Kati na ulimwengu kwa ujumla. Kuhusiana na suala hilo, Jeremy Corbyn kiongozi wa chama cha Labour nchini Uingereza ameitaka serikali ya London kuangalia upya mahusiano yake na Saudia sambamba na kupiga marufuku ya kuiuzia nchi hiyo silaha zake. Hata hivyo lau kama Corbyn angekuwa ni Waziri Mkuu wa Uingereza asingetoa matamshi kama hayo na badala yake angekuwa kama Theresa May, Waziri Mkuu wa sasa wa nchi hiyo ambaye kwa kuzingatia maslahi ya kisiasa na kiuchumi ameamua kushirikiana na Saudia na kuendelea kuiuzia silaha ambazo zinatumika katika kufanya mauaji ya halaiki dhidi ya raia madhlum wa Yemen.

*************************

Ndugu wasikilizaji kama tulivyosema kuwa chuki na ubaguzi wa rangi dhidi ya Uislamu ni mpango ulioandaliwa na madola ya Magharibi. Hata kama baadhi ya viongozi wa nchi za Kimagharibi huwa wanatoa matamshi kwamba Uislamu ni dini ya amani na maridhiano na kwamba vitendo vya makundi ya kigaidi na ukufurishaji vinakinzana na mafundisho yaliyoletwa na Mtume Muhammad (saw) ambaye ni Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu, lakini katika siasa za utendaji viongozi hao wamekuwa wakihusika moja kwa moja katika kuyaimarisha makundi hayo ya ukufurishaji na ugaidi.

Kampeni dhidi ya Uislamu huko Magharibi

Ukweli ni kwamba, kwa upande mmoja viongozi hao wanakiri kwamba makundi ya kigaidi na ukufurishaji hayana mahusiano yoyote na mafundisho ya dini ya Uislamu inayolingania uadilifu na amani, huku kwa upande wa pili wakihusika katika kuyaimarisha na kuyaunga mkono makundi hayo hatari. Bi Theresa May, Waziri Mkuu wa Uingereza akiwa waziri wa mambo ya ndani au waziri mkuu kwa mara kadhaa amekuwa akiashiria asili ya kundi la kigaidi la Daesh. Kama mlivyosikia katika kipindi kilichopita, May aliweka wazi msimamo wake kwamba Daesh linakinzana wazi na mafundisho ya Uislamu. Theresa May ambaye miaka mitatu iliyopita alikuwa waziri wa chama cha wahafidhina nchini Uingereza aliyasema hayo kufuatia kifo kilichoibua hisia za wengi cha David Cawthorne Haines aliyekuwa raia wa Uingereza na mwanaharakati wa haki za binaadamu na aliyeuliwa na wanachama wa kundi hilo la (ISIS) huko nchini Syria kwa kusema: " Wanajiita utawala wa Kiislamu, lakini acheni nikuelezeni ukweli. Hao sio dola wala sio Uislamu. Idolojia zao za kuchukiza hazina mahusiano yoyote na Uislamu halisi." Mwisho wa kunukuu." Mwisho wa kunukuu. Aidha Bi Theressa May aliashiria nukta nyingine muhimu ambazo zinaonyesha ufahamu alionao juu ya mafundisho ya Uislamu kwa mfano tu alisema: "Qur'an inasema, Hakuna kulazimishana katika dini." Kadhalika alienda mbali na kuongeza "Hivyo acheni nifikishe ujumbe ndani ya ukumbi huu, kwamba makundi yenye misimamo mikali hayataweza kutugawa. Acheni tuweke wazi ujumbe huu kwamba sisi tunafahamu kuwa, dini ya Uislamu ni dini ya amani na haina mahusiano yoyote na idiolojia ya uadui. Acheni tushikamane bega kwa bega na Waislamu wa Uingereza. Watu ambao wamekusanyika na kutoa nara ya 'Hapana', basi tunatakiwa sisi sote kwa pamoja tusimame kupinga idiolojia za namna hiyo na kuzishinda na hivyo tuwaepushe vijana wa Uingereza na misimamo ya kuchupa mipaka." Mwisho wa kunukuu. Hata hivyo ndugu wasikilizaji licha ya viongozi hao wa Magharibi kufahamu uhalisia huo wa kuhusu kutofungamana dini ya Kiislamu na aina yoyote na ugaidi, lakini kivitendo hawajafanya juhudi yoyote yenye lengo la kupunguza chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu kupitia vyombo vyao vya habari au katika nyuga za kisiasa. Kinyume chake kila pale kunapotokea tukio lolote la kigaidi, ni viongozi hao hao ndio huwa mstari wa mbele kuutaja Uislamu na Waislamu kuwa ndio wahusika wake na hivyo kupalilia moto wa chuki na mashambulizi kuwalenga wafuasi wa dini hiyo ya amani na maeneo yao ya kidini kama vile misikiti na hata makaburi yao.

