Dec 22, 2017 23:19 UTC
  • Jumamosi, Disemba 23, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe 4 Mfunguo Saba Rabiu Thani 1439 Hijria sawa na tarehe 23 Disemba 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1266 iliyopita yaani tarehe 4 Mfunguo Saba Rabiu Thani 173 Hijria, alizaliwa Sayyid Abdul Adhim al Hassani mmoja wa wajukuu wa Imam Hassan al Mujtaba (a.s) huko katika mji wa Madina. Sayyid Abdul Adhim Hassani alikuwa mcha Mungu na msomi. Alikuwa mmoja kati ya shakhsia walioaminiwa na Imam al Hadi (as) na alinukuu hadithi moja kwa moja kutoka kwa Maimamu watukufu kama vile Imam Ridha, Jawad na al Hadi (as). Sayyid Abdul Adhim Hassani alihamia Iran kutokana na pendekezo la Imam al Hadi (as) kwa ajili ya kuwaongoza Waislamu na akaishi katika mji wa Rei karibu na Tehran ya sasa. Sayyid Abdul Adhim Hassani aliuawa shahidi mwezi Shawwal mwaka 250 Hijria. Kaburi la mtukufu huyo liko katika mji wa Rei na ni miongoni mwa maeneo ambayo Waislamu kutoka maeneo mbalimbali duniani wanayazuru na kuyatembelea. ***

Haram ya Mtukufu Abdul Adhim Hassani

 

Katika siku kama ya leo miaka 926 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa mjini Baghdad Abubakar Muhammad Anbari, faqihi, mtaalamu wa hadithi na lugha. Anbari alisoma elimu ya dini, nahwu na lugha akiwa kijana mdogo kutoka kwa baba yake. Baada ya kuhitimu masomo yake katika nyanja tofauti, alianza kufundisha na kulea wanafunzi wengi. Alitokea kuwa faqihi mkubwa na kutabahari katika elimu ya lugha ya Kiarabu. Msomi huyo ameandika vitabu vingi maarufu zaidi kikiwa ni kitabu cha ‘Manshurul-Fawaaid.' ***

Abubakar Muhammad Anbari

 

Miaka 69 iliyopita katika siku kama ya leo, watu saba miongoni mwa viongozi mashuhuri wa Japan wakati wa Vita vya Pili vya Dunia walinyongwa, kufuatia hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Tokyo. Mahakama hiyo ambayo iliundwa ikiwa ni katika muendelezo wa mahakama ya Nuremberg ya Ujerumani ili kuwahukumu watenda jinai za kivita huko Japan, iliwahukumu viongozi 25 wa Japan ambapo 18 kati yao walihukumiwa kwenda jela. Waziri Mkuu wa wakati huo wa Japan, alikuwa kiongozi wa ngazi za juu zaidi aliyefikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Tokyo na kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa. ***

Hideki Tojo

 

Na siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, mkuu wa zamani wa shirika la kuogofya la usalama na la siri la Urusi ya zamani ambaye pia alikuwa kiongozi nambari mbili wa nchi hiyo katika zama za Joseph Stalin, Lavrentiy Pavlovicha Beria, alihukumiwa kifo na kunyongwa kwa tuhuma za kwenda kinyume na misingi ya sheria za Chama cha Kikomonisti sambamba na kufanya njama dhidi ya serikali. Katika kipindi cha utawala wa Stalin, Pavlovicha Beria alitoa amri ya kuuliwa watu wengi na akafanya umwagaji damu ndani ya Chama cha Kikomonisti na katika Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani. ***

Lavrentiy Pavlovicha Beria