Alkhamisi, Disemba 14, 2017
Leo ni Alkhamisi tarehe 25 Rabiul Awwal 1439 Hijria sawa na Disemba 14, 2017.
Katika siku kama ya leo miaka 22 iliyopita, makubaliano ya amani ya Bosnia yaliyojulikana kwa jina la "Dayton Peace Agreement" yaani Makubaliano ya Amani ya Dayton" yalithibitishwa kwa mara ya mwisho katika kikao kilichofanyika mjini Paris, Ufaransa. Makubaliano hayo ambayo yalifanyika kwa mashinikizo ya viongozi wa Marekani tarehe 21 Novemba 1995, yalitiwa saini na Marais wa wakati huo wa Bosnia Herzegovina, Serbia na Croatia. Mafanikio pekee ya makubaliano hayo kwa upande wa Waislamu, yalikuwa ni kuhitimishwa mauaji ya kinyama yaliyokuwa yakifanywa dhidi yao na Waserbia.
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 14 Disemba 1981 Bunge la utawala haramu wa Israel 'Knesset' liliiunganisha rasmi miinuko ya Golan ya huko Syria na ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu. Hatua hiyo ya kinyama ilikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa nchi za Kiislamu, Kiarabu pamoja na jamii ya kimataifa. Utawala dhalimu wa Israel uliikalia kwa mabavu miinuko hiyo ya Golan ya Syria katika vita baina yake na Waarabu mwaka 1967.
Miaka 106 iliyopita inayosadifiana na tarehe 14 Disemba 1911, baada ya juhudi na jitihada za miaka mingi, hatimaye Ncha ya Kusini yaani South Pole ilivumbuliwa na kwa mara ya kwanza na wavumbuzi kadhaa waliwasili katika eneo hilo. Katika siku hii, Roald Amundsen baharia mashuhuri wa Kinorway aliyekuwa akishindana na Robert Falcon Scott wa Uingereza ili kuifikia ncha hiyo ya kusini, aliibuka mshindi na kuitundika bendera ya Norway katika ncha hiyo. Robert Falcon Scott akiwa na wenzake walikumbana na theluji kali wakati wanarejea na kupoteza maisha yao.
Miaka 212 iliyopita katika siku kama ya leo, sawa na 14 Disemba 1805, iligunduliwa nishati ya joto ya makaa ya mawe na George Branclon, mhunzi kutoka Uingereza. Kabla ya hapo, makaa ya mawe yalikuwa yakitumiwa kama mojawapo ya vifaa vya kujengea nyumba. Shehena ya kwanza ya madini ya makaa ya mawe yaliyotumiwa katika nishati ya joto, ilipatikana katika bandari moja iliyoko Uingereza.
Siku kama ya leo miaka 1003 iliyopia sawa na tarehe 25 Rabiul Awwal mwaka 436 Hijiria alifariki dunia Ali Bin Hussein Baghdadi maarufu kama Sayyid Murtadha fakihi na alimu mkubwa wa Kiislamu. Sayyid Murtadha aliyejulikana pia kwa kwa lakabu ya Alamul Huda. Alizaliwa mwaka 355 Hijiria huko Baghdad na alijifunza elimu za fasihi ya Kiarabu, mantiqi na mashairi na kwa miaka 30 alihukumu mjini Baghdad. Sayyid Murtadha ameacha vitabu vingi na miongoni mwa vitabu hivyo ni Tanzihil Anbiyah, Taqribul Usul pamoja na kitabu cha maashairi chenya beti elfu 20.