Jumatano tarehe 29 Novemba 2017
Leo ni Jumatano tarehe 10 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1439 Hijria sawa na Novemba 29, 2017.
Siku kama ya leo miaka 1484 iliyopita alifariki dunia babu yake Mtume, Abdul Muttalib katika mji wa Makka. Mtukufu huyo alikuwa miongoni mwa wakuu wa kabila la Kuraish kabla ya kudhihiri Uislamu na alikuwa hodari mno katika fasihi ya lugha ya Kiarabu. Bwana Abdul Muttalib alikuwa msimamizi na mshika ufunguo wa nyumba tukufu ya al-Kaaba. Vilevile babu huyo wa Mtume alikuwa akitayarisha chakula na maji kwa ajili ya watu wanaozuru nyumba hiyo ya Mwenyezi Mungu na kazi hiyo aliirithi kutoka kwa baba yake. Aliheshimu mno mikataba na ahadi zake na kwa sababu hiyo alikuwa na ushawishi mkubwa baina ya watu. Miongoni mwa watoto wa mtukufu huyo ni Abdullah, baba yake Mtume wetu Muhammad (saw) na Abu Twalib, baba yake Imam Ali bin Abi Twalib (as).

Tarehe 10 Rabiul Awwal miaka 1467 iliyopita, miaka 28 kabla ya Hijra, Mtukufu Mtume Muhammad (saw) alimuoa Bibi Khadija binti Khuwailid (as). Bibi Khadija alikuwa mwanamke sharifu, mwenye imani na maarufu kwa ukarimu wake katika zama za ujahilia na alikuwa maarufu kwa lakabu ya "Twahira" kwa maana ya msafi na mtoharifu. Baada ya kufunga ndoa na Nabii Muhammad (saw) Bibi Khadija alikuwa msaidizi mkubwa na mwenzi wa mtukufu huyo katika hatua zote za maisha yake. Alisabilia kila kitu kwa ajili ya Uislamu na Mtume Muhammad (saw). Bibi Khadija (as) aliishi pamoja na Mtume kipindi cha miaka 25 na daima alikuwa mke mwema na mwenye kujitolea kwa mumewe Mtume Muhammad (saw) mbora wa walimwengu.

Siku kama ya leo 497 iliyopita, Ferdinand Magellan baharia wa Kihispania alifanikiwa kuvuka mkono bahari ambao leo hii umepewa jina lake yaani Lango Bahari la Magellan na akafika katika bahari ya Pacific kupitia bahari ya Atlantic. Wakati huo Ferdinand Magellan alikuwa akijishughulisha na masuala ya uvumbuzi wa baharini katika pwani ya Amerika ya Kusini.
Katika siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, Harakati ya Ukombozi ya Kupambana na Ufashisti iliundwa nchini Yugoslavia chini ya uongozi wa Josip Broz Tito. Wapiganaji wa harakati hiyo walitoa pigo kubwa kwa wanajeshi wa Ujerumani wakati Yugoslavia ilipokuwa ikikaliwa kwa mabavu na jeshi la Ujerumani. Mwaka 1944 wapiganaji wa harakati ya ukombozi ya kupambana na Ufashisti nchini Yugoslavia waliwafukuza nchini mwao wanajeshi vamizi wa Ujerumani kwa kusaidiwa na jeshi Jekundu la Urusi ya zamani.
Miaka 70 iliyopita katika siku kama ya leo, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliunga mkono kwa wingi wa ushindi mdogo suala la kugawanywa ardhi za Palestina baina ya serikali mbili yaani ya Palestina na ya Kiyahudi. Uamuzi huo usio wa kiadilifu na usio wa kimantiki ulichukuliwa chini ya ushawishi wa serikali za Magharibi hususan Marekani na Uingereza.

Miaka 23 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 8 Azar mwaka 1373 alifariki dunia Ayatullah Muhammad Ali Araki, mmoja wa marjaa wakubwa wa taqlidi wa Waislamu akiwa na umri wa miaka 103. Mwanzuoni huyo wa Kiislamu alizaliwa katika mji wa Arak katikati mwa Iran na tangu akiwa na umri mdogo alikuwa na shauku kubwa ya kujifunza elimu ya dini. Ayatullah Muhammad Ali Araki kwa muda mrefu alifundisha katika chuo kikuu cha kidini cha Qum na miongoni mwa vitabu vyake ni risala ya Ijitihadi na Taqlidi pamoja na Sherhe ya Uruwatul Uthqaa.
Siku kama ya leo miaka 7 iliyopita sawa na tarehe 8 mwezi Azar mwaka 1389 Hijria Shamsia, Madakta Majid Shahriyari na Fereydun Abbasi waliokuwa Wahadhiri wa Fizikia ya Nyuklia wa Iran walilengwa katika mashambulio mawili tofauti ya kigaidi mjini Tehran. Dakta Abbasi alijeruhiwa ambapo Dakta Majid Shahriyari Mhadhiri wa Chuo Kikuu, Mwanafizikia na Msomi wa Nyuklia wa Iran akauawa shahidi katika shambulio hilo. Magaidi waliofanya jinai hiyo walitiwa nguvuni na kukiri kwamba, wanashirikiana na shirika la ujasusi la Israel MOSSAD.