Dec 13, 2017 12:58 UTC
  • Jumatano tarehe 13 Disemba 2017

Leo ni Jumatano tarehe 24 Rabiul Awwal 1439 Hijria sawa na 13 Disemba, 2017.

Katika siku kama ya leo miaka 14 iliyopita, Saddam Hussein, dikteta wa zamani wa Iraq alitiwa mbaroni akiwa katika maficho yake karibu na Tikrit huko kaskazini mwa Baghdad. Saddam alijificha katika eneo hilo baada ya Iraq kuvamiwa na majeshi ya Marekani na Uingereza mwezi Machi 2003. Kutiwa nguvuni dikteta huyo wa Iraq aliyemwaga damu za raia wengi wa nchi hiyo kuliwafurahisha sana Wairaki na nchi kama vile Iran na Kuwait ambazo zimepatwa na maafa makubwa kutokana na udhalimu za Saddam Hussein dhidi ya nchi hizo. Katika upande mwingine, pamoja na kuwa walimwengu walikuwa wakisubiri kwa hamu kusikia jinai zilizotendwa na dikteta huyo wa zamani wa Iraq wakati wa utawala wake, Marekani ilimweka dikteta huyo chini ya uangalizi wake baada ya kumtia nguvuni lengo likiwa ni kuzuia kufichuliwa ushirikiano wa karibu uliokuwapo kati ya dikteta huyo na serikali za Magharibi khususan ikulu ya Marekani ya White House.

صدام حسین

Katika siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, Sheikh Mahmoud Shaltut Mkuu wa Chuo Kikuu cha Al Azhar na Mufti Mkuu wa Misri aliaga dunia. Mwanazuoni huyu mkubwa wa Misri alizaliwa mwaka 1892 nchini Misri. Akiwa na umri wa miaka 14 alianza masomo ya shule ya upili katika Chuo cha Kidini cha Alexandria. Alipata chetu cha chuo kikuu mwaka 1918 na kuanza kufunza katika chuo hicho hicho na kisha alihamia Chuo Kikuu cha al Azhar mwaka 1927. Alizidi kupanda cheti kielimu na kuteuliwa kuwa mwanachama wa Baraza la Fatwa chuoni hapo. Mwaka 1958 aliteuliwa kuwa mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Al Azhar ambapo alitoa huduma kubwa. Kati ya hatua muhimu alizochukua Sheikh Shaltut katika kipindi cha uongozi wake ni jitihada za kuimarisha umoja na ukuruba baina ya madhehebu za Kiislamu. Baada ya kuandikiana barua kadhaa na Ayatulahil Udhma Borujerdi, marjaa mkubwa wa Kishia, Sheikh Shaltut alitambua rasmi Madhehebu ya Shia Ithnaashari. Aliamuru madhehebu ya Shia yafunzwe katika Chuo Kikuu cha Al Azhar sawa na madhehebu zingine za Kiislamu. Vilevile alitoa fatwa mashuhuri na kusema kuwa inajuzu kwa Mwislamu atakaye,  kufuata madhehebu ya Shia Ja'fariya. Sheikh Shaltut aliaga dunia mwaka 1963 akiwa na umri wa miaka 72.

Sheikh Mahmoud Shaltut

Katika siku kama ya leo miaka 92 iliyopita, Majlisi ya Waasisi nchini Iran ambayo iliundwa kwa ajili ya kuhamisha mfumo wa kisultani kutoka silsila ya Qajar hadi utawala wa kifalme wa Pahlavi, ilitekeleza kazi yake kwa kufanya mabadiliko ya kimsingi katika Katiba ya Iran. Kwa msingi huo utawala wa miaka 153 wa wafalme wa Kiqajari nchini Iran ulifikia kikomo na badala yake ukaanza utawala wa miaka 53 wa Pahlavi hapa nchini.

Majlisi ya Waasisi nchini Iran

Na miaka 123 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo, alifariki dunia mmoja wa maraaji' wakubwa wa Kiislamu Ayatullah Mirza Habibullahi Rashti. Katika uhai wake alielekea mjini Najaf, Iraq kwa ajili ya masomo ya dini na kuhudhuria masomo ya Sheikh Murtadha Ansari. Ayatullah Mirza Habibullahi Rashti alitokea kuwa mmoja wa maulamaa wakubwa katika mji mtakatifu wa Najaf. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni pamoja na"Badaiul Afkar, al Imama na al Iltiqaat. 

Ayatullah Mirza Habibullahi Rashti