Nov 27, 2017 15:39 UTC
  • Jumapili, Novemba 26, 2017

Leo ni Jumapili tarehe saba Rabiul-Awwal Mfungo Sita 1439 Hijria, sawa na tarehe 26 Novemba 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1097 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 64 Ali Bin Muhammad Tanukhi, alimu, mtaalamu wa fasihi na malengo mashuhuri wa karne ya nne Hijiria, huko mjini Basra, kusini mwa Iraq. Alizaliwa mjini Antakya (Antioch) mashariki mwa Uturuki ya Leo ambapo akiwa kijana mdogo alielekea mjini Baghdad, Iraq na kufanya makazi. Ali Bin Muhammad Tanukhi alitabahari katika elimu ya nahw, lugha, uhandisi na fasihi, huku akihesabika kuwa mmoja wa wasomi mashuhuri wa zama zake. Baada ya kuishi sana Baghdad, hatimaye Tanukhi alielekea mjini Basra na kujishughulisha na kazi ya ukadhi na ni kwa ajili hiyo ndio maana akatokea kuitwa kwa jina la Kadhi Tanukhi. Aidha mbali na kuwa na elimu ya juu pia msomi huyo alipata umashuhuri kwa kutoa hotuba. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na kitabu cha 'al-Uruudh'.

Ali Bin Muhammad Tanukhi

Siku kama ya leo miaka 162 iliyopita, alifariki dunia mjini Istanbul, mji mkuu wa utawala wa Othmania Adam Mitskevich, malenga na mwandishi mkubwa wa nchini Poland. Alizaliwa mwaka 1798 na kama alivyokuwa baba yake, akajiingiza katika harakati za kupigania uhuru. Adam Mitskevich aliishi katika kipindi ambacho Poland ilikuwa imegawanywa kati ya Urusi ya zamani, Austria na Prussia ambapo yeye alikuwa akifanya juhudi za kujaribu kuionganisha tena nchi yake. Ni kwa ajili hiyo ndio maana mwaka 1823 akabaidishwa nchini Russia. Hata hivyo baada ya miaka sita alilazimika kutoroka nchi hiyo na kuingia Ufaransa ambapo akiwa huko alijishughulisha na kazi ya kufundisha fasihi. Baada ya hapo Adam Mitskevich alielekea mjini Istanbul, Uturuki ambapo akiwa hapo alikuwa na lengo la kuunda kikosi cha jeshi la Wapoland kitakachokuwa na jukumu la kupambana na Russia ya zamani. Hata hivyo alifariki dunia kabla ya kukamilisha lengo lake hilo. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na kitabu cha 'Jioni ya Mababu' na 'Wafanyaziara wa Polanda'.

Adam Mitskevich

Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, mkutano wa siku 3 wa viongozi wa Marekani, Uingereza na Umoja wa Sovieti ulifanyika mjini Tehran katika hali ambayo, Iran wakati huo ilikuwa chini ya uvamizi wa majeshi ya nchi hizo. Mkutano wa Tehran ulifanyika baada ya Marekani kuingia katika Vita vya Pili vya Dunia na kuzuka kambi mpya dhidi ya jeshi la Ujerumani. Walioshiriki katika mkutano huo walikuwa Rais Franklin Delano Roosevelt wa Marekani, Waziri Mkuu wa Uingereza, Winston Churchill na Joseph Stalin kiongozi wa wakati huo wa Umoja wa Kisovieti.

Katika kikao hicho

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 85 Ayatullah Muhammad Gharawi Kashani, msomi mkubwa wa sheria za Kiislamu (fiqhi) na mwanamapambano mkubwa wa wa ulimwengu wa Kiislamu nchini Iran. Alizaliwa mjini Kashan, moja ya mikoa ya katikati mwa Iran katika familia ya elimu na watu wa fadhila. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi msomi huyo mkubwa alianza kusoma elimu ya dini mjini Kashan na Isfahan ambapo baada ya hapo alielekea mjini Najaf, Iraq kwa ajili ya kuendelea zaidi na masomo. Akiwa mjini Najaf, Ayatullah Muhammad Gharawi Kashani alipata kusoma kwa maulama wakubwa wa mji huo. Aidha alimu huyo hakutenganisha katu kati ya elimu na dini na daima aliamini kuwa ni mambo yasiyokubali kutengana. Mbali na kuwalea wanafunzi, pia alikuwa akipambana vikali na utawala wa kidikteta wa Shah.

Ayatullah Muhammad Gharawi Kashani,

Siku kama ya leo miaka 9 iliyopita, watu karibu 200 waliuawa na wengine wanaokaribia 300 kujeruhiwa katika mji wa Mumbai nchini India kufuatia mashambulio kadhaa ya kigaidi na mapigano ya siku tatu baina ya vikosi vya usalama na magaidi. Hoteli kubwa mbili na kituo kikuu cha treni katika mji huo wa kibiashara wa Mumbai vililengwa katika mashambulio hayo ya kigaidi. Serikali ya India iliibebesha lawama Pakistan na kuituhumu kwamba, ilihusika katika mashambulio hayo. India ilidai kuwa, magaidi hao walipata mafunzo nchini Pakistan. Hata hivyo Pakistan ilikanusha madai hayo na kutangaza kuwa, iko tayari kushiriki katika uchunguzi wa pamoja na India ili kuwasaka wahusika wakuu wa mashambulio hayo ya kigaidi.

Shambulio la kigaidi

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, jeshi la kujitolea la wananchi (Basiji) liliundwa kutokana na amri ya Imam Khomeini mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kuundwa jeshi la watu milioni 20 nchini Iran. Taasisi hiyo ya wananchi kutoka matabaka mbalimbali ya kijamii, kwa kuwa na wapiganaji wenye imani, moyo wa kujitolea na ari ya kuchapakazi imekuwa na nafasi muhimu katika matukio mbalimbali ya Mapinduzi ya Kiislamu hasa kipindi chote cha vita vya kujihami kutakatifu vya taifa la Iran dhidi ya uvamizi wa Iraq. Jeshi la Basiji bado linashiriki katika masuala mbalimbali ya kijamii, kiutamaduni na kijeshi hapa nchini Iran. 

Na siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, Ustadh Mirkhani, mmoja wa waalimu hodari wa Sanaa ya hati na maandishi ya kuvutia wa Iran aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 80. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali alijifunza Sanaa ya hati kwa walimu mahiri wa Iran katika fani hiyo. Kwa muda mfupi Mirkhani aliweza kufikia daraja ya ualimu katika Sanaa hiyo na kisha akaanza kufundisha. Ustadh Mirkhani alikuwa na kipaji maalumu katikak Sanaa ya hati huku akiwa stadi pia katika utunzi wa mashairi.

Ustadh Mirkhani