Oct 12, 2017 02:45 UTC
  • Alkhamisi tarehe 12 Oktoba, 2017

Leo ni Alkhamisi tarehe 21 Muharram 1439 Hijria, sawa na tarehe 12 Oktoba mwaka 2017.

Leo tarehe 20 mwezi wa Mehri kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, inasadifiana na maadhimisho ya kumuenzi Khaja Shamsuddin Muhammad Hafiz Shirazi, mshairi na malenga mkubwa wa Kiirani. Hafiz alizaliwa mwaka 727 Hijiria Shamsia mjini Shiraz moja kati ya miji ya kusini mwa Iran. Alikuwa mtaalamu wa tafsiri ya Qur'ani, falsafa na fasihi ya Kiarabu na alipata umashuhuri kwa jina la Hafiz kutokana na kuhifadhi kwake Qur'ani Tukufu kwa visomo tofauti. Mbali na elimu hizo, Khaja Shamsuddin Muhammad Hafiz, alikuwa mtaalamu mkubwa wa elimu ya Irfan.

Kaburi la Hafiz Shirazi katika mji wa Shiraz

Siku kama ya leo miaka 713 iliyopita inayosadifiana na tarehe 21 Muharram 726 Hijria, alifariki dunia faqihi na msomi mashuhuri wa ulimwengu wa Kiislamu, Hassan bin Yussuf bin Mutahhari Hilli, maarufu kwa jina la Allamah Hilli. Allamah Hilli alipata elimu kwa wanazuoni wakubwa kama Khaja Nasiruddin Tusi na anatajwa kama miongoni mwa wasomi wa kipekee wa zama zake. Ameandika zaidi ya vitabu mia moja katika taaluma mbalimbali za Kiislamu. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni 'Tadhkiratul Fuqahaa' ambacho kinaelezea mitazamo mbalimbali za madhehebu ya Kiislamu, tafsiri ya Qurani Tukufu ya 'Nahjul Imaan' na 'Muntahaal Matwalib'.

Allamah Hilli

Tarehe 12 Oktoba miaka 525 iliyopita mvumbuzi na baharia wa Kitalini, Christopher Columbus alivumbua bara la America. Columbus alianza safari yake ya baharini kwa kutumia merikebu tarehe 3 Agosti mwaka 1492 kutoka kwenywe bandari ya Palos nchini Uhispania akielekea kwenye Bahari ya Atlantic. Baharia huyo hakujua kwamba anaelekea bara America na kwa msingi huo tarehe 12 Oktoba 1492 na baada ya safari ya siku 70 baharini alipoona nchi kavu kwa mbali alidhani kuwa anakaribia Asia, kwa sababu alikua akiamini kwamba ardhi ina umbo la mviringo. Kwa msingi huo Christopher Columbus alivipa visiwa alivyokuwa amegundua jina la India ya Magharibi.   

Christopher Columbus

Na siku kama ya leo miaka 18 iliyopita, Jenerali Parviz Musharraf, aliyekuwa mkuu wa majeshi ya Pakistan alifanya mapinduzi yasiyo ya umwagaji damu na kumuondoa madarakani Waziri Mkuu wa wakati huo wa nchi hiyo Muhammad Nawaz Sharrif. Baada ya mapinduzi hayo Musharraf ambaye alichukuwa madaraka ya rais wa nchi, alivifanyia mabadiliko baadhi ya vipengee vya katiba ya nchi hiyo na kuzidisha nguvu na uwezo wa rais. Hata hivyo kutokana na kuongezeka mashinikizo ya ndani na nje, Musharraf alisalimu amri mwezi Novemba 2007 na kuachia cheo cha Mkuu wa majeshi ya Pakistan. Musharraf aliondoka kikamilifu madarakani mwezi Julai 2008, baada ya kushika kasi vyama vya upinzani ambavyo vilishinda uchaguzi wa rais.

Jenerali Parviz Musharraf