Jumatatu tarehe 18 Disemba 2017
Leo ni Jumatatu tarehe 29 Rabiul Awwal 1439 Hijria sawa na tarehe 18 Disemba 2017.
Miaka 115 iliyopita katika siku kama ya leo, kituo cha kwanza cha redio duniani kiliasisiwa na Guglielmo Marconi, mvumbuzi na mbunifu wa Kiitalia. Kwa utaratibu huo, kukaweko mawasiliano ya haraka baina ya Ulaya na Amerika. Katika zama hizo redio ilikuwa ikitumiwa zaidi kama chombo cha mafunzo. Marconi alifikia hatua hiyo kutokana na bidii na shauku kubwa aliyokuwa nayo tangu awali ya kufanya utafiti katika uwanja huo.
Miaka 103 iliyopita katika siku kama ya leo, Uingereza iliikoloni rasmi Misri. Inafaa kukumbusha kwamba, wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia, utawala wa Othmania ulikuwa mwitifaki wa madola yaliyokuwa yakiipinga Uingereza yaani Ujerumani na Austria. Uingereza nayo ikiwa na lengo la kukabiliana na kitendo hicho, iliikalia kwa mabavu Misri, ambayo hadi katika kipindi hicho ilikuwa chini ya udhibiti na utawala wa Othmania. Harakati za ukombozi za wananchi wa Misri dhidi ya mkoloni Mwingereza zilizaa matunda mwaka 1922, ambapo nchi hiyo ilijitangazia uhuru wake.
Siku kama ya leo miaka 94 iliyopita, alifariki dunia alimu na mtaalamu wa elimu ya fikihi Ayatullah Sayyid Muhammad Firuzabad. Sayyid Muhammad Firuzabadi Najafi, alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi wa Akhund Khorasani na Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi. Sayyid Muhammad Firuzabadi alikuwa marjaa wa Waislamu wa Kishia enzi za uhai wake. Mwanazuoni huyo alifariki dunia usiku wa mwisho wa mwezi Rabiul-Awwal mwaka 1345 Hijiria mjini Samarra, Iraq na kuzikwa mjini Najaf. Kitabu cha ‘Jaamiul-Kalim Fi Hukmil-Libaasil-Mashkuuk’ ni miongoni mwa athari za msomi huyo.
Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita msomi wa Ujerumani, Otto Hahn, alifanikiwa kupasua kiini cha atomu, hatua ambayo ilikuwa mwanzo wa zama za atomu. Mtaalamu huyo wa kemia alizaliwa mwaka 1879 huko Frankfurt na kupata shahada ya uzamivu katika taaluma ya kemia. Tangu wakati huo alijishughulisha na utafiti katika taaluma fizikia. Baada ya utafiti mkubwa na katika siku kama hii ya leo Otto Hahn alifanikiwa kupasua kiini cha atomu. Hatua hiyo iliibua nishati kubwa ambayo baadaye ilianza kutumika katika vinu na mabomu ya nyuklia. Mwaka 1944 Otto Hahn alitunikiwa tuzo ya Nobel katika taaluma ya kemia.
Tarehe 18 Disemba miaka 38 iliyopita Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha makubaliano ya kufuta aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake. Makubaliano hayo yana lengo la kuondoa dhulma zinazofanywa dhidi ya wanawake duniani. Hata hivyo makubaliano hayo, kama yalivyo mengine mengi ya kimataifa, yanatawaliwa na mitazamo ya kimaada ya Magharibi inayosisitiza usawa wa jinsia mbili za mwanamke na mwanaume katika kila kitu. Hii ni katika hali ambayo mwanamke na mwanaume wanatofautiana kimwili na kiroho. Kwa sababu hiyo dini za Mwenyezi Mungu hususan Uislamu zinasisitiza kuwa njia ya kuwakomboa wanawake ni kuwatayarishia mazingira ya uadilifu kwa kutilia maanani uwezo wao wa kimwili na kiroho.

Na siku kama ya leo miaka 38 iliyopita na katika siku kama ya leo, Dakta Muhammad Mufatteh alimu, mwanaharakati na mwanamapambano wa Kiirani aliuawa shahidi na makundi ya kigaidi. Baada ya kumaliza masomo yake ya kimsingi alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Qum. Sambamba na kusoma masomo ya dini, Muhammad Mufatteh alikuwa akisoma pia katika Chuo Kikuu cha Tehran na kufanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika falsafa yaani PHD. Baada ya kupata shahada hiyo akaanza kufundisha kama mhadhiri huku akiendesha harakati za mapambano dhidi ya utawala dhalimu wa Shah uliokuwa ukitawala hapa nchini Iran.