Sep 18, 2017 02:14 UTC
  • Jumatatu tarehe 18 Septemba, 2017

Leo ni Jumatatu tarehe 27 Dhulhija 1438 Hijria sawa na Septemba 18, 2017.

Miaka 29 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 27 Shahrivar mwaka 1367 Hijria Shamsia, aliaga dunia, Ustadh Muhammad Hussein Shahriyar mshairi mashuhuri wa Kiirani. Alizaliwa mjini Tabriz kaskazini magharibi mwa Iran na baada  ya kumaliza masomo yake ya sekondari katika Chuo cha Dar al-Funun mjini Tehran alijiunga na chuo cha tiba. Hata hivyo baada ya miaka michache aliacha masomo na kurejea katika kijiji alichozaliwa. Ustadh Shahariyar alitoa mashairi yake ya kwanza akiwa na umri wa miaka 23. Sambamba na kushadidi harakati za Mapinduzi ya Kiislamu nchini, Shahriyar aliungana na wimbi hilo kwa kutumia mashairi yake. Vilevile alikuwa mashuhuri sana kwa kumpenda Mtume wa Ahlubaiti zake na mapenzi hayo yalidhihiri katika tungo na mashairi yake.

Ustadh Muhammad Hussein Shahriyar

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita yaani tarehe 18 Septemba mwaka 1961 aliaga dunia Dag Hammarskjold mwanasiasa na Katibu Mkuu wa Pili wa Umoja wa Mataifa. Mwanasiasa huyo wa nchini Sweden alifariki dunia baada ya ndege iliyokuwa imembeba wakati wa safari yake katika ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuanguka. Hammarskjold alikuwa Congo kwa lengo la kufanya mazungumzo na pande husika ili kumaliza vita vya ndani nchini humo. Mwanasiasa huyo alizaliwa mwaka 1905 na alihesabiwa katika zama zake kuwa mmoja kati ya waandishi stadi nchini Sweden. Mwaka 1952, Dag Hammarskjold alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobeli kutokana na harakati zake za kuimarisha amani duniani.

Dag Hammarskjold

Katika siku kama ya leo miaka 308 iliyopita, alizaliwa Samuel Johnson mwandishi wa drama, malenga na mwandishi wa visa wa Kiingereza. Alianza shughuli zake za fasihi sambamba na ukosoaji wake katika taaluma hiyo. Baada ya muda mwanatamthilia huyo aliingia katika uga wa utunzi wa mashairi. Samuel Johnson aliaga dunia mwaka 1784.

Samuel Johnson

Siku kama ya leo miaka 747 iliyopita, alifariki dunia Muslihud-Din Sa’adi Shirazi, malenga na mwalimu mkubwa wa mashairi na tenzi za lugha ya Kifarsi. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali katika uga wa lugha na masomo ya dini, Sa’adi Shirazi alielekea mjini Baghdad, Iraq kwa ajili ya kujiendeleza kielimu. Akiwa mjini hapo alijifunza masomo ya elimu za enzi hizo, huku akifanya safari katika maeneo mbalimbali kama vile Sham, Palestina, Hijazi, Roma na nchi nyingine za dunia. Katika safari hizo, Sa’adi Shirazi alipata kujifunza tamaduni za watu tofauti na hivyo akaongeza kipaji chake katika kusoma mashairi. Baadaye alirejea eneo alikozaliwa na kujikita katika kutoa elimu kwa vijana wa mji huo. Mwaka 655 malenga huyo alihitimisha kazi ya kuandika kitabu muhimu kwa jila la Bustan kilichojumuisha masuala ya akhlaqi na malezi bora ambacho alianza kukiandika akiwa katika safari zake hizo.

Muslihud-Din Sa’adi Shirazi