********************************

 Katika miezi ya hivi karibuni Uingereza ilishuhudia mashambulizi kadhaa ya kigaidi mjini Londona na Manchester ambapo katika hujuma hizo watu 35 waliuawa. Katika shambulizi la nne na la tano la kigaidi wahanga wake walikuwa ni Waislamu ambao walishambuliwa baada ya kuwa wamemaliza kuswali msikitini. Katika ripoti ya hivi karibuni kabisa gazeti la Uingereza la The Independent liliandika kuwa, jinai zinazohusiana na chuki dhidi ya Uislamu ni zaidi ya ubaguzi wa rangi dhidi ya dini, jinai ambazo zimeshika kasi zaidi kwa namna ambayo haijashuhudiwa, hasa baada ya Uingereza kutangaza kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya (Brexit). Kwa mujibu wa uchunguzi wa hivi karibuni uliofanywa na polisi ya nchi hiyo, kiwango cha matukio yanayohusiana na chuki, kimeongezeka zaidi nchini Uingereza katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita baada ya kufanyika kwa kura ya maoni na kufikia zaidi ya asilimia 50 katika maeneo tofauti ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la The Independent baadhi ya taasisi za Kiislamu zimeelezea ongezeko la jinai za chuki kuwalenga Waislamu nchini humo. Aidha ni kwamba, kesi nyingi zilizoripotiwa kuanzia mwezi April mwaka huu kuwalenga Waislamu zilijumuisha mashambulizi ya ndani ya vyombo vya usafiri wa umma, kuwafukuwa kazini katika mashirika makubwa ya kibiashara, kuzuiliwa kufanya marasimu ya kidini ikiwemo swala hususan kwa wanafunzi wanaohitimu shule na kesi nyingi mfano wa hizo.

Ugaidi ulivyo na mahusiano asilia na utawala wa Aal-Saud

Katika mataifa mengine ya Magharibi pia mienendo ya ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya Waislamu imeripotiwa kwa ongezeko kubwa zaidi. Moja ya uthibitisho wa wimbi hilo ni ongezeko la mirengo ya kulia yenye misimamo mikali, ubaguzi na chuki ya hali ya juu dhidi ya dini ya Kiislamu na Waislamu kwa ujumla. Hata hivyo madola ya Magharibi hayafanyi juhudi yoyote ile kwa ajili ya kupunguza chuki hizo dhidi ya Uislamu. Licha ya kufahamu kwamba ugaidi ni moja ya vitisho vikubwa vinavyohatarisha usalama, lakini katika uga wa kisiasa ndio kwanza yanaendelea kuyaimarisha zaidi magenge hayo kwa silaha na fedha. Hii ni kusema kuwa, serikali ya Uingereza kwa kushirikiana na Marekani imekuwa ikisaidia kueneza harakati za ukufurishaji na kigaidi. Miezi michache iliyopita harakati za wananchi kwa kushirikiana na majeshi ya serikali za Syria na Iraq zilifikia mafanikio makubwa kwa kuwatimua magaidi wa genge la Daesh kutoka katika maeneo waliyokuwa wanayadhibiti magaidi hao. Pamoja na hayo weledi wengi wa masuala ya kisiasa bado walikuwa na nadharia tofauti juu ya mafanikio hayo muhimu.

****************************

Ndugu wasikilizaji akthari waliamini kuwa, madamu vyanzo vya kifedha vya makundi hayo bado vinaendelea, basi hatari ya makundi ya kigaidi na ukufurishaji bado itaendelea kuwepo. Hii ikiwa na maana kwamba, kubakia hai tishio la makundi ya ukufurishaji na kigaidi, kuna maana ya kubakia hai pia fikra za chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu huko katika nchi za Kimagharibi. Hii ni kwa kuwa, makundi hayo yamepelekea kuchafuliwa sura halisi ya dini ya Uislamu na mafundisho ya dini hiyo yanayolingania uadilifu, amani na maridhiano. Hivi sasa kunaibuka swali hili kwamba, madola ya Magharibi ni kivipi yanaunga mkono harakati za ukufurishaji na kigaidi na kadhalika chuki za dhidi ya Uislamu katika mataifa yao? Katika kikao cha Kundi la G20 mjini Hamburg, Ujerumani, suala lililowasilishwa lilikuwa ni kuzuia vyanzo vya makundi ya kigaidi hususan genge la ukufurishaji la Daesh (ISIS). Karibu nchi zote zilizoshiriki mkutano huo ikiwemo Saudia ziliunga mkono pendekezo hilo. Hata hivyo nukta ya kichekesho ni hii kwamba, hakuna nchi hata moja ya Kimagharibi ambayo ilikuwa tayari kutaja kwamba makundi hayo hatari ya kigaidi yanalishwa fikra za uchupaji mipaka na fedha na nchi gani ya dunia. Aidha katika fremu hiyo hiyo nchini Uingereza kulifanyika chunguzi mbili juu ya chanzo cha kifikra na kifedha kwa makundi ya ukufurishaji na kigaidi. Moja ya chunguzi hizo ilitolewa mwanzoni mwa mwezi Julai mwaka huu huku nyingine ikizuiliwa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Theressa May ambapo haijatangazwa hadi sasa.

Ndugu wasikilizaji sehemu ya 3 ya makala haya yanayozungumzia chuki na ubaguzi unaofanywa na viongozi na serikali za nchi za Magharibi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./

 

Tags