Dec 08, 2017 12:55 UTC
  • Ijumaa 8 Disemba, 2017

Leo ni Ijumaa tarehe 19 Mfunguo Sita mwaka 1439 Hijria sawa na tarehe 8 Disemba 2017.

Miaka 149 iliyopita mwafaka na leo, ulianguka utawala wa Washugani au kwa jina jingine watawala wa kijeshi huko Japan. Kuanguka kwa utawala huo kulipelekea kuanza kwa marekebisho ya kijamii, kisiasa na kiutamaduni nchini humo. Washugani walikuwa moja kati ya makumi ya silsila zenye nguvu huko Japan, walioanzisha utawala wao wa kidikteta tangu karne ya 12 Miladia.

Mtawala wa zamani wa Japan

Miaka 114 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Herbert Spencer mwanafikra na mwanafilosofia wa Kiingereza. Spencer aliazaliwa mwaka 1820 Miladia na kujifunza elimu mbalimbali kutoka kwa baba yake. Aidha alijiongezea ujuzi wa kielimu kutokana na juhudi zake za kupenda kutalii mambo. Herber Spencer aliamini kuwa, mtu anaweza kujipatia elimu kwa kushuhudia na kupata uzoefu.

Herbert Spencer

Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita yalijiri mapigano ya baharini ya Falklands pambizoni mwa visiwa vya Falklands katika bahari ya Atlantic kati ya Uingereza na Ujerumani. Vikosi vya wanamaji vya Ujerumani vilipigwa vibaya na vile vya Uingereza na kupelekea visiwa hivyo kwa mara nyingine tena kuwa chini ya himaya ya Waingereza.

Mapigano ya baharini ya Falklands

Na miaka 68 iliyopita katika siku kama ya leo, Chian Kai-shek kiongozi wa wapigania uhuru wa China alikimbilia Taiwan akiwa na wafuasi wake wengi baada ya kushindwa na wapiganaji wa chama cha Kikomonisti chini ya uongozi wa Mao Tse Tung na kuunda serikali ya kitaifa ya Uchina. Uungaji mkono wa Marekani kwa kiongozi huyo wakati huo ulipelekea Taiwan kujitenga na Uchina na kiti cha nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama kikapatiwa Taiwan.

Chian Kai-shek