Dec 02, 2017 23:11 UTC
  • Jumapili, Disemba 3, 2017

Leo ni Jumapili tarehe 14 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1439 Hijria, sawa na tarehe 3 Disemba 2017 Miladia.

Miaka 1375 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 14 Mfunguo Sita mwaka 64 Hijria, Yazid bin Muawiya alikufa huko Sham (Syria ya leo) baada ya kutawala kwa muda wa miaka mitatu na miezi tisa. Katika mwaka wa kwanza wa utawala wake wa kidhulma, Yazid bin Muawiya alitoa amri ya kuuliwa kikatili Imam Hussein AS, mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad SAW pamoja na wanawe na wafuasi wake watiifu katika jangwa la Karbala. Katika mwaka wa pili wa ukhalifa wake, aliwaua kwa umati wakazi wa mji mtukufu wa Madina na katika mwaka wa mwisho wa utawala wa Yazid, mji mtakatifu wa Makkah ulizingirwa na Masjidul Haram ikaharibiwa. Kabla ya kutwaa madaraka kwa nguvu, Yazid bin Muawiya bin Abi Sufyan alikuwa ameghiriki katika maasi na maisha ya anasa na hakuwa na utambuzi wowote juu ya misingi na mafundisho ya Kiislamu. Waislamu walimchukia sana Yazid kutokana na dhulma na ukatili mkubwa aliowafanyia Watu wa Nyumba toharifu ya Bwana Mtume Muhammad SAW na wapenzi wa Ahlul Bait AS na kutokana na jinai zake nyengine nyingi.***

Yazid bin Muawiya

 

Katika siku kama ya leo miaka 133 iliyopita, alizaliwa Dakta Rajendra Prasad, mwanasiasa na mwanafalsafa wa India huko katika mojawapo ya vijiji vya jimbo la Bihar. Rajenda Prasad aliweza kuendelea na masomo na kufikia daraja ya udaktari, licha ya hali duni ya kifedha ya familia yake. Aidha alishiriki na wananchi wa India katika mapambano ya kupigania uhuru wa nchi yao. Prasad vilevile alishirikiana bega kwa bega na Mahatma Gandhi katika mapambano ya kisiasa dhidi ya wakoloni wa Kiingereza na kwa mara kadhaa aliteuliwa kuongoza chama cha Congress ya Kitaifa ya India. Rajendra Prasad aliteuliwa kuwa Rais wa kwanza wa India baada ya uhuru wa nchi hiyo na kuasisiwa mfumo wa jamhuri nchini humo mwaka 1950. ***

Rajendra Prasad,

Miaka 98 iliyopita katika siku kama ya leo, Auguste Renoir mchoraji mkubwa wa Kifaransa aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 78. Renoir alizaliwa tarehe 7 Machi 1841 na kwa haraka mno aliweza kuonyesha dhuku na mapenzi yake kwa taaluma ya uchoraji. Akiwa na umri wa miaka 19 tayari Auguste Renoir alikuwa ameshaondokea kuwa mchoraji mahiri na mashuhuri mjini Paris. ***

Auguste Renoir

Katika siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilipasishwa kwa wingi wa kura za wananchi. Katiba hiyo inasisitiza juu ya kuzingatiwa thamani za Kiislamu, uadilifu wa kijamii na kuheshimiwa haki za binadamu. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, katika mwaka 1368 Hijria Shamsiya, kipengee cha ziada kiliongezwa kwenye katiba hiyo, baada ya kupasishwa na Baraza la Wataalamu linalomteuwa Kiongozi Mkuu wa Iran na kuidhinishwa pia na wananchi. Kwa mujibu wa kipengee hicho cha nyongeza, katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi sasa ina vipengee 14 na vifungu 177. ***

Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, kulitokea janga kubwa la kuvuja gesi ya kemikali katika kiwanda kimoja cha Marekani katika mji wa Bhopal huko katikati mwa India. Kiwanda hicho kilikuwa kikimilikiwa na kampuni ya Kimarekani iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Union Carbide. Uzembe wa maafisa wa kiwanda hicho na kutozingatiwa viwango vya usalama ulipelekea kuvuja kwa gesi ya sumu ya sianidi (cyanide) kutoka katika kiwanda hicho na kuenea katika hewa. Maelfu ya wakazi mji wa Bhopal walipoteza maisha na mamia ya wengine kujeruhiwa katika janga hilo ambalo lilitambuliwa kuwa janga kubwa zaidi la viwandani duniani. ***

Janga la kuvuja gesi ya kemikali

Na miaka 30 iliyopita katika siku kama ya leo, kombora la kwanza la balestiki lililotengenezwa katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilifanyiwa majaribio kwa mafanikio wakati wa vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Saddam Hussein dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika kipindi hicho ambapo Iran ilikuwa chini ya vikwazo vikali vya nchi za Magharibi huku ikipigana na adui kulinda ardhi yake, awamu ya kwanza ya majaribio ya kombora hilo ilifanyika kwa mafanikio na uzalishaji wake ukaanza wakati wa vita vya Saddam Hussein dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. ***

Kombora la balestiki