Jumatano, Disemba 6, 2017
Leo ni Jumatano tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1439 Hijria sawa na 6 Disemba, 2017.
Siku kama ya leo miaka 1492 iliyopita kwa mujibu wa nukuu za maulama wengi wa Kiislamu, alizaliwa Mtume Muhammad (saw) katika mji mtakatifu wa Makka. Baba yake, Abdullah alifariki dunia kabla ya kuzaliwa Mtume na mama yake, Amina binti Wahab, alifariki dunia mtukufu huyo akiwa na umri wa miaka sita. Katika kipindi cha mwanzoni mwa ujana wake Muhammad alikuwa akijitenga na jamii ya kijahilia ya watu wa Makka na kwenda kwenye pango la Hiraa lililoko karibu na mji wa Makka na kuketi huko kwa masaa kadhaa akitafakari katika maumbile ya dunia na kufanya ibada. Malaika Jibrilu alimteremkia mtukufu huyo akiwa katika pango hilo na kumpa ujumbe wa Mola Muumba. Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw) alikumbana na mashaka mengi katika jitihada zake za kufuta ibada ya masanamu na kueneza imani ya Tauhidi na kumwabudu Mungu Mmoja.

Siku kama hii ya terehe 17 Rabiul Awwal miaka 1356 iliyopita pia alizaliwa mjukuu wa mtukufu huyo Imam Ja'far Swadiq (as) katika mji mtakatifu wa Madina. Kipindi cha maisha yake kilikuwa zama za kuchanua elimu na maarifa, tafsiri ya Qur'ani na kusambaa elimu mbalimbali. Imam Sadiq (as) alitumia fursa hiyo ambayo ilisadifiana na kuanza kuporomoka utawala wa Bani Umayyah na kuchukua madaraka utawala wa Bani Abbas, kwa ajili ya kueneza maarifa asili ya Kiislamu na kulea kizazi cha wasomi na maulama katika nyanja mbalimbali. Kwa minasaba hii adhimu Idhaa ya Kiswahili Redio Tehran inatoa mkono wa baraka kwa Waislamu wote duniani.

Miaka 239 iliyopita katika siku kama ya leo, sawa na tarehe 6 Disemba mwaka 1778, alizaliwa Joseph Louis Gay-Lussac mwanafizikia na mwanakemia wa Ufaransa. Gay-Lussac amefanya tafiti nyingi na kugundua vitu tofauti katika kipindi cha maisha yake. Miongoni mwa aliyoyagundua mwanakemia huyo ni gesi ya sumu ya halogen, kipimio cha ulevi, hydromita au chombo cha kupimia uzito wa maji na viowevu na kuitambua Chloride na Iodine kama elementi mpya. Miongoni mwa kazi zake muhimu za kisayansi alizofanya mwanakemia huyo ni kuweka kanuni ya kupanuka kwa gesi. Kanuni hiyo iliyopewa jina lake pamoja na la mshirika wake ilijulikana kama Law of Charles and Lussac. Gay-Lussac alifariki dunia mwaka 1850.
Miaka 100 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Finland iliyokuwa chini ya utawala wa Russia ilijipatia uhuru wake. Kuwa jirani Finland na Russia kuliwatia wasi wasi mno viongozi wa Finland, kiasi kwamba, katika karne ya 12 Miladia, waliiomba Sweden iwahami dhidi ya Moscow. Hata hivyo, Wasweden wakaikalia kwa mabavu Finland. Mwaka 1721 Russia iliivamia Finland na kudhibiti sehemu ya ardhi ya nchi hiyo. Hatimaye mwaka 1917 vikosi vamizi vya Russia vililazimika kuondoka nchini Finland na nchi hiyo ikajitangazia uhuru.
Katika siku kama hii ya leo miaka 27 iliyopita alifariki dunia Jahan Beglu, profesa wa miziki ya kiasili ya Kiirani akiwa na umri wa mia 62. Profesa Jahan Beglu alizaliwa mwaka 1307 Hijria Shamsia Mwanamuziki huyo wa miziki ya kiasili alijifunza sanaa ya muziki kutoka kwa wasomi wakubwa wa tasnia hiyo na kisha akaelekea Austria na kupata shahada ya juu zaidi katika fani hiyo. Alirudi nchini na kuwasaidia wanafunzi wengi kufanya utafiti na kukuza tasnia hiyo.
Siku kama ya leo 25 iliyopita, Wahindu wenye misimamo mikali waliubomoa Msikiti wa Babri katika mji wa Faizabad kwenye jimbo la Uttar Pradesh nchini India. Msikiti huo ulijengwa mwaka 1528 na Zahiruddin Muhammad Babur juu ya kilima na tangu wakati huo ulijulikana kwa jina la Msikiti wa Babri. Baada ya kupita karne tatu tangu ujengwe yaani mwaka 1855, mtawala mmoja Muingereza alipotosha ukweli kwa makusudi na kuandika kuwa msikiti huo umejengwa kwenye magofu ya jumba la ibada ya masanamu la Wahindu. Suala hilo lilikuwa chanzo cha fitina na ugomvi mkubwa kati ya Waislamu na Wahindu. Mwaka 1992 Wahindu wenye misimamo ya kufurutu mipaka walivamia Msikiti wa Babri na kuubomoa kikamilifu, suala ambalo lilizusha vita baina ya Waislamu na Wahindu.