Ijumaa, Disemba 15, 2017
Leo ni Ijumaa tarehe 26, Mfunguo Sita, Rabiul Awwal, 1439 Hijria sawa na Disemba 15, 2017 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1095 iliyopita alifariki dunia Ebn-e Sammak, mtaalamu mkubwa wa hadithi mjini Baghdad, Iraq. Hata hivyo historia haijaweka wazi tarehe na mahala alipozaliwa msomi huyo mkubwa, lakini jambo linalofahamika ni kwamba msomi huyo aliishi mjini Baghdadi katika himaya ya wasomi wa mji huo, pia msomi huyo naye alipata kuwalea wasomi wengine mashuhuri akiwemo Hakim Nishaburi.
Miongoni mwa vitabu vya Ebn-e Sammak ni kitabu cha "al Aamal" na vitabu vingine kadhaa kuhusu fadhila za Mtukufu Mtume Muhammad (saw).

Miaka 61 iliyopita muwafaka na leo alifariki dunia Walt Disney shakhsiya mashuhuri wa sekta ya filamu za watoto. Disney alizaliwa mwaka 1901 huko Marekani. Walt Disney alihitimu masomo katika Chuo Kikuu cha Havard na kutunukiwa shahada ya udaktari katika sayansi ya uchoraji na uchongaji (Fine Art). Disney alitoa mchango mkubwa katika kuimarisha sanaa ya filamu za katuni. Mara kadhaa alitunukiwa tuzo za Oscar katika uwanja huo wa kutengeneza filamu za katuni.
Na miaka 42 iliyopita sawa na leo, yaani tarehe 15 Disemba 1975, zilimalizika zama za udhibiti na ushawishi wa Uhispania huko Sahara ya Magharibi baada ya nchi hiyo kulazimika kuondoka katika eneo hilo. Polisario ni moja ya harakati za ukombozi wa Sahara Magharibi iliyowalazimisha Wahispania kukimbia eneo hilo. Harakati hiyo iliundwa mwaka 1973 baada ya wanamapinduzi wa Sahara kuasisi makundi kadhaa ya kupigania ukombozi wa eneo hilo.